Msemaji wa APRM Tanzania, Hassan Abbas akifafanua masuala mbalimbali kuhusu APRM na utafiti katika masuala ya kilimo kwa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Saint John cha Dodoma,wakati walipotembelea Banda la APRM kwenye Maonyesho ya Nane Nane,Mjini Dodoma.
MPANGO wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) tawi la Tanzania umesema moja ya changamoto kubwa iliyobainishwa katika maoni ya Watanzania kuhusu utawala bora nchini chini ya Mpango huo ni suala la utekelezaji wa miradi na mipango ya Serikali.
Kutokana na changamoto hiyo, Mpango huo umeeleza kufurahishwa na kitendo cha Serikali ya Tanzania kufanyiakazi haraka changamoto hiyo kwa kuchukua Mfumo wa Utekelezaji wa Malaysia (PEMANDU) ambao umetajwa kufanikiwa katika nchi kadhaa zilizoutekeleza.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo (Jumapili) kwenye Maonesho ya Wakulima, Nane Nane, yanayoendelea mjini Dodoma, Msemaji wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas alisema kitendo cha Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kuuchukua mfumo huo na kuuwekea mazingira ya Kitanzania chini ya dhana ya “MATOKEO MAKUBWA SASA” ni cha kupongezwa na kitaleta manufaa kwa nchi.
“Moja ya falsafa ya APRM kote Afrika ni kuzitaka nchi hizi kuheshimu umuhimu wa utafiti na hasa kujifunza kutokana na makosa lakini vile vile mafanikio ya nchi nyingine ndani na nje ya Bara hili.
“Mfumo wa utekelezaji wa miradi wa PEMANDU ni dhana iliyotekelezwa na kuonekana matokeo yake kuwa ni mazuri. Tanzania kwa hakika imefanya jambo kubwa kuchukua mfumo huu na tunaamini nchi nyingine wanachama wa APRM wakiona mafanikio ya hapa watachukua mfano huo kutoka Tanzania,” alisema Bw. Abbas.
Alisema APRM Tanzania itashirikiana na Kitengo cha Ufuatiliaji kilichoundwa chini ya Rais ili kwa pamoja kuhakikisha kuwa maeneo sita ya kuanzia yaliyobainishwa yanakuwa ni mfano adhimu kwa sekta na miradi mengine itakayoingizwa siku zijazo.
“Kwa kuwa kila mwaka APRM Tanzania itakuwa ikiandaa taarifa za utekelezaji wa masuala yaliyojitokeza katika Ripoti ya APRM na kujadiliwa mbele ya wakuu wa nchi zilizojiunga na APRM, tutashirikiana kwa karibu na Kitengo cha Ufuatiliaji ili mfumo huu wa MATOKEO MAKUBWA si tu ufanikiwe hapa nchini bali pia uwe moja ya maeneo ambayo Ripoti yetu ya kwanza itasaidia kuwavutia wenzetu wengine wa Afrika waje kujifunza kutoka Tanzania,” alidokeza.
Hata hivyo Bw. Abbas akishauri kuwa utekelezaji wa hatua hizi ni vyema ukashirikisha wananchi na taasisi nyingine za utafiti kama APRM ili kuupa mafanikio mfumo wa PEMANDU hapa nchini.
“APRM inasisitiza katika ushirikishaji na kwa kuwa APRM inashirikisha wananchi basi taasisi hizi mbili yaani APRM na Kitengo cha Ufuatiliaji kilichoanzishwa hapa nchini kutekeleza dhana ya PEMANDU zinapaswa kuwa chanda na pete,” alishauri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...