BENDI za Twanga Pepeta, Msondo Ngoma na wanamuziki kibao kutoka Sikinde ni sehemu ya wasanii watakaosindikiza tamasha kubwa la Gurumo 53 litakalofanyika mwezi huu.
Tamasha hilo ambalo ni mahsusi kwaajili ya kumuaga mwimbaji mkongwe Muhidi Maalim Gurumo (pichani) litafanyika Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya TCC Club Chang’ombe Jumamosi Desemba  14, 2013.
Kwa mujibu wa kamati ya watu sita inayoratibu tamasha hilo, Gurumo anaagwa baada ya kutangaza rasmi kuachana na muziki wa jukwaani baada ya kudumu kwenye kazi hiyo kwa miaka 53.
Mratibu wa kamati hiyo Juma Mbizo amesema kutakuwa pia na wasanii wa bongo fleva, vichekesho na sarakasi.
Aidha Mbizo amesema tamasha litatanguliwa na bonanza la soka la maveterani.
Hadi kustaafu kwake Gurumo aliyezitumikia pia bendi za Kilimanjaro Chacha,Rufiji Jazz, Kilwa Jazz, Sikinde na OSS – Ndekule, alikuwa ni kiongozi na mmoja wa wamiliki wa Msondo Ngoma ambayo hapo awali ilijulikana kwa majina ya NUTTA, Juwata na OTTU. Gurumo ameitumika Msondo katika majina yote ya nyuma.
Wasanii waliowahi kuitumikia Sikinde ambao watakuwepo kumsindikiza Gurumo ni pamoja na Cosmas Chidumule, Abdallah Gama, Hussein Jumbe, Mashaka Shaaban, Kalamazoo, Henry Mkanyia na Karama Legesu. Wengine ni Ali Yahaya na Boniface Kachala, Benno Villa Anton, Tshimanga Kalala Assossa na Ibrahim Mwinchande.
Baadhi ya wasanii wengine watakaotumbuiza ni Komandoo Hamza Kalala, Kassim Mapili, Hafsa Kazinja na Waziri Ali.

Kamati ya Gurumo iko chini ya uenyekiti wa Asha Baraka, makamu ni Waziri Ali na katibu ni Said Mdoe huku mratibu akiwa Juma Mbizo, wajumbe ni Said Kibiriti na Richardson Sakala. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Leo ni tarehe 21/11/13, Yawezekana hili tamasha limeshafanyika ila tangazo limechelewa kutoka.Vinginevyo kuna makosa ya tarehe iliyotajwa ktk habari hii.

    ReplyDelete
  2. Tangazo linaongelea DECEMBER 14, nadhani mdau ulichanganya na NOVEMBER!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...