Mkurugenzi wa Mfuko wa Sekta Binafsi Afrika (Africa Enterprise Challange Fund) AECF, Bw. Hugh Scott kati akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu shindano la awamu ya tatu ya dirisha la ufadhili wa Kilimo cha biashara, ambapo watazania wenye mawazo ya biashara katika sekta ya Kilimo wanahamasishwakuomba ushiriki.Kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji ya mfuko huo, Dkt. Salum Diwani na kulia ni Mkurugenzi wa Mfuko huo nchini Tanzania, Dkt. Alexandra Mandelbaum.
Watanzania wenye mawazo ya biashara katika sekta ya Kilimo wamehamasishwa kushiriki shindano la awamu ya tatu ya dirisha la ufadhili wa Kilimo cha biashara kwa ajili ya kuendeleza sekta ya Kilimo ambayo inawagusa watu wengi nchini hasa waishio vijijini.
Mkurugenzi wa Africa Enterprise Challenge Fund (AECF), Bw. Hugh Scott aliwambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa mfuko huo umezindua shindano hilo ili kusadia Kilimo cha biashara kama njia ya kusaidia kukuza sekta hiyo ya Kilimo hapa nchini.
AECF ni mfuko wa sekta binafsi wa dola za Kimarekani milioni 217 unasaidiwa na baadhi ya wafadhili wakubwa katika fedha za maendeleo chini ya Muungano wa Mapinduzi ya kijani ya Kilimo kwa nchi mbalimbali za Afrika (AGRA).
Mkurugenzi huyo alisema shindano hilo la awamu ya tatu ya dirisha la ufadhili wa Kilimo cha biashara linalenga kupata mawazo ya biashara katika maeneo mawili yakiwemo ya Kilimo cha biashara katika mnyororo wa thamani na katika ufumbuzi unaoongeza huduma za kifedha vijijini katika kusaidia uzalishaji katika kilimo cha kibiashara na sekta zinazohusiana.
Shindano hilo la dirisha la ufadhili Kilimo cha biashara maalum kwa ajili ya Tanzania lilizinduliwa tarehe 20, January mwaka huu na litakuwa wazi hadi hadi Machi 31, 2014.
Bw. Scott alisema awamu hii pia itashirikisha kufadhili waombaji watakaofanikiwa kupitia mchanganyiko wa ruzuku na mikopo itakayorejeshwa ya kati ya dola za Kimarekani 100,000 na dola milioni 1.
Alisema waombaji wa shindano hilo wanatakiwa kuonyesha mawazo ya biashara yenye matokeo ya uhakika kwa watu masikini vijijini nchini Tanzania, kuongeza ajira na mapato, kupunguza gharama na kuongeza uzalishaji.
Akifafanua zaidi alisema kampuni zinazostahili kuomba ni zile zinazohusika na ukulima au uzindikaji, wale wanaoanzisha mipango ya kilimo cha mkataba, watengenezaji na wasambazaji wa pembejeo za Kilimo, wachukuzi na wafanyabiashara na watoa huduma wengine katika sekta binafsi, ikiwemo huduma za taarifa ya soko.
Alisema alisema fomu za kuomba kushiriki shindano hilo zinapatikana kwenye intaneti kupitia tovuti http//aecfafrica.org/windows/ Tanzania-window.
Kwa upande wake, mjumbe wa kamati ya uwekezaji ya AECF, Dkt. Salum Diwani alisema matarajio ya shindano hilo ni kuona ushiriki mpana wa jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania ili kusadia sekta hiyo kupiga hatua.
Alisema wenye mawazo yenye ubunifu wachangamkie fursa hiyo ambayo italeta manufaa kwa maisha ya watanzania na ukuaji wa uchumi vijijini nchini.
“Hii ni njia muafaka ya kusaidia mabadiliko katika mfumo wa soko nchini,” alisema na kuongeza kusema kuwa wenye mawazo bora na bunifu ndiyo wanaolengwa katika shindano hilo.
Akifafanua zaidi alisema si rahisi kwa wakulima kupata huduma za kifedha duniani kote, hivyo mfuko huo umeamua kufanya hivyo kukiwezesha Kilimo kukuwa.
Alisistiza kuwa uchumi wa Tanzania na Afrika utakua kwa kasi kubwa kama sekta ya Kilimo itazidi kuboreshwa na kuwa hiyo ndiyo dhamira ya mfuko wao.
Awamu ya kwanza ya shindano hilo ilizinduliwa mwezi Novemba 2011 na kampuni 10 zilipata ufadhili wakati awamu ya pili ilizinduliwa mwezi Juni 2012 na kampuni 12 zilipata ufadhili.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...