Barack Obama aliapoapishwa rasmi kwa mara ya kwanza kama rais wa 44 wa Marekani siku ya Jumanne ya Januari 20, 2009, dunia nzima ilifurahi na kusisimka kumuona mtu mweusi wa kwanza akiingia Ikulu ya White House kuanza miaka yake minne ya utawala.
Miongoni mwa watu waliofurahishwa na tukio hilo alikuwa ni Mama Catherine Ringo wa Tanzania ambaye siku hiyo hiyo, na wakati ule ule Rais Obama anakula kiapo ndipo alipojifungua mtoto wa kiume katika hospitali ya TMJ jijini Dar es salaam.
“Wauguzi wa TMJ wakiongozwa na Dokta Erasto walifurahi na kusimkwa sana kwa kuzaliwa mwanangu huyo nao wote wakampa jina la Baraka Obama hapo hapo kitandani”, anasema Mama Ringo ambaye ni mfanyakazi wa TRA.
“Yaani we acha tu”, anaongezea.
“Mie mwenyewe kwanza nampenda sana (Rais) Obama. Nilikuwa nafuatilia katika TV kila hatua za kampeni yake, saa ingine hadi usiku wa manane, kiasi hata mume wangu alikuwa akinisema.
“Wakati wa uja uzito, hasa hasa siku za mwishoni mwa kampeni ambazo na kwangu zilikuwa siku za lala salama kabla ya kujifungua nilikuwa sikosi kuangalia kampeni ilivyopamba moto.
"Na niliposikia (Rais) Obama kashinda kwa kishindo sikuamini masikio yangu…Mswahili kuingia White House??? Ilikuwa kama ndoto.
“Ilipofika siku ya kuapa kwake name machungu yakanianza na muda wa kuapa wenyewe sikuweza kuona maana nilikuwa leba na mara mtoto alipozaliwa nikamsikia Dokta Erasto anasema kwa furaja ni Obama! Ni Obama!” nikajua nimejifungua mtoto wa kiume.
“Cha ajabu kingine ni kwamba hapo TMJ nilikuwa nimelazwa katika chumba namba 20 wakati wa kujifungua mwanangu’, anasema Mama Ringo. Baraka hivi sasa ana umri wa miaka minne na ushee na anasoma shule ya vidudu ya Sunrise Nursery School iliko Kinondoni Morocco jijini Dar es salaam.
“Hata yeye mtoto anampenda sana (Rais) Obama na akimuona kwenye TV ama magazeti anasema Mama ona Obama…Obama… Obama..ile…” anaongezea Mama Ringo ambaye furaha hiyo iliendelea Mnamo Januari 21, mwaka huu wakati Rais Obama alipoapa kwa mara ya pili baada ya kushinda uchaguzi kwa mara ya pili.
Siku hiyo alinunua kreti tatu za soda na kuwagawia marafiki zake ofisini pamoja na mawakala wa mizigo ambao wote wanamwita Mama Obama akiwa kazini.
Mama Ringo ni mmoja wa Watanzania mwenye kujisikia raha sana kwa kusikia Rais Obama atazuru Tanzania mwezi Ujao.
“Yaani we acha tu. Nafurahi kweli kuwa wajina wa mtoto wangu anakuja na nikipata ngekewa ya kumwona hata kwa mbali tu nitafurahi sana sana.
“Ila nitafurahi zaidi kama ,mwanangu atakutana naye ana kwa ana wajina wake huyo.
Najua ni ngumu lakini huwezi kujua…..”anamalizia Mama Baraka Obama ambaye pia ana binti mwenye umri wa miaka minane aitwaye Dabriah.
Mama Catherine Ringo a.k.a Mama Obama akiongea na Globu ya Jamii jijini Dar es salaam
Kadi ya kliniki ya mtoto Baraka Obama
Baraka Obama akiwa na umri wa miezi mitatu
Obama akiwa na umri wa miaka minne na miezi kadhaa
Obama akiwa na dada yake Dabriah
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...