Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa Serikali itafanya kila iwezalo kuwakamata na kuwapeleka katika Vyombo vya sheria Watu waliohusika kuwamwagia Tindikali Raia wawili wa Uingereza hivi karibuni.

Amesema Vyombo vya Ulinzi na Usalama viko Imara na kwamba vitaendelea kulinda amani ya Nchi ikiwemo kuwabaini Wahalifu wote na kuwapeleka katika Vyombo husika.

Dkt Shein ameyasema hayo leo alipokuwa akiwahutubia Wananchi kupitia Baraza la Idd lililofanyika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Amesema kwa mara ya pili kila inapokaribia Sherehe za Sikukuu kumekuwa na mfululizo wa Matukio ya kihalifu na kuongeza kuwa kila aliyehusika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Vitendo hivi si uungwa ni Ukatili, hatutawatia hatiani Wasiohusika lakini kila aliyehusika hatutamsamehe” Alionya Dkt Shein.

Aidha Dkt. Shein amelaani kushamiri kwa Vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji hasa kwa Watoto ambapo jumla ya Watoto wakike 480 Zanzibar wamebakwa katika kipindi cha mwezi Julai 2012 hadi Aprili mwaka huu.

Amesema hilo ni jambo la kushtua sana na kwamba wakati umefika kila mmoja kuchukua hatua zinazofaa kudhibiti hali hiyo.

Dkt Shein ametoa wito kwa Wananchi na Viongozi wote kuendelea kupendana bila kuchukiana na kulinda Amani, Umoja na Kuvumiliana kwa manufaa ya Zanzibar.

Amesema panapotokea tofauti za hoja kuhusu suala la Maendeleo ya Nchi jambo la busara ni kuzungumza na kujadili kwa kuzingatia sheria zilizopo kwa manufaa ya Zanzibar.

Dkt Shein ametoa Shukrani kwa Jeshi la Polisi kwa kudumisha hali ya amani katika kipindi chote cha Mwezi wa Ramadhani na kulitaka Jeshi hilo lizidishe juhudi zake kipindi cha Sherehe za Idd na siku za usoni.

Kabla ya Baraza la Idd Dkt Shein alitoa Mkono wa Idd kwa Wazee na Watu wasiojiweza katika hafla iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Huu ufanyajikazi 'business as usual' ushapitwa na wakati, kwa nini maeneo yaliyo tete kwa wahalifu kama vile darajani, stonetown n.k yasiwekwe
    Closed-circuit television (CCTV) ili kuwatambua wahalifu. Kila siku ni lugha hio hio tu serikali itafanya kila liwezekanalo kuwakamata wahalifu, wamemkamata nani tokea mkurugenzi wa manispaa, sheikh soraga na sheha wa tomondo kumwagiwa acid? au ndio serikali haina fedha? lkn za kufanya sherehe za mapinduzi zipo. tunchoka bhana tunataka vitendo sasa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...