Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwafurahia wasanii chipukizi Gosbert Bwere(4) anayepiga ngoma na mwenzake Nyambari Mganga(5) walipokuwa wanamtumbuiza muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Nansio,Ukerewe, kwa ziara ya kikazi.
----------------------------------------
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa siyo kazi ya Serikali kuviokoa
vyama vya ushirika kutoka kwenye madeni kwa sababu shughuli za ushirika ni za
sekta binafsi na mali
ya wanachama wenyewe.
Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwa makosa ya ushirika na wezi wa baadhi
ya viongozi wa vyama vya ushirika hatimaye yanabebeshwa vyama vya siasa.
Kama namna ya
kuwasaidia wananchi, Rais Kikwete amewataka viongozi mbali mbali wa mikoa
kuwasaidia wananchi ili kupata viongozi waadilifu na waaminifu na wala siyo
wezi kama ilivyo sasa kwa vyama vingi vya
ushirika.
Rais Kikwete
ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Septemba 7, 2013, wakati
alipopokea Ripoti ya Maendeleo ya Mkoa wa Mwanza kwenye Ikulu Ndogo mjini
Mwanza kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo.
Rais Kikwete
aliwaambia viongozi hao wa Mkoa wa Mwanza: “Tumewahi huko nyuma kulipa madeni
yote ya vyama vya ushirika. Nia ilikuwa kuvisaidia vyama hivyo na wanachama
wake kujipanga upya na kupata uhalali wa kuweza kukopa fedha za kjuendesha
shughuli zao. Lakini sasa, vyama hivyo, vimerudi kule kule kwenye madeni.”
Alitoa mfano wa
Chama cha Ushirika cha Mkoa wa Pwani kama moja
ya vyama vya ushirika ambavyo madeni yake yalilipwa na Serikali lakini sasa
kina deni kubwa zaidi kuliko hata lile lililolipwa na Serikali.
“Wale watu wa
Pwani walikwenda kukopa na benki moja ikakubali kuwapa fedha. Wameshindwa
kulipa na ule ushirika nadhani utakufa. Njia bora kwa vyama vya namna hiyo ni
kuviachia vife tu kwa sababu havina faida yoyote kwa mkulima.”
Aliongeza:
“Vyama vya ushirika siyo mali
ya Serikali. Ni mali
ya wanaushirika na hivyo ushirika ni sekta binafsi. Lakini hakuna shaka kuwa
baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wanatesa wananchi. Wanakopa fedha
kwenye mabenki lakini wanashindwa kuzirudisha fedha hizo na hilo linapotokea Serikali inalaumiwa kwa hali
hiyo.”
Rais alikuwa
anatoa maelekezo yake baada ya kuambiwa kuwa Chama cha Ushirika cha Nyanza cha
Mkoa wa Mwanza kilikuwa kinakamilisha mpango wa kukopa kiasi cha sh bilioni
saba kutoka Benki ya Raslimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kununulia pamba.
Lakini
aliwaambia viongozi hao: “Uamuzi wa kukopa ama kutokukopa ni wa kwenu. Nyanza
ni mali
yenu, wezi waliopata kukibebesha madeni chama hicho mliwachagua nyie wenyewe.
Fedha ni zenu lakini hatimaye athari za makosa yenu yanaiathiri Serikali na
hata vyama vya siasa.”
“Kuna wakati
viongozi wa Chama cha Nyanza walipata kuuza godown ya thamani y ash milioni 600
kwa sh milioni 50 tu. Hawa ni wezi wa mchana wanaoiba kweupe. Wanaiba lakini
wanataka Serikali iwasaidie. Kwa nini? Nadhani kazi yetu kama
viongozi ni kuwasaidia wananchi kupata viongozi adilifu na aminifu siyo wezi,”
alisema Mheshimiwa Rais Kikwete na kuongeza:
“Tatizo ni kwamba
hata sisi viongozi tunakataa kuwashughulikia wezi kwa sababu hawa ni watu
maarufu na wakati mwingine baadhi ya viongozi wanakula nao na jambo hilo limekuwa tatizo kubwa sana . Tunavifikisha vyama vya ushirika mahali
ambako sina uhakika kama bado ni mali ya wakulima. Wakulima
wanakutana na ushirika wakati wa kuchagua viongozi tu na baada ya hapo wakulima
hawaonekani tena.”



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...