Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna msaidizi mwandamizi (SACP) DAVID MISIME amewaomba Viongozi wa Tarafa za Bereko, Kolo, Pahi na Kondoa Mjini kushirikiana na Jeshi la Polisi kuielimisha jamii kuanzia ngazi ya familia kwa kuwaeleza kuwa matatizo na migogoro iliyopo ndani ya jamii haitatuliwi kwa kujichukulia sheria mkononi bali ni kwa kufanya majadiliano ndani ya vikao katika ngazi mbalimbali na kufuata sheria. Migogoro haitatuliwi kwa kushambulia na kuwapiga watu wengine au kuwauwa watumishi wa serikali, viongozi waliochaguliwa na wala kufunga barabara.
Aliyasema hayo wilayani Kondoa alipokuwa akitembelea tarafa nne za Wilaya hiyo (Bareko, Kolo, Kondoa Mjini na Pahi) ili kuongea na viongozi wa tarafa hizo na kutoa elimu ya kuimarisha Polisi jamii na kuwakabidhi rasmi wakaguzi wa tarafa na Polisi kata ili waweze kushirikiana nao kutoa elimu kwa jamii, kutii sheria bila shuruti, kujenga familia zisizokuwa na mhalifu na kubaini viini vya uhalifu, vurugu na migogoro katika maeneo yao.
Kamanda MISIME alisema uhalifu, vurugu na migogoro vina sababishwa na kuwepo kwa muunganiko wa mambo mbalimbali yanayotokea ndani ya jamii, ni vigumu kwa jeshi la polisi pekee kuzuia vitendo hivyo bila kushirikisha viongozi wa serikali za mitaa, vijiji, kata, tarafa, dini, watu maarufu, wataalam mbalimbali na wananchi. Endapo kutakuwa na ushirikiano wa dhati na kufanya majadiliano, kutoa elimu kulingana na taaluma ya kila mmoja wananchi wataelewa umuhimu wa kutatua migogoro kwa majadiliano, mashauriano badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Aidha alisema malengo makubwa ya polisi jamii na ulinzi shirikishi ni kuweka mazingira ya ushirikiano wa dhati kati ya polisi na wananchi ili jamii iweze kupata ujasiri wa kukemea, kufichua, kuzuia uhalifu na kutatua migogoro kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo. Pia kujenga utayari wa kuchukia uhalifu na kutoa taarifa za uhalifu kwa kuunda kamati za ulinzi na usalama katika ngazi za mitaa, vitongoji, vijiji, kata na tarafa na hata katika maeneo ya ibada lakini pia kuzitambua rasilimali za kiuchumi, kuzilinda na kuheshimu mipaka.
Pamoja na hayo aliwapongeza wananchi kupitia viongozi wa tarafa hizo kwa kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi ambavyo vimesaidia kupunguza uhalifu na aliwataka waendelee kuimarisha na kuunda vipya.
Nao viongozi mbalimbali wa Tarafa hizo wakiwemo Maafisa Tarafa, Madiwani wa Kata, Mahakimu wa Tarafa, Maafisa Ugani, Watendaji wa Kata na Tarafa, Wenyeviti wa Serikali za mitaa, Viongozi wa Dini, Wazee maarufu wa Kata na Tarafa pamoja na Viongozi wa Vikundi vya Ulinzi shirikishi, wamemshukuru Kamanda MISIME kwa kuweza kufika kwenye tarafa hizo na kuzungumza nao namna ya kuweza kushirikiana na Polisi katika kuimarisha ulinzi ili kupunguza uhalifu katika Tarafa hizo na kusema kuwa elimu walioipata wataifanyia kazi kwa kuelimisha jamii juu ya ulinzi na usalama katika jamii inayowazunguka.
Halikadhalika viongozi hao wamesema Polisi jamii imewezesha wananchi wakawa na mafunzo mazuri ya kuepuka mambo maovu pia wameomba Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma liendelee na utaratibu huu wa kutembelea Kata na Tarafa ili kuweza kutoa elimu itakayo wapatia mbinu mbalimbali za kuweza kukabiliana na uhalifu na wahalifu.
Wameliomba pia Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma liandae utaratibu wa kuwapatia mafunzo ya udereva vijana wao wanoendesha pikipiki (bodaboda) ikiwa pamoja na kuwapatia leseni za udereva ili kuepusha ajali zitokanazo kwa kutojua sheria za usalama barabarani.
Aidha viongozi wa mgambo na ulinzi shirikishi wameomba wapatiwe mafunzo mablimbali ya kukabiliana na uhalifu kama ukamataji salama pamoja na vitendea kazi ikiwemo vitambulisho, pingu, virungu na sare za kazi kwani imekuwa changamoto kubwa katika kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Katika kuhitimisha vikao hivyo na viongozi hao wa tarafa Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma DAVID MISIME – SACP amesema Viongozi wa gazi zote na wananchi wajijengee utamaduni wa kuitisha vikao vya pamoja na kujadili namna ya kutatua migogoro inayowakabili katika maeneo husika.
Pia amewaagiza maafisa tarafa washughulikie daftari la wakazi ili kuweza kuwajua wakazi wa maeneo yao na kuwatambua wageni na wavamizi ambao ndiyo chanzo cha migogoro na uhalifu.
DAVID A. MISIME - SACP
KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...