Na Geofrey Tengeneza
Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mh. Liberata Mulamula ametoa rai kwa vyombo
vinavyohusika kuharakisha mchakato wa kuigeuza Bodi ya Utalii (TTB) Tanzania kuwa
Mamlaka ya Utalii Tanzania ili kukiwezesha chombo hili kuwa na uhuru zaidi na uwezo
mkubwa katika kutangaza vivutio vya utalii na kusimamia sekta ya utalii nchini.
Hayo yalisemwa na Balozi Mulamula hivi karibuni alipomtembelea Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Dk. Aloyce K. Nzuki ofisini kwake ili pamoja
na mambo mengine kuzungumza namna gani Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani
utasaidia juhudi za TTB katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania katika soko
la Marekani.“Ni muhimu ifike mahali TTB iwe na nguvu kisheria na uwezo zaidi katika
kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa au kuwepo kwa migongano, hivyo ni vema
mchakato huo wa mageuzi ukaharakishwa” alisema Balozi Mulamula.
Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo Dr. Aloyce Nzuki alisema tayari Bodi ya Utalii
ilikwishaandaa andiko kuhusu kuigeuza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa Mamlaka
ya Utalii Tanzania (TTA) na andiko hilo kwa sasa liko Wizarani.
Aidha balozi Mulamula ameipongeza TTB kwa kubuni onesho la utalii liitwalo Swahili
International Tourism Expo (S!TE) litakalo kuwa likifanyika kila mwaka mwezi Oktoba
ambalo litatumika pia kuonesha utamaduni wa mwambao na kukuza lugha ya Kiswahili.
Ameahidi kuweka kiunganisho (link) cha tovuti ya onesho hilo la S!TE katika tovuti ya
Ubalozi. Sambamba na hilo amesema pia kuwa kuanzia mwaka huu ofisi yake ambayo
imekuwa ikiandaa na kuratibu safari ya wafanyabiashara mashuhuri wa Marekani
kutembelea Tanzania (VIP Safari) sasa itakuwa ikiandaa safari hiyo na kuwaleta
wafanyabiashara hao mwezi Oktoba wakati wa onesho hilo la S!TE badala ya utaratibu
wa zamani wa kuwaleta wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es
salaam maarufu kama Sabasaba.
Ameahidi kuwa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani utafanya kila liwezekanalo
kusaidia juhudi za TTB katika kuitangaza Tanzania kama eneo zuri la utalii duniani
na akaiomba TTB kuendelea kuwapa taarifa mbalimbali za vivutio vya utalii kadri
iwezekanavyo ili kuwasaidia kutekeleza azma hiyo.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Dr. Aloyce K. Nzuki (kushoto)
akimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mheshimiwa Liberata Mulamula
(kulia) baada ya balozi huyo kumtembelea ofisini kwake na kuwa na mazungumzo
naye.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mheshimiwa Liberata Mulamula akiangalia nakala
ya andiko kuhusu mapendekezo ya kuigeuza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa
Mamlaka ya Utalii Tanzania (TTA) ambalo limekwisha wasilishwa Wizarani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...