Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati akizungumzia mkakati wa serikali wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote jana jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, Mhandisi Peter Ulanga (katikati) na Kulia ni Katibu wa Mfuko huo, Bi. Justina Mashiba.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote katika mwaka wa fedha wa 2013/14 inatarajia kuwafikishia wananchi waishio maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto wa kibiashara huduma ya mawasiliano ya simu ikiwa ni utekelezaji sera ya taifa ya utoaji huduma hiyo.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa aliwambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa serikali imejipanga kuwafikishia wananchi hao huduma hiyo muhimu kwa maendeleo.
“Tayari serikali imesaini mkataba na makampuni manne ya watoa huduma kujenga minara ya simu katika maeneo hayo,” alisema na kuongeza kuwa makampuni hayo ni pamoja na TTCL, Airtel, Vodacom na Tigo.
Alisema mwezi Machi 2013 Mfuko huo ulisaini mikataba na watoa huduma za mawasiliano ya simu wanne (4) walioshinda zabuni za kupeleka mawasiliano ya simu katika maeneo yasiyo na huduma za mawasiliano.
Alisema awamu ya kwanza itahusisha mikoa 14 na itagharimu Tshs bilioni 9.4 na ya pili mikoa 21 itakayogharimu Tshs bilioni 12.5 ambazo zitatolewa na serikali kama ruzuku na kiasi kinachobaki kitatolewa na watoa huduma hao.
Pi awamu ya tatu inalenga kufikisha huduma hiyo katika maeneo ya ndani zaidi ya vijiji ambavyo wakazi wake nyumba zao zipo mbalimbali na zabuni yake itatangazwa katika mwaka huu wa fedha 2013/14.
Akifafanua zaidi alisema utekelezaji wa Zabuni ya Kwanza na ya Pili unatarajia kunufaisha kata 284, vijiji 1,650 vyenye jumla ya wakazi 1,917,424.
Alitaja teknolojia rahisi na zenye kupunguza gharama zitakazo tumika kuwa ni pamoja na matumizi ya umeme jua, betri za magari na majenereta ya kutumia disel licha ya kukiri kuwa bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa nishati ya umeme.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga alisema kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme ni changamoto kubwa katika kuwafikishia huduma za mawasiliano wananchi wa vijijini na maeneo yasiyo na mvuto kibishara.
Alisisitiza kuwa uwekezaji wa umeme jua ni gharama kubwa lakini baada ya muda itakuwa rahisi sana.
Alisisitiza kuwa utekelezaji huo unaenda sambamba na matumizi ya teknolojia rahisi kwa kuangalia maeneo ya ndani sana na yenye wakazi wachache ili kupunguza gharama za kuweka minara.
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulianzishwa mwaka 2009 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mawsasiliano kwa madhumumuni ya kupeleka huduma ya mawasilano katika maeneo ya vijijini na yasiyo na mvuto kibiashara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...