MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imesema itasikiliza Machi 3, mwaka huu pingamizi la awali la Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP) la kupinga maombi ya kufanya marejeo kuhusu kuliondoa shitaka la kukaidi amri halali iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam dhidi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda kwa sababu maombi hayo hayana mashiko ya kisheria.
Uamuzi huo umetolewa leo na Jaji Augustino Mwarija baada ya mabishano ya kisheria ya mawakili wa pande zote mbili.
Kabla ya jaji kuahirisha kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Bernad Kongola, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa na upande wa Jamhuri ulikuwa tayari kuendelea.
Hata hivyo, Mawakili wa Utetezi, Juma Nassoro na Obeid Hamidu walidai kuwa walikuwa tayari kuendelea na usikilizwaji lakini waliomba muda kwa ajili ya kujibu pingamizi la awali la Jamhuri.
Nassoro alidai kuwa Februari 24, mwaka huu utetezi ulipokea majibu ya maombi yao lakini yaliambatana na pingamizi la awali.
“Mheshimiwa tunaomba muda wa ziada kwa ajili ya kujibu pingamizi hilo kwa njia ya maandishi au tarehe fupi kwa ajili ya kulisikiliza ili mshitakiwa aweze kupata haki yake” alidai Nassoro.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa maombi ya utetezi kuongezewa muda hayana msingi na kwamba yanapoteza muda wa mahakama.
Katika pingamzi hilo, DPP amedai kuwa maombi ya Sheikh Ponda hayaruhusiwi kusikilizwa chini ya kifungu cha 372 kidogo cha 2 cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kifungu hicho kinaeleza kwamba mtu hataruhusiwa kuwasilisha maombi yoyote ya marejeo ambayo yanatokana na maamuzi au amri ya mahakama ya chini ambayo hayakumaliza kesi.
Jaji Mwarija alisema ili haki iweze kupatikana kwa pande zote mbili, kesi hiyo itasikilizwa pingamizi la awali Machi 3, mwaka huu.
Katika kesi ya msingi, Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka ya kukaidi amri halali, kuharibu imani za dini, kushawishi na kutenda kosa.
Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Awali, Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), aliwasilisha ombi la kuzuia dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo kwa sababu ya maslahi ya nchi na usalama wake mwenyewe.
Baada ya Shekh Ponda kunyimwa dhamana wakili wake, Nassoro aliwasilisha ombi jingine mahakamani hapo la kufuta shitaka la kwanza ambalo ni kukaidi amri halali akidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza vinginevyo lifunguliwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...