Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema ni jambo la kutia moyo kuona
mahusiano na mashirikiano kati ya Oman na Zanzibar yanaendelea kuimarika siku
hadi siku.
Amesema mbali na
mahusiano ya kiserikali, nchi hizo pia zina uhusiano wa kindugu ambao hauwezi
kusahauliwa, hali inayopelekea watu wengi wa Oman kuamua kuja Zanzibar kwa
ajili ya mapumziko wakati wa likizo zao.
Akizungumza na Balozi
mdogo wa Oman Sheikh Saleh Al-Hafidh, aliyefika Ofisini kwake Migombani kwa
ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi, Maalim Seif amesema
mahusiano hayo yatazidi kuimarishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.
Amesifu kazi nzuri
iliyofanywa na balozi huyo katika kipindi kifupi cha miezi mitatu alichofanya
kazi Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuratibu na kufanikisha kufanyika kwa Tamasha
la Kiislamu hapa nchini.
Amemtaka Sheikh Saleh
aendelee kuwa balozi wa kuitangaza Zanzibar nchini Oman na nchi nyengine
atakazokwenda kuzifanyia kazi.
Aidha Makamu wa
Kwanza wa Rais amesifu juhudi zinazochukuliwa na Sultan Qaboos wa Oman katika
kuisadia Zanzibar katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi na kitaaluma.
Amesema mara zote
Sultan Qaboos amekuwa akitekeleza ahadi zake za kuisaidia Zanzibar, na
kuonyesha mashirikiano makubwa katika kuwaendeleza Wazanzibari kupata elimu ya
juu ambapo tayari ametoa nafasi kadhaa za masomo nchini Oman.
Kwa upande wake
Balozi mdogo wa Oman Sheikh Saleh Al-Hafidh, ameishukuru Serikali na wananchi
wa Zanzibar kwa kumpa mashirikiano mazuri yaliyorahisisha kutekeleza majukumu
yake ya kikazi kwa ufanisi.
Amesema ataendelea
kushirkiana na Zanzibar wakati wowote licha ya kumaliza muda wake wa utumishi
hapa nchini, na kwamba amepata moyo huo baada ya kujionea mwenyewe ukarimu na
ustaarabu wa Wazanzibari ambao kwa kiasi kikubwa unashabihiana na ule wa watu
wa Oman.
Hassan Hamad (OMKR)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...