Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa, ujenzi wa barabara hapa nchini umekuwa ni kichocheo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii hasa pale barabara hizo zinapopita katika maeneo ya uzalishaji zikiunganisha na maeneo ya masoko. 
 Akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika katika eneo la Old Maswa nje kidogo ya mji wa Bariadi wakati wa uzunduzi wa ujenzi wa barabara ya Bariadi - Lamadi, Rais Kikwete alielezea kuwa kukamilika kwa barabara hiyo pamoja na sehemu iliyobaki inayoanzia Bariadi kupitia Maswa hadi Mwigumbi mkoani Shinyanga kutapunguza kwa kiasi kikubwa umbali wa usafiri kwa kuunganisha miji ya Shinyanga na Musoma. 
Kwa hivi sasa ili kusafiri kati ya Shinyanga na Musoma msafiri analazimika kuzungukia Mwanza mjini kutokana na hali ya barabara hii ambayo ni ya changarawe kutopitika vizuri hasa nyakati za mvua. Rais Kikwete yuko mkoani Simiyu kukagua shughuli za maendeleo ambapo alianza moja kwa moja kuuzindua mradi wa ujenzi wa barabara ya Bariadi hadi Lamadi yenye urefu wa kilometa 71.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Shilingi bilioni 67.4. 
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Paschal Mabiti alimshukuru Rais Kikwete kwa kuipa kipaumbele barabara hiyo hadi kufanikisha kuanza kwa ujenzi wake. “Barabara hii mbali ya kuwa kiungo muhimu na mikoa ya jirani ya Mara, Mwanza na Shinyanga lakini pia inapita katika maeneo mengi ya uzalishaji na hivyo kuwa kichecheo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa eneo hili” alielezea Mhe. Mabiti. 
 Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumzia maendeleo ya mradi huo alibainisha kuwa, hapo awali Mkandarasi anayetekeleza maradi huo Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd kutoka Jamhuri ya Watu wa China, alianza hovyo hovyo na kwa kasi kidogo lakini ameweza kubanwa na hatimaye hivi sasa anaendelea vizuri akiwa tayari mefikia asilimia 51 ya kazi yote ya ujenzi wa barabara hiyo. 
 Waziri Magufuli alielezea kuwa tayari Mkandarasi huyo anakamilisha ujenzi wa madaraja 85 na tayari kiasi cha kilometa 16 za lami zimekwishajengwa. Kwa upande mwingine Waziri Magufuli alieleza kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, Serikali ililazimika kulipa fidia kiasi cha Shilingi milioni 795 kwa wananchi waliofuatwa na barabara hiyo na ambao walikuwa nje ya hifadhi ya barabara. 
Aidha mkandarasi kwa upande mwingine alilazimika kulipa kiasi cha Shilingi milioni 602.14 kwa ajili ya kupata maeneo ya kuchimba mchangarawe na kokoto pamoja na uhamishaji wa miundombinu ya umeme na simu katika maeneo ambayo barabara hii inapita. Akizungumzia kusuasua kwa utendaji wa baadhi ya Makandarasi wanaotekeleza miradi mikubwa ya barabara hapa nchini, Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Patrick Mfugale alisema kuwa kuchelewa kulipwa kwa madai ya Makandarasi kunasababisha kulipia tozo za ziada na hivyo kuyafanya madeni kuongezeka kadri madai hayo yanavyochelewa kulipwa. 
 Ziara hiyo ya Rais Kikwete katika mkoa wa Simuyu inatarajiwa kuendelea katika wilaya nyingine mkoani humo ambapo anatarajiwa pia kuweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa daraja la Mwanhuzi katika wilaya ya Meatu.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiweka jiwe la Msingi kuzindua rasmi ujenzi wa barabara ya Bariadi hadi Lamadi yenye urefu wa kilometa 71.8
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete aliyeshika mkasi akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa barabara ya Bariadi hadi Lamadi yenye urefu wa kilometa 71.8. Kushoto kwa Rais ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kulia kwa Rais ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Paschal Mabit
 Kutoka kushoto; Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, Mkuuwa Mkoa wa Simiyu Mhe. Paschal Mabiti, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Eng. Patrick Mfugale, wakibadilishana mawazo wakati wa sherehe za uzinduzi wa barabara ya Bariadi - Lamadi inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Moja ya madaraja yanayojengwa katika barabara ya Bariadi - Lamadi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...