Waziri  wa Nchi  Ofisi ya wa Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dkt. Mary Nagu wa pili  kulia akizindua ripoti ya Uwekezaji Tanzania  mwaka 2012, iliyokuwa ikionyesha hali ya uwekezaji wa mitaji binafsi kutoka nje na mtanzamo wa wawekezaji Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC),Bi. Juliet Kairuki, kushoto ni Naibu Gavana wa   Benki Kuu  (BoT), Dkt. Natu Mwamba.
---------------------------------------------------------------------------------

TANZANIA imeendelea kufanya vizuri katika sekta mbalimbali za uwekezaji na kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa na ajira kwa watanzania hapa nchini. 
Ripoti ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa uwekezaji katika sekta nyingi za uchumi zimefanya vizuri sana isipokuwa sekta ya kilimo bado haijafanya vizuri. 
Akizindua ripoti hiyo mwishoni mwa wiki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dkt. Mary Nagu (pichani) alisema serikali bado inaendelea kufanyia kazi maeneo mbalimbali ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji nchini.
“Kazi kubwa iliyopo mbele yetu ni kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta za madini na gesi ili kuisaidia nchi kupata faida zaidi na kutumia fursa hiyo kujenga miundombinu katika sekta ya ya Kilimo ili nayo iweze kuvutia uwekezaji zaidi,” aliongeza Dkt. Nagu. 
Alisema ripoti hiyo imeonyesha uwekezaji wa mitaji binafsi kutokana nje na mtanzamo wa wawekezaji na hii imeweza kuonyesha mazingira ya uwekezaji nchini ni mazuri na yanavutia wawekezaji kuja kuwekeza. 
“Ripoti inaonyesha kuwa Tanzania imeweza kufanikiwa kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, kutoka dola za Kimarekani milioni 6,941.5 mwaka 2008 hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 9,278.1 mwaka 2011,” alisema. 
Dkt. Nagu alisema Katika mazingira hayo serikali ingependa kuona ongezeko hilo la uwekezaji linaenda sambambana na maendeleo ya uchumi wa watanzania wa kawaida. “Lengo letu haswa, tunapenda watanzania walio wengi waweze kushiriki katika uchumi wao, wawezeshwe kwa maendeleo endelevu na kuchangia zaidi pato la taifa,” alisisitiza waziri huyo mwenye dhamana ya uwekezaji. 
Ripoti hiyo imekuja baada ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC),Benki Kuu ya Tanzania (BoT)na Ofisi ya Taifa Takwimu (NBS), kushirikiana kwa pamoja kufanya utafiti ambao umekuja na majibu yaliyolenga kuonyeha hali halisi na changamoto zilizopo ili kupata fursa ya kufanya maboresha mazingira ya uwekezaji hapa nchini. 
“ Viongozi na wadau mbalimbali wanawajibika kutumia tafiti hiyo katika shughuli za maendeleo ili kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri kiuwekezaji na kuchangia maendeleo ya nchi,” alisema. Dkt.Nagu alisema kuwa serikali itatumia ripoti hiyo na kuhakikisha inakuwa ni sehemu ya kufanyia maboresho ya sera ya uwekezaji ambayo itaweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji nchini.
 Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), Bi. Juliet Kairuki alisema utafiti huo ulihusisha Kampuni zilizowekeza Tanzania Bara na Tanzania Visiwani ambapo utatumika katika kupanga mikakati zaidi ya kuongeza uwekezaji. 
“Kazi kubwa ya kituo chetu ni kuhakikisha Tanzania inapata wawekezaji na tafiti hii ndiyo itatumika katika utendaji wa kila siku na kuupatia kipaumbele kufikia malengo yanayokusudiwa na taifa katika kuhamasisha na kuvutia wawekezaji,” alisema. 
Bi. Kairuki alisema kuanzia mwaka 1996 hadi 2013 kituo kimeweza kusajiri miradi ya uwekezaji 8,487 kati ya hiyo miradi 4,230 ni ya watanzania, 2,119 ni ya wawekezaji kutoka nje ya nchi na 2,137 ni ya ubia.
 “ Miradi hiyo inatarajia kuajiri watu 1,223,122 na uwekezaji huo una thamani ya Dola za Kimarekani milioni 70,219.65 na pia kituo chake kimefanya utafiti na kubaini asilimia 80 ya miradi iliyosajiriwa na kituo inaendelea vizuri,” alisisitiza mkurugenzi huyo wa kituo. 
Bi. Kairuki alisema kituo chake kinatafuta fedha kwa ajili ya kuangalia uwezo wa wawekezaji wa ndani sababu hadi sasa hakuna taarifa na picha stahiki juu ya uwekezaji huo. 
Naye Mkurugenzi wa Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS), Dkt. Albina Chuwa alisema utafiti huo umefanyika kwa kufuta vigezo vya Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa na iliweza kuwashirikisha watumiani katika ngazi zote za utekelezaji kukidhi mahitaji ya kutathimini na kufuatilia sera ya uwekezaji nchini. 
“ Utafiti umehusu kampuni zote zenye mitaji kutoka nje, taarifa zao zilizokusanywa ni pamoja na vyanzo vya mitaji, aina ya uwekezaji na mchanganuo wake na pia kampuni hizo zilitoa mwitikio mzuri,”Dkt. Chuwa alisema. Alisema ofisi yake inahamasisha watunga sera, wanasiasa kutumia takwimu hizo kuboresha na kuongeza kasi ya uwekezaji hapa nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Kweli Mwanamke akiwezeshwa anaweza. Cheki hapo. hakuna jibaba wala moja lakini mambo yanaenda mswano. Dah!
    hadi laha manaake...

    ReplyDelete
  2. Je mitaji hiyo imetengeneza ajira ngapi za moja kwa moja na zile ambazo ni indirect? Mana hilo ndo muhimu zaidi, sio mtu anaingia mtaji wa kufufua kiwanda cha kutengeneza mafuta badae anageuza kiwanda kuwa godown, analeta mafuta toka Malaysia

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...