Swali muhimu tunaloulizwa Watanzania tunaoishi ughaibuni ni: tunataka nini hasa kwenye katiba mpya? Na ni kwa namna gani tunataka changamoto zetu ziingizwe kwenye katiba mpya? 

Katika kipindi hiki cha Bunge Maalumu la Katiba tumeonelea ni muafaka kuyapatia majibu maswali haya. Kwa kuanzia na bila kupoteza muda, Watanzania wa ughaibuni tunataka masuala yafuatayo yaingizwe kwenye katiba mpya: 
· Uraia wa nchi mbili; 
· Haki ya kurudi Tanzania kwa Watanzania na Watu wenye asili ya Kitanzania yaani “Right of Return”; 
· Haki ya kupiga kura yaani “voting rights”; 
· Kupata wawakilishi wa kuwawakilisha Watanzania wa ughaibuni serikalini na bungeni; 
· Haki ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo za Tanzania. 

Katika kujibu swali la pili ambalo ni: ni kwa namna gani tunataka haya tunayoyataka yaingizwe bungeni? Jibu la swali hili ni rahisi sana. 

Tunawaomba Waheshimiwa wa Bunge Maalumu la Katiba pale watakapoanza kuyajadili masuala ya uraia na yale ya Watanzania waishio ughaibuni basi wakubaliane na maombi yetu yaliyotajwa hapo juu na wayapigie kura na kuyaingiza kwenye katiba. 

Mwakilishi wetu kwenye Bunge Maalumu la Katiba Mheshimiwa Kadari Singo naye anaomba msaada wa Waheshimiwa wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba katika kuyapigia kura maoni haya na kuyaingiza kwenye katiba mpya.

Kwenye maombi yetu, karibu asilimia 95 ya Watanzania wanaoishi ughaibuni wanakubaliana nasi viongozi wao wa Jumuiya za Watanzania kwenye diaspora kuwa uraia wa nchi mbili unatoa suluhisho kwenye matatizo yao wanayokumbana nayo siku hadi siku huku ughaibuni. 

Vile vile uraia wa nchi mbili utalipatia taifa faida nyingi tu za kiuchumi, kiutamaduni, kielimu, kisayansi, kiteknolojia na katika masuala mengine mengi ambayo ni muhimu katika kuleta maendeleo ya Tanzania kwa ujumla. 

Suala la uraia wa nchi mbili na haki ya kurudi nyumbani kwa binadamu yeyote anayeishi kwenye nchi nyingine lipo vile vile kwenye “The Universal Declaration of Human Rights” kama haki ya msingi kwa kila binadamu. 

Kwenye haki za binadamu mtu yeyote ana haki ya kurudi katika nchi aliyozaliwa au katika nchi aliyo na ndugu na familia yake. Kwa mantiki hiyo “Right of Return” kama ilivyojadiliwa hapo juu ni muhimu sana kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuwakatalia haki hii, je si kukiuka misingi ya haki za binadamu? 

Watanzania tuna rekodi nzuri ya kuheshimu haki za binadamu na nadhani huu ni wakati muafaka kwa Bunge Maalumu la Katiba kuidhinisha uraia wa nchi mbili ili kutoa haki kwa Watanzania wa ughaibuni kurudi makwao watakapotaka kufanya hivyo. 

Vile vile huu ni wakati muafaka kwa Bunge Maalumu la Katiba na kwa Serikali kukubali kuwa Watanzania waishio ughaibuni wanatakiwa

kupewa haki yao ya kupiga kura. Hakuna sababu yeyote ya kimsingi ya kuwakatalia haki hii. 

Kama kukiwepo na “political will” basi itakuwa ni rahisi kwa Watanzania wa ughaibuni kuruhusiwa kupiga kura. Kupiga kura ni haki ya kila raia na watanzania wa ughaibuni wamekuwa wakinyimwa haki hii kwa muda mrefu. 

