Shule ya Msingi Kumbukumbu iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni imekabidhiwa mradi wa maji safi ya kunywa wenye thamani ya zaidi ya Sh15Milioni uliotekelezwa na Klabu ya Rottary Mzizima. 
 Akizungumza mara baada ya kupokea mradi huo kutoka kwa Rais wa klabu hiyo, Ambrose Nshala katika hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo, Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge alisema mradi huo una umuhimu wa pekee kwa kuwa shule nyingi za Dar es Salaam hazina huduma za maji. 
 Alisema kutokana na hali hiyo wanafunzi wengi wamekuwa wakienda shuleni na vidumu vya maji kwa ajili ya matumizi ya vyooni kwa wanafunzi na hata walimu jambo ambalo linahatarisha afya zao kwani maji ya namna hiyo ni machache na yasiyokidhi mahitaji. 
 Songoro alisema mradi huo umewapata changamoto kwao kutokana na ukweli kuwa kiasi cha fedha kilichotumika ni kidogo kulinganisha na mradi wenyewe na kiwango hicho kisingewezekana kwa miradi inayotekelezwa na manispaa na mradi kama huo ungeweza kugharimu hadi Sh100 Milioni. 
 “Sheria ya manunuzi ni tatizo kwani kwa mradi huu ungeambiwa si chini ya Sh100Milioni zimetumika na hilo ni tatizo ambalo linakwamisha utekelezaji wa miradi mingi katika manispaa” alisema na kuongeza kuwa kuna miradi mingi utekelezaji wake umekwama kutokana na watalaam kuwasilisha bajeti zisizowezekana. 
 Awali akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo, Rais wa Rottary, Ambrose Nshala alisema mradi huo ambao unahusisha matenki ya maji ya lita zaidi ya 10,000 una mashine pia ya kusafisha maji na kuyafanya yawe salama kwa kunywa kwa watoto moja kwa moja kutoka bombani. Alisema mradi huo ni fedha zao wanachama na wahisani wengine na zingine zimetokana na mbio za hisani za Rottary Marathon na shule hiyo ni moja kati ya zingine 25 za Jijini Dar es Salaama ambazo zimesaidiwa kutatua kero mbalimbali na wahisani hao.
 Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kumbukumbu wakiwakaribisha wageni wakati wa hafla ya kukabidhi mradi wa maji uliofadhiliwa na Klabu ya Rottary Mzizima
 Rais wa Rottary Club Mzizima, Ambrose Nshala (kushoto), akiwasili katika Shule ya Msingi Kumbukumbu akiwa na Naibu Meya Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge wakati walipowasili shuleni hapo. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, John Maziku.
 Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kumbukumbu, John Maziku (kushoto), akitoa maelezo kwa Rais wa Rottary Club Mzizima Ambrose Nshala (wa pili kushoto), Naibu Meya manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge na Diwani wa Kata ya Kinondoni, Husna Hemedi kuhusiana na matenki ya kuhifadhia maji wakati wa kukabidhi mradi huo uliofadhiliwa na Rottary Club Mzizima, Dar es Salaam.
Rais wa Rottary Club Mzizima, Ambrose Nshala na Naibu Meya Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge wakikata utepe kuzindua mradi wa maji uliofadhiliwa na klabu hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...