Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete ameridhia kuundwa kwa bodi ya Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi itakayosaidia kuongeza mapato ya Jeshi la Polisi ili kuendelea kuboresha huduma ndani ya Jeshi la Polisi na hatimaye kuongeza ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizindua bodi hiyo ya Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi yenye wajumbe nane, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mheshimiwa Pereira Silima alisema, moja kati ya vipaumbele ambavyo bodi inapaswa kuviangalia ni pamoja na kuboresha makazi ya askari ili waweze kutoa huduma bora kwa jamii.
Mheshimiwa Pereira alisema kuwa, kuwepo kwa shirika hilo kwa upande wa jeshi la polisi kutasaidia kuongeza kipato kwa Jeshi ili liweze kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wake, huku akitolea mfano wa shirika la Suma JKT pamoja na J`eshi la Magereza
Nae Mwenyekiti wa bodi hiyo, Bwana Emmanuel Umba alisema yeye pamoja na wajumbe wenzake wa bodi hiyo, wataifanya kazi waliyokabidhiwa na Serikali kwa weledi na kuhakikisha kuwa wanaleta mrejesho wenye mafanikio ili watanzania wawe salama kwani kwa kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wa jeshi la polisi kutaongeza ufanisi katika utendaji kazi zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema alisema usalama, amani na utulivu vina gharama kubwa na kwamba majeshi mengine katika mataifa makubwa na yaliyoendelea, wanatumia mfumo huo wa kuwa na mashirika ya uzalishaji mali katika kujipatia kipato cha ziada ili kuboresha huduma katika majeshi yao ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...