Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokutana na kufanya Mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon mwezi Septemba mwaka huu wakati wa Mkutano wa 68 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Katibu Mkuu ametuma salam za rambirambi kwa Familia na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha Mlinzi wa Amani Mtanzania ambaye amepoteza maisha siku ya jumapili baada ya kushambuliwa na kundi la waasi la M23 katika eneo la Kiwanja- Rushuru kilimita 25 magharibi ya mji wa Goma. katika shambulio hilo, Mlinzi mwingine ambaye pia ni Mtanzania amejeruhiwa. kumekuwapo na mapigano kati ya Majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC) na Kundi la M23.

Na Mwandishi Maalum

Kwa   mara nyingine  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban  Ki Moon, amelaani vikali  tukio la kuuawa kwa mwanajeshi  wa kitanzania  aliyekuwa akihudumu katika Misheni ya  Umoja wa Mataifa ya  Kutuliza Amani katika Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo ( MONUSCO)

Kifo cha mwanajeshi huyo mtanzania   kimetokea jana jumapili baada ya kushambuliwa na kundi la M23 ambalo linapigana na majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya KONGO ( FARDC)

Katika salamu zake  rambirambi kwa  familia ya  marehemu  na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mkuu   huyo wa Umoja wa Mataifa, ameelaani vikali mauaji hayo na kuahidi kwamba  Umoja wa Mataifa utaendelea kutekeleza  majukumu yake ikiwa  ni pamoja na kuchukua  hatua   zote muhimu kuwalinda raia wa DRC

“ Ninalaani vikali mauaji ya  mlinda amani kutoka Tanzania ambaye alishambuliwa  na kundi la M23 katika eneo la    Mashariki ya  DRC, ninatoa  salamu zangu za  rambirambi kwa familia ya marehemu,  na  kwa Serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania ” ananukuliwa Katibu Mkuu akisema.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoufikia Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,   siku  ya jumapili , zinaeleza kwamba Mlinzi huyo wa  amani aliyepoteza maisha  na ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa   anacheo cha  Luteni na kwamba alishambuliwa wakati  kikosi chake kikiwa katika harakati za kutoa ulinzi wa  raia katika eneo la Kiwanja- Rutushura  kilomita 25 kutoka  Magharibi mwa  mji wa Goma.

Katika mashambuli hayo mlinzi mwingine wa amani ambaye pia ni mtanzania amejeruhiwa.

 Aidha  taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  inaeleza kwamba Umoja wa Mataifa utachukua  hatua zote muhimu kwa mujibu wa Azimio namba 2098 ( 2013 ) kutimiza wajibu wake .

Ni kupitia Azimio hilo ambalo lilipitishwa mwezi Marchi  mwaka huu,  Baraza  Kuu la Usalama liliridhia kuanzishwa kwa Brigedi Maalum ( FIB) ambayo pamoja na mambo mengine imepewa  jukumu la kutumia nguvu pale inapobidi ikiwa  ni pamoja na kuwapokonya silaha makundi ya wanagambo wenye silaha likiwamo kundi  hilo la M23 na makundi mengine ambayo yamekuwa yakiendesha mapigano na machafuko katika DRC.

Mapigano yanayoendelea hivi sasa kati ya majeshi  ya serikali ya Kongo na kundi la M23 yamefuatia kuvunjia hivi  karibuni  kwa mazungumzo ya  Kampla  yaliyokuwa yakiendelea  kati ya pande  mbili. Hali inayolifanya eneo hilo la Mashariki ya Kongo kuzidi kuwa tete.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Poleni sana wafiwa na wa-tz!

    Ila wa-tz inabidi tujiulize kwanini wanajeshi wetu wanakufa sana siku hizi kwenye hizi opereshen?..je umahiri wa jeshi letu upo kama zamani?mafunzo yao ni mazuri kama zamani?silaha zao?maslahi? au hizi siasa nazo zimeingia mpaka jeshini na kuharibu mfumo mzima wa mafunzo ya hawa walinda amani wetu?

    Nadhani iundwe tume kuchunguza mafunzo ya wanajeshi wetu maana hata zikiwa zinatolewa taarifa kuwa jeshi letu ni imara sijui bora lakini kwa rate hii ya kuuliwa&kujeruhiwa tena na waasi wasio na special training inaonesha kuwa kuna walakini kwenye jeshi letu na kufunika haya kwa taarifa za kutiana moyo itazidi kutu-cost na hatuwezi kujua litakalofuata!

    Again poleni sana familia yote.

    sam

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...