Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesifu maendeleo yaliyopatikana
katika skuli ya msingi ya ALI KHAMIS CAMP inayosimamiwa na Jeshi la Wananchi la
Tanzania (JWTZ).
Amesema skuli hiyo
imekuwa na maendeleo ya kupigiwa mfano kwa skuli za Tanzania, na kwamba
yamepatikana kutokana na umakini na nia njema ya jeshi hilo katika kuwapatia
watoto elimu bora. Maalim Seif ametoa
pongezi hizo katika skuli hiyo, wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi za
elimu kisiwani Pemba.
Aidha amesema
mafanikio hayo yamepatikana kutokana na mashirikiano makubwa yaliyopo kati ya
wananchi, Wizara ya elimu pamoja na Jeshi hilo, sambamba na nia njema iliyopo
katika kuwapatia wananchi maendeleo.
Amesema Jeshi la
Wananchi ni taasisi muhimu katika kuchangia maendeleo ya nchi, na kwamba vikosi
vya (14 na 151 KJ) vimeonyesha mwitikio mzuri wa kushirikiana na wananchi
katika jitihada za kujikwamua kimaendeleo.
Amesema Serikali
itaendelea kushirikiana na Jeshi hilo katika kuhakikisha kuwa linatimiza
malengo yake ya kuwapatia elimu pamoja na huduma za afya wananchi wa eneo hilo.
Katika ziara hiyo
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuchangia mifuko 50
ya saraji ndani ya kipindi cha wiki moja, ili kuchangia ujenzi wa skuli hiyo,
sambamba na kugharamia mafuta yatakayotumika kwa ajili ya usafishaji wa kiwanja
cha michezo kwa watoto katika eneo hilo.
Mapema Mwalimu Mkuu
wa Skuli hiyo Eugene Anathory Ruta amesema mafanikio ya skuli hiyo yamechangiwa
kwa kiasi kikubwa na ziara ya Makamu wa Kwanza wa Rais aliyoifanya katika skuli
hiyo mwezi Juni, mwaka huu.
Amesema tangu
kufanyika kwa ziara ya mwezi Juni, wafadhili kadhaa wamejitokeza kuchangia
maendeleo ya skuli hiyo, na kwamba sasa wana mpango wa kujenga skuli za
maandalizi na Sekondari ambazo tayari ujenzi wake umeanza hatua za msingi. Kwa upande wake
kamanda wa kikosi cha (14 KJ) J.K. Mbwelo amesema maendeleo ya skuli hiyo
hailengi kwa wanajeshi pekee bali kwa jamii nzima iliyowazunguka.
Kwa sasa wananchi
wengi wa maeneo ya Machomanne, Wawi na Vitongoji wamekuwa wakipatiwa huduma za
matibabu na elimu katika kituo cha afya ya skuli katika kambi hiyo ya Ali Khamis Camp. Maalim Seif pia
alitembelea skuli ya Sekondari ya Madungu na kuelezea kuridhishwa na maendeleo
ya skuli hiyo.
Wakati huo huo akiwa
katika skuli ya Fidel Castro, Makamu wa Kwanza wa Rais amepongeza hatua ya kutengezwa
na kujengwa upya kwa skuli hiyo, hatua ambao imeirejeshe hadhi yake ya asili. Ameuagiza uongozi wa
skuli hiyo kufanya kazi ya ziada, ili kuhakikisha kuwa ubora wa majengo
unakwenda sambamba na matokeo mazuri ya wanafunzi katika mitihani ya Taifa.
Nae Msaidi Mwalimu
Mkuu wa Skuli ya Fidel Castro. Khamis Rashid Nassor, amemuhakikishia Makamu wa
Kwanza wa Rais kuwa tayari wameweka mikakati imara kuona kuwa Skuli hiyo
inarejesha hadhi yake ya Kitaaluma. Matengenezo hayo makubwa
ya skuli hiyo, nyumba za walimu na mabweni ya wanafunzi, pamoja na ujenzi mpya
wa jengo la utawala na vyumba vya kusomea, yamegharimu zaidi ya shilingi Bilioni
tatu na nusu.
Aidha katika hali
siyokuwa ya kawaida, Maalim Seif aliingia madarasani kuona jinsi walimu
wanavyofundisha pamoja na kuangalia ufahamu wa wanafunzi katika skuli za
Madungu na Fidel Castro.
Pongezi Maailm Sheikh Seif Shariff Hamad kwa jitihada zako za Uongozi Visiwani!
ReplyDeleteTupo pamoja kuijenga JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA!!!