Tunaiomba serikali na Bunge Maalumu la Katiba kusikiliza kilio hiki kutoka ughaibuni na wahakikishe kuwa suala hili linaingizwa kwenye katiba mpya, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa wawakilishi wa Watanzania waishio ughaibuni watakaochaguliwa na Watanzania wa Ughaibuni kwa kufuata Katiba ya Tanzania na kwa kufuata sheria zitakazotungwa nchini Tanzania. 

Kwa kumalizia tunawaomba Watanzania wasaini “petition” ya kuomba uraia pacha iliyowekwa kwenye blogu mbalimbali. 

Tunaliomba Bunge Maalumu la Katiba liyaangalie maombi yetu haya na liyafanyie kazi ili yaingizwe kwenye katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Imeandaliwa na Deogratius Mhella, 
Katibu wa Vikao vya Muungano wa Jumuiya za Watanzania Marekani na DICOTA 
Katika kufikisha Maombi ya Watanzania wa Ughaibuni kwenye Vyombo vya habari ili kuelimisha umma wa Watanzania kuhusu maombi ya Watanzania waishio ughaibuni kwenye Bunge Maalumu la Katiba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Nimekuona uncle wangu Katallah. Canada kumekupenda sana.

    Mjomba George!sametlme

    ReplyDelete
  2. mm nauliza je wale walojifanya wasomali wanyaranda wa kongo wakaomba hifadhi ya ukimbizi ughaibuni je wanaweza wakafaidika na uraia wa nchi mbili

    ReplyDelete
  3. Hivi kweli unajifanya msomali au mburundi hili kupata uraia wa nchi za ulaya, leo hii unataka uraia wa Tz kweli?

    Jamani hili swala sioni mantiki yake, hakuna mambo ya uraia wa nchi mbili, chagua moja kati ya Tz au huko mliko.

    ReplyDelete
  4. Nadhani msiombe uraia wa nchi mbili bali uraia wa zaidi ya nchi moja ili kukidhi haja za waliozaliwa Tanzania na kujilipua! Kuweni makini wakati wa kuendesha zaidi ya farasi mmoja. Nadhani kutahitajika ujanja flani amabao nao itabidi tuingize kwenye sharia zetu.

    sesophy

    ReplyDelete
  5. DAAAHH SASA MNATAKA KULETEA WINGI TU HUKU BONGO, MNAWEZA KUINUFAISHA BONGO KIUCHUMI, KISAYANSI NK BILA HATA YA KUWA NA URAIA WA NCHI MBILI, WAWEKEZAJI WAKO WENGI NA WANAZIDI KUMIMINIKA BILA HATA YA KUWA NA URAIA WA BONGO, MNAKARIBISHWA KUFANYA MAMBO KAMA VILE WALIVYO WACHINA, WATURUKI NK....LKN SI KULAZIMISHA SWALA LA URAIA WA NCHI MBILI, KWA SASA BADO HATUPO INTERESTED...

    ReplyDelete
  6. Sasa utakuta mtu kajilipua kwamba kakimbia vita Rwanda, Burundi au Somalia, leo hii unataka na uraia wa Tz, Kaaazi kweli kweli

    ReplyDelete
  7. Eti ''NA MIMI MTANZANIA !''

    Wakati ulipofika Majuu uliukana Utanzania ukaona hauna thamani na leo tena unautaka?

    ReplyDelete
  8. sasa kama mtu kajiripua kama msomali au mrwanda tatizo liko wapi wakati hajaukana UTANZANIA...

    ReplyDelete
  9. Tunaunga mkono Uraia wa nchi mbili. Sio Watanzania wote walioko nje wamejilipua. Labda asilimia moja tu ndio waliojiripua!

    ReplyDelete
  10. Uraia wa nchi mbili utasaidia kukuza uchumi wa Tanzania. Tanzania ni yetu hata Huku ughaibuni ni yetu

    ReplyDelete
  11. Afrika Mashariki sisi TZ ndo bado tuko Nyuma katika suala hili. Kwa nini tusiende sambamba na wenzetu? Shida ipo wapi?

    ReplyDelete
  12. Walioamua kuwepo kwa vyama vingi kwa udogo wao lakini wenya uwezo mkubwa wa kufikiri ndiyo hao hao watakaoamua uraia pacha.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...