![]() |
Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Biashara, Balozi Ombeni Sefue |
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa 'Big Results Now' ni miongoni mwa agenda kuu zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa saba wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), unaotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam,siku ya jumatatu wiki ijayo.
Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Baraza, Balozi Ombeni Sefue, amewaambia waandishi wa habari jana kuwa mada maalum juu ya ushiriki wa sekta binafsi katika mpango huo wa matokeo makubwa sasa utawasilishwa kwenye mkutano.
"Kuna maeneo sita ambayo yaliainishwa katika utekelezaji wa mpango huo na wajumbe wa mkutano watajadiliana namna ya utekelezaji wake na maboresho mbalimbali ilikuleta ufanisi zaidi," alisema.
Mwenyekiti huyo ambaye hakutaka kwenda kwa undani zaidi kuhusu mpango huo alielezea matumaini yake kwamba wajumbe kutoka sekta zote za umma na ile ya binafsi watatoa mchango mkubwa kwenye mkutano huo na swala kubwa mbele yao ikiwa kuleta maendeleo ya taifa na watu wake.
" Hakuna shaka, mkutano utakuwa makini na ni matarajio yangu kuwa wajumbe wote watakuwa na lengo moja badala ya kulaumiana kila upande bila sabubu za msingi," aliongeza Balozi Sefue.
Kwa mujibu wa Balozi Sefue,kikundi Kazi cha baraza kitawasilisha pia mada kuhusu mazingira ya kufanya Kazi na uwezeshaji kiuchumi,ukizingatia kuwa serikali ya awamu ya nne imedhamiria kwa dhati kuona utekelezaji wa mambo hayo unafanikiwa.
" Maswala haya mawili ( economic empowerment and business environment) yanahitaji ufahamu wa kina na kuona ni namna gani kwa pamoja tunaweza kuyashughulikia na kuleta matokeo mazuri," alisema na kuongeza kuwa mkutano utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza.
Balozi Sefue amewataka wajumbe toka pande zote kutoa michango yao ya mawazo kwenye mkutano ili mwisho wake suluhisho ya matatizo iweze kupatikana kwani pande zote zinaaminika na umma wa Tanzania.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF),Bw.Godfrey Simbeye alisema wajumbe kutoka taasisi hiyo wamejiandaa na agenda zao kwenye mkutano huo muhimu.
Bw.Simbeye amesema kuwa sekta binafsi inaitaka serikali iwe makini katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara ilikuiwezesha sekta hiyo kufanya biashara kwa faida na kupanua wigo wa ukusanyaji kodi ambayo ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya nchi.
"Kama mazingira ya kufanya biashara yatakuwa mazuri na kuvutia, basi mafanikio kufikia malengo ya milenia 2025 yanaweza kufanikiwa kwa urahisi," alisema na kuongeza kuwa ni lazima serikali itoe kipaumbele zaidi kwa eneo hilo.
Bw.Simbeye alisema jitihada za pamoja zinahitajika kuhakikisha nchi inasonga mbele na kuwa na uchumi wa kati na kuleta manufaa makubwa kwa watanzania wote.
" Sisi kama TPSF tunapenda suala la uwezeshaji kiuchumi linapata msukumo stahiki na serikali ukilinganisha na jitihada zinazofanywa kwa sasa katika kushughulikia suala hilo," alisisitiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...