Na Bin Zubeiry
Ferroviario wakiwa mbele ya basi la Azam FC liliwapokea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Azam inacheza kwa mara ya pili mwaka huu michuano hiyo ya Shirikisho, baada ya mwaka jana kutolewa hatua ya 16 Bora na AS FAR Rabat ya Morocco, ikiwa chini ya kocha Muingereza, Stewart John Hall, aliyejiuzulu Novemba mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Mcameroon, Joseph Marius Omog.
Azam imekuwa kambini katika hosteli zake za kisasa zilizopo Azam Complex kwa muda wote wiki hii tangu baada ya mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar Jumapili, ambayo walishinda mabao 4-0 Chamazi.
Viingilio katika mchezo huo vinatarajiwa kuwa Sh. 7, 000 kwa jukwaa la VIP A, Sh. 5,000 VIP B na mzunguko Sh. 2,000.
Mwenendo wa timu ya Azam chini ya kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon ‘Simba Wasiofungika’ kwa ujumla ni mzuri, hadi sasa ikiwa imepoteza mchezo mmoja tu kati ya tisa tangu aanze kazi mwezi uliopita.
Azam inayomilikiwa na bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, ni timu pekee inayoendeshwa kisasa nchini ambayo matarajio ni kufuata nyayo za klabu nyingine bora Afrika kama TP Mazembe ya DRC.
Omog alisaini mkataba ma Azam Desemba mwaka jana akitokea klabu ya A.C Leopards ya Kongo Brazavville ambayo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo kwa misimu miwili mfululizo (2012 na 2013) na kumaliza ukame wa mataji wa miaka 30.
Aliiachia timu hiyo ubingwa wa Kongo akiwazidi wapinzani wao, Diables Noirs kwa pointi 10 kutokana na kukusanya pointi 87 katika ligi yenye timu 18.
Mwaka juzi (2012) aliiwezesha A.C Leopards kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria na Sfaxien ya Tunisia.
Mafanikio hayo ya kutwaa ubingwa wa Afrika yalifikiwa baada ya miaka 38.
Kadhalika mwaka jana, A.C Leopards chini ya ukufunzi wa Omog ilitinga hatua ya makundi ya Ligi ya mabnigwa Afrika na kupangwa katika kundi moja na timu mbili zilizocheza fainali; Al Ahly ya Misiri (bingwa) na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Yote hayo ameyafanya akitumia asilimia kubwa ya wachezaji wa ndani ya Kongo huku akiwainua kutoka katika hali ya kuonekana wachezaji wa wastani hadi kuwa tishio na kuhofiwa kote barani Afrika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...