Afisa Michezo Jiji la Mwanza Bw. Mohamed Bitegeko (kulia) akipokea fomu ya usajili kutoka kwa Katibu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Mwanza, Bw. Peter Mujaya, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza  Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye jana alijisajili rasmi kushiriki katika mbio za kilometa tano (5) za mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba ,2013 katika uwanja wa CCM Kirumba.
Afisa Michezo Jiji la Mwanza Bw. Mohamed Bitegeko (kulia) akipokea jesi ya kukimbilia ambayo itatumika mwaka huu katika mbio za Rock City Marathon,  kutoka kwa Meneja Biashara wa Airtel katika kanda ya Ziwa Bw. Raphael Dandi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza  Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye jana alijisajili rasmi kushiriki katika mbio za kilometa tano (5) za mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba ,2013 katika uwanja wa CCM Kirumba.
======  ======= =======
Mkuu wa mkoa wa Mwanza kushiriki Rock City Marathon 2013

SIKU chache baada ya kamati ya maandalizi ya mbio za Rock City Marathon 2013 kutangaza usajili rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo ametangaza kushiriki mbio hizo kutokana na umaarufu wake maeneo mengi Kanda ya Ziwa.

Mbio hizo zinatarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba ,2013 katika uwanja wa CCM Kirumba na tayari watu wengi wameanza kuchukua fomu ili kushiriki.
Ndikilo alitangaza ushiriki wake jana katika hafla fupi ya uzinduzi wa Rock City Marathon 2013 kanda ya ziwa yenye lengo la kuhamasisha wananchi wengi kujitokeza mwaka huu.

Ndikilo ambaye aliwakilishwa na, Afisa Michezo Jiji la Mwanza Mohamed Bitegeko, mbali na kuipongeza kampuni ya Capital Plus International ambayo ni mwaandaji wa mbio hizo, alitoa wito kwa viongozi wa chama cha Riadha Mkoani Mwanza, waratibu na wasimamizi wa michezo wilayani na Mkoa wa Mwanza kuongeza nguvu katika kuhamasisha ushiriki wa watu ili mkoa huo uweze kuvumbua na kuinua vipaji vipya katika riadha.

“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), African Barrick Gold, Precision Air, Airtel, Bank M, Parastal Pensions Fund (PPF), Nyanza Bottlers, New Mwanza Hotel, Sahara Communication na Umoja Swithch ambao wamejitokeza kuunga mkono jitihada hizi ambazo zitasaidia kuinua mchezo wa riadha nchini pamoja na kutangaza nchi yetu,” alisema.

Aliagiza viongozi wa michezo na utamaduni wa Mwanza kuitumia fursa inayoletwa na mbio hizo ili kutangaza mkoa wa Mwanza, na Tanzania kwa jumla kimataifa.

“Tumeshuhudia wanariadha mbali mbali vijana wa nchi kama Kenya wakiibuka washindi katika mbio zilizofanyika mjini Berlin, Ujerumani hivi karibuni na kujinyakulia fedha nyingi pamoja na zawadi mbali mbali. Hii iwe chachu kwetu kama mkoa na Taifa kwa ujumla kutilia mkazo mchezo huu kwani licha ya kuwa ni ajira kwa vijana lakini pia zinatumika kama kitambulisho kikubwa cha taifa letu kimataifa endapo wanariadha wetu wataweza kufanya vizuri,” alisema Ndikilo. 

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Riadha mkoa wa Mwanza Silas Nkungu alisema mbiyo za Rock City Marathon imeleta hamasa kubwa katika mkoa wa Mwanza hasa kwa kuitangaza kimichezo na kuongeza kuwa kwa mwaka huu, Mwanza imeshika nafasi ya nne kitaifa katika michezo.

Mratibu wa mbio hizo Bw Mathew Kasonta alisema tofauti na mwaka jana, kwa mwaka huu washiriki wataweza kujisajili kupitia Airtel Money na kuongeza kuwa fomu zitapatikana kwenye maduka yote ya Airtel.

“Kwa wale watakao tumia Airtel Money kujisajili, unapaswa kutuma pesa kwa jina la fumbo (MARATHON) ambapo utapokea ujumbe utakaouonyesha pale utakapokwenda kuchukua fomu za usajili katika ofisi za makao makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mbeya, Arusha na Mwanza,” alisema.

Kasonta aliongeza kuwa washiriki wenye vigezo pia wataweza kusajili kwa kupata fomu zipatikanazo katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza, na katika ofisi za kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya tatu, upande wa kulia katika jengo la ATC, Mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam.

Alibainisha kuwa fomu za usajili zitapatikana katika viwango vya bei vifuatavyo; shilingi 5,000 kwa mbio za km 21 (kwa watu wote), shilingi 3,000 kwa mbio za km 5 (mbio kwa makampuni na taasisi).

Alisema kuwa fomu kwa mbio za kilometa 3 (kwa wazee kuanzia miaka 55 na watu wenye ulemavu wa ngozi) na mbio za kilometa 2 kwa watoto (wenye umri wa miaka 7 mpaka 10) zitapatikana bure.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...