Farm Africa kupitia mradi wake Usimamizi Endelevu Mfumo wa Ikolojia wa Msitu wa Nou (SNFEMP) na kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) wamekabidhi pikipiki 10 kwa halmashauri za wilaya za Mbulu na Babati.
Pikipiki hizo 10 aina ya Honda XL zina thamani ya jumla ya Shilingi Milioni Sabini na Tano.
![]() |
Maafisa Misitu wa wilaya za Babati na Mbulu wakiwa na pikipiki walizokabidhiwa. |
Akipokea pikipiki hizo katika hafla fupi iliyofanyika ofisi ya Farm Africa, Dareda Babati, Ijumaa tarehe 14 Februari, mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Babati, Bibi Zainabu Mnubi alisema “tunaishukuru Farm Africa kwa kuwa wadau wetu wakubwa wa maendelo kwa muda wa takribani miaka 20 sasa na tumekuwa tukishirikiana nao katika shughuli mbalimbali na leo hii kutupatia vyombo vya usafiri ni kwa sababu ya mapungufu waliyioona tunayo katika utekelezaji wa shughuli za jamii”.
Maafisa 10 wa serikali katika kata 10 za wilaya za Mbulu na Babati walikabidhiwa rasmi pikipiki moja kila mmoja wao kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wanaoishi kando kando ya msitu wa Nou. Pikipiki hizo zilizokabidhiwa kwa maafisa wa serikali zitalipiwa road licence, bima, matengenezo madogo na mafuta ya kutembelea utekelezaji wa shughuli za mradi kwa muda wote wa mradi (2014-2016).
Naye mwakilishi wa mkurugenzi wa halmashauri ya Mbulu, Bw. Goodluck Kyando alisema maeneo mengi yapo wilayani humo mbali na wakati mwingine wakazi wanakaa muda mrefu bila kufikiwa na wataalam. “Lakini kwa sasa kwa sababu wanavyo vifaa vya usafiri itakuwa rahisi kwa wao kuwafikia kwa urahisi na kuwahudumia hususani wananchi hawa wanaoishi kando kando ya msitu.”
Mara mradi utakapokamilika, pikipiki hizi zitabaki kuwa mali ya Tanzania Forest Service Agency(TFS), na halmashauri za wilaya za Mbulu na Babati. Hizi zikiwa ni Juhudi za kuboresha shughuli za ugani katika kata zilizopo katika mfumo ekolojia wa msitu wa Nou.
Mratibu wa Mradi, Bw Philip Mbaga alitoa wito kwa watendaji waliokabidhiwa pikipiki hizo wazitumie vizuri na wajitahidi kuzitunza ili iwe rahisi kuwafikia wanajamii na kuwasaidia katika masuala ya utaalam.
![]() |
Baadhi ya pikipiki zilizokabidhiwa |
Kwa upande wao,TFS na halmashauri za wilaya zitawajibika kuhakikisha pikipiki zinatumika kwa manufaa ya kuwahudumia wananchi na pia kuhakikisha zinatunzwa na kuangaliwa vyema.
Farm Africa, TFS na Halmashauri za wilaya na maafisa wa serikali katika kata wamesaini mkataba wa makubaliano kuhusu umiliki wa pikipiki na utendaji kazi kwenye kata husika kwa manufaa ya wakazi wa maeneo hayo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...