Mgimwa wa pili kulia, akifurahi pamoja na wana CCM wenzake, siku ya kwanza ya kampeni zake kuwania ubunge jimbo la Kalenga iliyofanyika katika kijiji cha Mseke
 --------------------------------
Na Francis Godwin
MGOMBEA ubunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Kalenga, Godfrey Mgimwa amesema hana chembechembe yoyote ya uzungu na amekishangaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kumtuhumu kwamba sio mtanzania..

"Kama kila mtanzania anayekwenda nje ya nchi kusoma anapoteza uraia wake, basi nchi hii itakuwa na wanasiasa na watanzania wengi wanaokosa sifa ya kuendelea kuwa raia wa Tanzania," alisema.

Akiongea kwenye mkutano wa kwanza wa kampeni za kinyang'anyiro hicho zilizofanyika katika kijiji cha Mseke, jimboni humo juzi, Mgimwa alisema "mimi ni Mhehe, mtoto wa familia ya marehemu Dk William Mgimwa, nimezaliwa Iringa, nimesoma Iringa na baadaye nikabahatika kwenda Uingereza nilikopata shahada yangu ya kwanza na ya pili."

Alisema kwa mara ya mwisho kuitumia passport yake ya Tanzania ilikuwa Desemba mwaka jana alipokuwa anakwenda Afrika Kusini kumuuguza marehemu baba yake Dk Mgimwa.

Kabla mauti hayajamkuta Januari 1, mwaka huu, Dk Mgimwa alikuwa mbunge wa jimbo hilo la Kalenga na Waziri wa Fedha.

Uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo utafanyika Machi 16, mwaka huu katika kinyang'anyiro kinachoshirikisha vyama vitatu vya siasa.

Mbali na CCM chama kingine kilichosimamisha mgombea ni Chadema ambacho mgombea wake ni Grace Tendega na Chausta kilichomsimamisha Richard Minja.

Mgimwa alisema Chadema hawana sera na katika shughuli zao za siasa za kila siku wamekuwa wakipoteza muda mwingi kuzungumza habari binafsi za watu badala ya kuongelea jinsi wanavyoweza kuyakabili matatizo ya watanzania.

"Jimbo la Kalenga limepiga hatua kubwa ya kimaendeleo lakini pia lina changamoto zake; waseme kabla ya kuja Kalenga wao na mgombea wao wamechangia shughuli ipi ya maendeleo katika jimbo letu hili?" alisema.

Alisema akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo kazi yake itakuwa kumalizia utekelezaji wa Ilani ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 na ahadi mbalimbali zilizoahidiwa na marehemu baba yake.

"Kipaumbele changu cha kwanza ni elimu, cha pili kilimo, cha tatu miundombinu na mawasiliano; hizo ni baadhi ya kazi nitakazofanya ili kuwaletea watu wangu maendeleo," alisema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu alisema katika kampeni hizo kwamba wananchi wa jimbo la Kalenga walikwishafanya uamuzi kwa kuichagua CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

"Yapo mengi tumefanya kwa miaka mitatu iliyopita, tunatakiwa kupewa fursa ya kumalizia kazi tuliyoanza. Mpeni Godfrey Mgimwa kura zenu za ndio ili amalizie ahadi za CCM za 2010 na zile za Dk Mgimwa," alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu alisema wanaoituhumu Chadema wakiihusisha na ubaguzi hawakosei na ndio maana kwa ubaguzi ule ule wamemkataa mtanzania mwenzao kwamba sio raia.


"Chadema wanakuja Iringa wakisema kwamba mtoto mliyemzaa nyie wahehe sio mtanzania; hivi angekuwa mweupe si wangesema ni mjerumani?" alisema.


Alisema njia pekee ya kumaliza ubaguzi wa Chadema dhidi ya watanzania wenzao ni kwa kuinyima kura katika uchaguzi huo mdogo  na Uchaguzi Mkuu ujao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...