Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni katika lugha Kiingereza na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kusema rasimu hiyo haitoi tafsiri sahihi ya maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal Juni 3 mwaka huu (2013).
Rasimu hiyo iliyotolewa na LHRC ambayo inasambazwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, pia inatumika katika mikutano na warsha mbalimbali zinazojadili kwa lengo la kutoa maoni kuhusu Rasimu iliyotolewa na Tume.
“Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi na wadau wengine kuwa Rasimu hiyo ya Katiba katika lugha ya kiingereza iliyoandaliwa na LHRC haitoi tafsiri sahihi ya maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume katika lugha ya Kiswahili na hivyo kupotosha umma kuhusu maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni,” amesema Katibu wa Tume hiyo, Bw. Assaa Rashid katika taarifa yake kwa Vyombo vya Habari leo (Julai 9, 2013).
Bw. Asaa amewataka wananchi kuendelea kusoma na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika lugha ya Kiswahili ambayo amesema imesambazwa kwa wananchi, taasisi, jumuiya na taasisi mbalimbali. Rasimu hiyo pia inapatikana katika tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) na kutolewa bure katika Ofisi za Tume zilizopo Dar es Salaam na Zanzibar.
Aidha, Tume hiyo imesema iliandaa Rasimu ya Katiba katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi ambao wengi wao wanajua kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili kuelewa maudhui ya Rasimu hiyo.
Katika taarifa yake, Tume imewataka wadau wote wanaotaka kutafsiri Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume kuwasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina Wataalamu wa Uandishi wa Sheria (Legislative Drafters).


.bmp)
hatuhitaji kiingereza kwenye katiba yetu kwani kiswahili ndiyo lugha yetu. Naunga mkono tume kwa kutoa tahadhari hiyo kwa wananchi.
ReplyDeleteWanaojadili katiba ni watanzania yani waswahili; hatuhitaji kiingereza.
Kwa nini watu wanataka kuiga kila kila kitu? Siamini kama kuna Mtz anataka rasimu ya katiba au katiba yenyewe iliyoandikwa kwa lugha ya kigeni,Kiswahili chetu kinatufaa sana na hatuhitaji kiingereza ktk katiba mpya,Tujivunie Kiswahili chetu. Tembea kokote iwe India,China,Ujerumani,Uberigiji,Hispania,Ufaransa,Italia na kwingineko kama utakuta nyaraka zao nyeti kama katiba ikiwa imeandikwa kwa lugha tofauti na lugha mama ya taifa husika
ReplyDeleteLazima wawatafsiria Wafadhili, pesa masihara??
ReplyDeleteKwani kuna mtanzania hajui Kiswahili hadi rasimu itafsiriwe kwa lugha ya kiingereza? Wabongo bwana!
ReplyDeleteKwa nn inapatikana Dar na Zanzibar tu kwani huko mikoani hawahitaji nakala? ama watanzania wako Dar tu.
ReplyDeleteNa nani hasa aliyetafsiri?mtajeni tumjue?kupoteza muda na hela za wananchi bure.wadau mbali mbali nakumbuka walishatoa maoni yao kabla hata ya rasimu wakipendekeza katiba iwe kwa lugha ya kiswahili sasa leo mnaanza kukanusha kanusha hapa maana yake nini?wakati mwengine mnaudhi sana jamani.
ReplyDeleteHawa LHRC wana matatizo sana hasa huyo Dr Helen Kijo. Yote hio ni kutafuta pesa ya wafadhili. Hatuhitaji hio english version. Sijui wakoje!
ReplyDelete