Na Richard Bagolele
Serikali Wilayani Chato imesema haitavumulia vitendo vya imani potofu hasa zile za kishirikina zinazoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hii.
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Rodrick Mpogolo ameyasema hayo leo wakati akihutubia kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chato kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Mhe. Mpongolo amesema matukio mengi yanayotokea katika Wilaya ya Chato hasa yale ya kishirikina kama mauaji ya vikongwe na mauaji mengine kwa imani potofu yanatokana na jamii kutokuwa na elimu na kuendekeza imani potofu “haya matukio ya mauaji ya vikongwe tunayoyashuhudia katika wilaya hii ni kwa sababu ya jamii kutokuwa na elimu, ni wajibu wetu kuwaelimisha wananchi” amesesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Amelitaka Baraza la Madiwani kushirikiana na wataalamu kutoa elimu kwa Jamii ya wananchi kupeleka watoto shule kwa hiari.
Amesema kutokana na taarifa za Mkoa wa Geita kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyefanya ziara hivi karibuni zinaonyesha kwa Mkoani Geita kuna mdondoko mkubwa wa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na kumaliza darasa la saba, hata mtihani wa kumaliza kidato cha nne katika wilaya ya Chato zaidi ya wananfunzi 1000 hawakufanya mtihani huo na kusema jambo hilo si la kuvumiliwa na kila mtu lazima atimize wajibu wake.
Kutokana na tatizo hilo Mkuu wa Wilaya ameitaka Halmashauri hiyo kutunga sheria ndogo ambazo zitasimamia masuala ya elimu Wilayani hapa.
Kwa mujibu wa Taarifa ya mkoa wa Geita kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliyefanya ziara hivi karibuni watoto walioandikishwa kuanza darasa la kwanza mwaka 2007 ni 52355 na waliofanya mtihani mwaka huu ni 30367 ambao hakumaliza shule wakiwa 21988 hali iliyomshtua sana Mhe. Rais.
Kutokana na Taarifa hiyo Mkuu wa Wilaya amewaomba viongozi wote, wazazi na walimu kushirikiana katika kuhakikisha wanafunzi wote wanaoandikishwa kuanza darasa la kwanza wanamaliza darasa la saba na wale wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanamaliza kidato cha nne.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...