Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa kocha wa makipa wa Simba, James Kisaka (57) kilichotokea leo asubuhi (Desemba 25 mwaka huu) katika Hospitali ya Burhani, Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu kwani Kisaka kabla ya kuwa kocha alikuwa mchezaji katika nafasi ya kipa. Mbali ya Simba, timu nyingine alizowahi kudakia ni Ndovu ya Arusha, Volcano ya Kenya na Small Simba ya Zanzibar.

Akiwa mwanafunzi Shule ya Sekondari Tambaza jijini Dar es Salaam aliwahi kuchezea timu za Oysterbay Stars, Eleven Stars ya Msasani, Sigara wakati ikicheza Ligi ya Temeke na Nyota Nyekundu kabla ya kutua Simba.

Pia alikuwemo kwenye timu ya Taifa ya vijana iliyokwenda Zimbabwe kwenye sherehe za uhuru wan chi hiyo mwaka 1980. Vilevile alikuwa mmoja wa wachezaji waliounda kombaini ya Tanzania ya UMISSETA akiwa na akina Said George, Nico Njohole, George Kulagwa na wengine. Hivyo mchango wake katika mchezo huu tutaukumbuka daima.

Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, Benny Kisaka, James alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa miguu kufa ganzi na matatizo ya kutoona vizuri.

Msiba uko nyumbani kwake Mbezi Mwisho (Kwa Yusuf), na anatarajia kuzikwa nyumbani kwao Kijiji cha Lusanga, Muheza mkoani Tanga.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kisaka, klabu ya Simba na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Marehemu Kisaka ameacha mjane na watoto wanne. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Rest in peace Legendary James Kisaka

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...