CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  kimewasilisha majibu na pingamizi la awali dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuhusu Kamati Kuu ya Chama hicho akiitaka mahakama kuzuia uanachama wake usijadiliwe hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Mbali na majibu hayo na pingamizi la awali, pia chama hicho kimejibu barua ya Zitto  pamoja na kuwasilisha mwenendo wa shauri lililopelekea kuvuliwa nyadhifa za uongozi katika chama hicho kama mlalamikaji alivyoomba.
Majibu hayo yaliwasilishwa katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kupitia mawakili  wa chama hicho, Tundu Lissu na Peter Kibatala ambao wamewasilisha pingamizi  la awali na kutoa hoja sita wakiitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo  kwa kudai haina mashiko ya kisheria.
Katika hoja ya kwanza, Chadema kimedai kwamba shauri hilo halina msingi kwa sababu halikuwasilishwa katika mahakama ya chini kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa kujibu wa kifungu cha 13 cha Mwenendo wa Mashauri ya Madai.
Hoja yake ya  pili, ni kuwa shauri hilo halina msingi na limewasilishwa masijala kuu ya Mahakama Kuu badala ya masijala ya Wilaya kinyume cha sheria na taratibu za masijala za mahakama.
Katika hoja ya tatu, mlalamikaji hajaomba maoni ya Mahakama Kuu kuhusiana na suala linalohusiana na uanchama wake Chadema.
Hati hiyo inaeleza katika hoja  ya nne kwamba shauri hilo halina msingi kwa sababu Zitto anaendesha mashauri mawili kwa wakati mmoja, Mahakama Kuu na rufaa ya kwenye Baraza Kuu la chama.
Katika hoja ya tano, inaleza kwamba shauri hilo Mahakama Kuu siyo mahali pake kwa sababu Zitto hajatumia nafasi zilizopo ndani ya Chadema.

Hoja ya sita, Mahakama Kuu haina mamlaka ya kutoa maamuzi ya maombi ya kuzuia Zitto asijadiliwe uanachama wake kwa sababu ni mambo ya yanayohusu Chadema.

Chadema wakijibu maombi ya msingi ya Zitto kupitia hati iliyosainiwa na Sylvester Masinde na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, wamedai kwamba hawana ubishi kwamba mlalamikaji alivuliwa uongozi Novemba 22, mwaka 2013.
Pia, inaeleza kwamba Zitto alishiriki katika Mkutano wa Kamati Kuu na alijua kinachoendelea kuhusu tuhuma zake.
Upande huo wa walalamikiwa umedai kuwa, maombi ya mlalamikaji hayana msingi na kwamba mbunge huyo alishiriki katika kampeni za kuhujumu uongozi halali wa chama na kuharibu hadhi ya chama kwa kukikashifu na kuanzisha mtandao ndani ya chama kwa lengo la kujiandaa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Chadema inaomba mahakama kutupilia mbali maombi ya mlalamikaji kwa kuwa hayana mashiko ya kisheria.
Mapema Januari 2, mwaka huu Zitto kupitia wakili Albert Msando alifungua kesi mahakamani hapo dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Willbrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Mahakama iliyoke chini ya Jaji John Utamwa ilikubali na kutoa zuio la muda hadi kesi ya msingi itakapoisha.
Katika maombi msingi, Zitto anaiomba mahakama kuiamuru kamati kuu na chombo chochote kisijadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.

Kadhalika, anaoimba mahakama imwamuru, Dk. Slaa kumkabidhi  nakala za taarifa na mwenendo mzima wa vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa katika ngazi ya juu ya chama hicho.
Zitto kupitia wakili wake Msando aliomba mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu na vikao vingine vya chama kutojadili suala la uanachama wake  hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Akiwasilisha hoja zake wakili Msando aliomba zuio hilo litolewe hadi Zitto atakapopata nafasi ya kuwasilisha rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kumvua uongozi katika chama, uliotolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 12 mwaka 2013.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Kumbe Tundu Lissu degree yake ya sheria ni ya Chuo Kikuu cha University of Dar es salaam. Sasa kweli najua kwa nini ni mropokaji na mtu wa kukurupuka. Degree gani ya sheria ni ya miaka mitatu na anakuwa mwanasheria wa kila kitu na huna speciality yoyote katika hiyo sheria. Kauli zake tuu zinakinzana na ukweli wa kisheria unaohitaji mtu asitoe statements zozote kwani zinaweza kutumika mahakamani katika shauri lilioko mahakamani. Mdogo wangu Lissu huku US degree ya sheria ni degree ya pili na lazima uwe speciality katika moja ya hiyo sheria kama vile mwanasheria wa katiba. Ushauri wa bure acha kuropoka na kukurupuka kutoa statements zitakuponza.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...