Maoni ya baadhi ya wadau kuhusu lawama kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwa posho ya Shilingi 300,000/= wanayolipwa kwa siku, haikidhi haja.

Maria Sarungi-Tsehai, Mjumbe wa Bunge la Katiba kupitia kwenye ukurasa wake wa Facebook ameandika:
Kimsingi tuliteuliwa kwenda kuwakilisha wananchi wa vikundi mbalimbali katika Bunge maalum la katiba kufanya kazi moja tu kwa siku 70 - kuandaa pendekezo la katiba kisha tutawanyike turudi makwetu. Hatujaenda huko kutajirika wala kupata ajira. Tunashukuru kwamba pamoja na hayo tumepatiwa hela ya kujikimu ya laki 3 kwa siku ambayo mtu akitumia vyema inatosha kabisa. Kuomba kuongezewa posho si haki kwa 80% ya watanzania wanaoishi kwa shilingi 1,000 kwa siku. Tutambue kuwa ni kweli gharama za maisha mjini ziko juu lakini tusitake kuleta ulafi. Mwenye mamlaka ya kuongeza posho za wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ni rais Jakaya Kikwete, tumtumie ujumbe kwamba asiongeze posho hizo - iliyopo inatosha!

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kupitia kwenye ukurasa wake wa Facebook ameandika:
Naomba niseme wazi kabisa kwamba, sitapokea nyongeza yeyote ya posho hata ikiongezwa. Inaweza isisaidie kuzuia walafi wengine kupata posho kubwa lakini ni bora kuhesabika kwamba nimesema hapana. Ifikie wakati tuseme hapana kwa excesses zisizo na maana. Ninamwomba Rais asikubali kuongeza posho kama baadhi ya wajumbe wa BM wanavyotaka. Wanachopata kinawatosha sana. Nawasihi wananchi mumwombe na ikibidi kumshinikiza Rais kukataa.

Mwenyekiti Msaidizi CUF, Julius Mtatiro kwenye ukurasa wake wa Facebook, Mtatiro kupitia kwenye ukurasa wake wa Facebook ameandika:
NCHI HII ITAMALIZWA;
Tunafahamu kuwa kuna njama zinapangwa ili wajumbe wa bunge la katiba ati waongezewe fedha zaidi.
Hoja hii imetolewa leo hii na mmoja wa wajumbe huku ikionekana kuwa maarufu na inayoungwa mkono na baadhi ya wajumbe, hasa wabunge wa CCM.
Binafsi na wenzangu wengi tumepanga kutumia kila uwezo kuzuia nia hiyo OVU, ifikie wakati tuambiane ukweli vinginevyo nchi hii watu watakufa masikini.
Shilingi laki tatu tunazopewa kwa siku zinatosha kabisa, ambaye hazimtoshi aongeze za kwake, na ambaye anaona hawezi kuongeza zake aondoke Dodoma ili kupisha wanaoweza kutunga katiba kwa posho ya shs 300,000 waendelee.
Laki tatu tunazopata zinatosha kila kitu na CHENJI inabaki, zinatosha kula, kulala, kumpa dereva na kuishi Dodoma.
Lazima sisi tunaotunga katiba tufahamu kuwa maisha ya wananchi ni muhimu na kwamba wana mahitaji yasiyokwisha hata baada ya bunge hili.
Baadhi yetu tulioko humu bungeni tutakataa jambo hili kwa maneno na vitendo. Wakipitisha kwa wingi wao tuta-boycott kuzipokea.
Kenya pale mnakumbuka hoja ya wabunge kujiongezea mapesa ilipingwa vikali na wananchi waliandamana hadi nje ya ukumbi wa bunge. Hapa Tanzania hata zikiongezwa milioni kila siku hutaona mwananchi anachukua hatua kwa vitendo, kuoneshwa kutoridhishwa kwake.
Tuna tatizo kubwa sana, sisi viongozi na wananchi wetu. Kuna mtu anasema, viongozi ni zao la jamii hiyohiyo.
Tuungane pamoja kusimamia jambo hili, ninyi mlioko nje na sisi tulioko ndani.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbrod Slaa akizungumza na gazeti la MWANANCHI amesema posho wanayopewa wajumbe ya Sh 300,000 kwa siku inatosha kabisa:
“kwa kuwa hata wafanyakazi wengine wa serikali wanapokea mshahara wa laki tatu mwisho wa mwezi.”
Joshua Nassari, Mbunge wa Arumeru Mashariki katika tovuti ya JamiiForums ameandika:
MSIMAMO WANGU, SAKATA LA POSHO BUNGENI.
Nimeona nukuu kwenye gazeti la nipashe la leo. Kimsingi ike nukuu si ya kwangu ni nineshazungumza na Mhariri wa jipashe Bw. Kwayu.
Sijui kama nukuu ile imewekwa kwa kukosea au kwa makusudi, wameahidi kurekebisha makosa lakini ni vyema nikaweka msimamo wangu hapa.
Kwa hali halisi ya maisha ya kawaida ya Mtanzania wa shilingi laki 3 ni fedha nyingi. Na taasisi ya Bunge ndiyo inayopaswa kuwapigania hawa watanzania ili vipato vyao vipande lakini taasisi hii siku zote imekubali kuwa upande wa serikali badala ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi.
Fedha hiyo bado ni nyingi mno kama kipato cha mtanzania kinabaki kuwa hapo kilipo.
Kabla ya kupigania ongezeko ambalo linaweza wakati mwingine likawa na mantiki, ni vyema wabunge wakaifanya kwanza kazi yao ya kupigania maisha bora na maslahi bora kwa wananchi hiki hiyo mantiki yao kama ya kufanya mabadiliko ya posho ya shilingi elfu arobaini 40,000/= atakayolipwa mbunge iwapo ataugua akiwa Dodoma iweze kuonekana. Otherwise na sisi wabunge tutakuwa ni sehemu ya dhambi ya mateso na hali ngumu ya maisha ya watanzania ambao bado wanajifungulia sakafuni na hawana maji safi ya kunywa.
Joshua Nassari (MB) na mjumbe wa bunge maalum la katiba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...