Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa Kwa Mikoa Iliyoathirika Zaidi Na Ukame Bw. Harrison Chinyuka akifafanua jinsi Mradi huo utakavyotekelezwa katika Wilaya za mikoa ya Kilimanjaro na Shinyanga, Mradi huo umezinduliwa leo Wilayani Same Mkoani Kilimanjaro, (kulia mwenye suti) ni Mkuu wa Wilaya ya Same Bw. Herman Kapufi. ( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Idara ya Uratibu wa Maafa imezindua Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa Kwa Mikoa Iliyoathirika Zaidi Na Ukame. Mpango huo umeandaliwa na Serikali Kutokana na athari za mabadiliko ya Hali ya Hewa nchini.

Mradi huo uliozinduliwa Wilayani Same mkoani Kilimanjaro tarehe 11/12/2013 kauli mbiu yake ni Athari Za Ukame, Zinapunguzika Jamii Husika Ikijengewa Uwezo. Akiongea wakati wa uzinduzi huo Mratibu wa Mradi Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Harrison Chinyuka alibainisha kuwa Mradi huo utatekelezwa kwa majaribio katika Mikoa miwili nchini ili kuhakikisha kwamba jamii hizo zinawezeshwa kuishi na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Hali ya Hewa.

“ Mkoa wa Kilimanjaro na Shinyanga ndio mikoa itakayotekeleza mradi huu , wilaya zitakazoshiriki katika mradi huu ni pamoja na Same, Hai na Mwanga kwa mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya za Kishapu, Shinyanga Vijijini na Shinyanga Mjini kwa mkoa wa Shinyanga. “ alisema Chinyuka.

Chinyuka alifafanua kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kushirikiana na wadau imeweza kufanya juhudi za ziada za kuhakikisha inaweza kukabiliana na mabadiliko ya Hali ya Hewa

“ Serikali Tayari imeainisha vihatarishi na uwezo wa kukabili maafa katika wilaya za Chamwino, Mpwapwa, Kondoa, Shinyanga Vijijini, Kishapu, Meatu, Bariadi, Maswa, Same na Mwanga. Mkakati wa Mawasiliano wa Taifa Wakati wa Maafa Mpango wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa Taifa na Mipango ya Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa ya Wilaya za Chamwino, Mpwapwa, Kondoa, Shinyanga Vijijini, Kishapu, Meatu, Bariadi, Maswa, Same na Mwanga imeandaliwa.”

Alisisitiza Chinyuka Kupitia mradi huo, Serikali inategemea kujikita katika kuwajengea uelewa viongozi, wadau, wanahabari na jamii, Kuendesha warsha ya wataalamu wa Wilaya na wadau waliopo wilayani jinsi ya kusaidia jamii kupunguza vihatarishi vya maafa, Kuainisha vikundi ya kina mama na vijana kwa lengo la kusambaza elimu hiyo.

Aidha mradi huo utajikita katika Kuelimisha vijana juu ya upandaji wa miti na kilimo cha mazao yanayohimili ukame hususan mihogo na viazi vitamu, Kuainisha na kutoa mafunzo kwa wadau ya matumizi ya mbegu na pembejeo za kilimo, mifugo na misitu, Kuainisha na kutoa mafunzo kwa wataalam ya Matumizi ya vifaa vya kukusanyia takwimu na mawasiliano na Kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa Kwa Mikoa Iliyoathirika Zaidi Na Ukame umefadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Halmashauri husika wakiwa Watendaji Wakuu wa Mradi huo. Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...