Na Dixon Busagaga wa globu ya jamii Moshi.
WAHAMIAJI haramu 56, Raia wa nchini Ethiopia, wamekamatwa katika
Kijiji cha Jiungeni, Kata ya Ruvu, wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisini Kwake, Kamanda wa Polisi
mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz alisema Wahabeshi hao walikamatwa
majira ya saa sita usiku, usiku wa kuamkia Juzi, wakiwa katika Lori
aina ya Fuso, yenye namba za usajili, T188 AYU, mali ya kampuni ya
E.Lyimo ya Mjini Moshi.
Kamanda Boaz alisema baada ya kupata taarifa ya uwepo wa watu
wanaotiliwa mashaka kijijini hapo, polisi walianza kufuatilia na
kuwahi Gari hilo likiwa na Wahamiaji hao ambao hata hivyo bado
haijafahamika walikuwa wakielekea wapi.
“Polisi waliwahi baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi na
kukamata wahabeshi 56, walikuwa wanasafirishwa kwenye Lori aina ya
Fuso, namba za usajili T188 AYU mali ya E.Lyimo ya mjini Moshi, bado
hatujafahamu walikuwa wanaelekea wapi lakini uchunguzi unaendelea,”
alisema Boaz.
Kamanda Boaz alisema mbali na Wahabeshi hao 56, Polisi walifanikiwa
kuwakamata Watanzania Watatu akiwemo Dereva wa Lori hilo,
aliyetambulika kwa jina la Daniel Mfinanga pamoja na wenzake wawili
ambao majina yao yanahifadhiwa kutokana na sababu za kiupelelezi.
Aidha Kamanda Boaz aliongeza kuwa Utingo wa Lori hilo, aliyemtaja kwa
jina la Ismael Juma, alifanikiwa kutoroka na kwamba jeshi hilo kwa
sasa linaendelea na msako ili kumtia mbaroni.
Kundi la wahamiaji haramu zaidi ya 40 wanaodhaniwa kuwa ni wa kutoka
Ethiopia na Somalia wakishuka kwenye Lori aina ya fuso katika kituo
kikuu cha muda baada ya kukamatwa wilayani Same wakijiandaa
kusafirishwa kwenda nchi ya Afrika kusini.
Wahamiaji haramu wakiwa katika ofisi za kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro muda mfupi baada ya kufikishwa wakitokea wilayani Same ambako walikutwa wakijiandaa kutaka kusafirishwa kwenda Afrika kusini.
Gari aina ya Fuso lililokutwa likiwa limebeba wahamiaji haramu tayari kuwasafirisha kwenda Afrika kusini.
Miaka ya 70 na 80 Wabongo walitumia njia hiyo hiyo kuelekea Ugiriki. Sasa hivi TZ watu wametajirika ndio wakisafiri wanaenda kwa ndege. Wengi walilizwa Bongo na ndugu zao kwa kuuzwa nyumba, viwanja, na vyombo vya dhahabu ili kugharamia nauli ya kwendea Ulaya.
ReplyDelete