Watu 10 wanaotuhumiwa na mauaji ya Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Marehemu Dkt. Edmund Sengondo Mvungi (pichani) , leo walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na shitaka moja la mauaji ya mwanasheria huyo mkongwe.
Saa 2:30 asubuhi washtakiwa hao wakiwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi walifikishwa katika viunga vya mahakama hiyo kwa ajili ya kusomewa mashitaka yao.
Washtakiwa hao ni, wafanyabiashara Chibago Magozi maarufu kama Chiligati (32), mkazi wa Vingunguti, John Mayunga ama Ngosha (56), mkazi wa Kiwalani na Juma Kangungu (29), mkazi wa Vingunguti.
Wengine ni mlinzi wa Dk. Mvungi, Longishu Losingo (29), mkazi wa Kariakoo Msimbazi, dereva Masunga Msukuma (40), mkazi wa Kitunda,Paulo Mdonondo (30), mkazi wa Tabata Darajani na Mianda Mlewa ama White (40), mkazi wa Vingunguti Shule ya
Tapa.
Wengine ni, Zacharia Msese (33), mkazi wa Buguruni Ghana kwa Hawa Masudi, Msigwa Matonya (30), mkazi wa Vingunguti Machinjioni na Ahmad Kitabu (30), mkazi wa Kinondoni Mwananyamala.
Walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Sundi Fimbo. Wakili wa Serikali Aida Kisumo alidai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya makusudi.
Wakili Kisumo alidai kuwa Novemba 3, mwaka huu, eneo la Msakuzi Kiswegere, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa kwa pamoja na kwa makusudi walimuua Dk. Mvungi.
Hata hivyo, Hakimu Sundi alisema kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza kesi za mauaji, hivyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote hadi pale upepelzi wa kesi yao utakapokamilika, na kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi haujakamilika hivyo waliomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kesi hiyo. Hakimu Sundi alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 5, mwaka huu, aliamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...