Diwani wa Kata ya Mutuka, Wilayani Babati Mkoani Manyara, Mwalimu Yona Wao (wa pili kushoto) akizungumza na wachezaji wa timu za soka za Mutuka FC na Chem Chem FC wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Kombe la Diwani huyo.kushoto ni Mwenyekit wa halmashauri ya Mji wa Babati, Mohamed Omary Farah.(picha woinde shizza,Manyara)
Diwani wa Kata ya Mutuka Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Mwalimu Yona Wao amezindua mashindano ya soka kwenye kata yake itakayoshirikisha timu tano za vijiji vilivyopo Mutuka.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Mwalimu Wao alisema mshindi wa kwanza atajinyakulia kiasi cha sh 80,000 mshindi wa pili atajinyakulia sh 50,000 na mshindi wa tatu atapata sh 30,000.
Mwalimu Wao alisema pia ili kunogesha mashindano hayo kipa bora, mchezaji mwenye nidhamu na mfungaji bora, kila mmoja wao atajinyakulia sh 10,000 na waamuzi wa mashindano hayo watakuwa wanalipwa sh 5,000 kwa kila mchezo.
“Lengo langu la kuzindua mashindano haya kwa timu za Mutuka FC, Chem Chem FC, Sendo Rangers na Endagile FC ni kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira wa miguu kwa vijana wa eneo hili,” alisema Mwalimu Mao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Babati, Mohamed Omary Farah alisema ili kuyapa ladha mashindano hayo atajitolea seti moja ya sare za michezo kwa mshindi wa kwanza wa mashindano hayo.
“Ili kumuunga mkono Diwani wenu nitatoa jezi kwa bingwa wa mashindano haya na ninyi ongezeni jitihada kwenye kucheza vizuri kwani hivi sasa michezo ni ajira mojawapo inayowanufaisha vijana wengi hapa nchini,” alisema Farah.
Kwa mujibu wa msimamizi wa mashindano hayo, Dawi Sumai ambaye ni Ofisa mtendaji wa kata ya Mutuka, michezo hiyo itakuwa inafanyika kwa mtindo wa ligi ikichezwa nyumbani na ugenini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...