Na Hassan Abbas
Katibu Mtendaji wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) tawi la Tanzania, Rehema Twalib ametoa pongezi kwa Rais Jakaya Kikwete na Serikali ya Tanzania kwa kuanzisha Kitengo cha Utekelezaji wa Miradi Mikubwa ili kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Bi Rehema alisema kuanzishwa kwa Kitengo hicho chini ya Ofisi ya Rais (PDB) ni sehemu ya utekelezaji wa maoni ya wananchi wengi ambapo walipohojiwa katika tathmini ya APRM waliainisha changamoto kubwa ya kukosekana kwa vipaumbele na udhaifu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali.
Katibu Mtendaji huyo aliyaema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa kuadhimisha Siku ya APRM iliyosherehekewa pia kwingineko Barani Afrika.
“Moja ya falsafa ya APRM kote Afrika ni kuzitaka nchi hizi kuheshimu umuhimu wa utafiti na hasa kujifunza kutokana na makosa lakini vile vile nchi zijifunze kutokana na mafanikio ya nchi nyingine ndani na nje ya Bara hili.
“Mfumo wa uwekaji vipaumbele na utekelezaji wa haraka yaani ‘BIG RESULT NOW’ ni dhana iliyotekelezwa na kuonekana matokeo yake kuwa ni mazuri katika nchi nyingine. Tanzania kwa hakika imefanya jambo kubwa kuchukua mfumo huu na tunaamini nchi nyingine wanachama wa APRM wakiona mafanikio ya hapa watachukua mfano huo kutoka Tanzania,” alisema.
Alisema kwa kuwa Serikali inatakiwa kufanyiakazi Mpangokazi wa Kitaifa wa APRM, taasisi hiyo imeridhishwa na kuundwa kwa kitengo hicho ambacho kitasaidia kuondoa malalamiko hayo ya wananchi na kuleta maendeleo.
Katika hatua nyingine, Bi Twalib amesema kuwa Serikali ya Tanzania mpaka sasa imetekeleza vyema majukumu yake katika tathmini ya APRM kwa mujibu wa miongozo ya Bara la Afrika kuhusu utekelezaji wa Mchakato huo.
“Hatua muhimu ambazo nchi yetu imezifikia ikiwa ni miongoni mwa nchi 17 tu kati ya wanachama wa AU waliofanikiwa kufika hatua hizi katika mchakato wa APRM ni hizi zifuatazo.
“Serikali imekamilisha zoezi la tathmini ya awali ya nchi na ripoti iko tayari itazinduliwa hivi karibuni. Kwa sasa tumeanza kusimamia utekelezaji wa Mpangokazi wa Kitaifa (NPoA) wa kuondoa changamoto zilizojitokeza. Mpango huu unasimamiwa na APRM Tanzania na Wizara, Taasisi zilizoguswa na tathmini zitaanza kufanyiakazi maoni ya wananchi katika mwakao ujao wa fedha,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...