Mhe. Chabaka Kilumanga, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro amefanya ziara katika Kisiwa cha Anjouan. Akiwa Anjouan Mhe. Balozi Kilumanga alipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Gavana wa Kisiwa hicho Mhe. Aniss Chamsudine kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Kisiwa cha Anjouan na baadhi ya Mikoa ya Tanzania, hususan katika nyanja za elimu na uwekezaji.
Baadaye, Mhe. Balozi alitembelea maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho na kujionea vivutio vya utalii pamoja na mazingira ya uwekezaji.
Kisiwa cha Anjouan chenye wakazi laki tatu, ni sehemu ya Muungano wa Visiwa vya Comoro.
Kisiwa hiki kimepambwa na mandhari nzuri ya mito ya maji baridi inayotiririka kwenye milima kutoka kwenye bwawa la asili lililopo kileleni mwa kisiwa hicho. Takriban kisiwa chote kimekolezwa na rangi ya kijani kutokana miti aina mbalimbali inayositawi vyema, kama vile minazi na mikarafuu jambo ambalo linachangiwa na hali ya hewa nzuri na ardhi yenye rutuba.
Itakumbukwa kwamba mwaka 2008 Tanzania iliongoza vikosi vya Umoja wa Africa kumaliza uasi wa Kanali Mohamed Bacar aliyejaribu kukitenga Kisiwa cha Anjouan kutoka kwenye Muungano wa Visiwa vya Comoro.
Tangu wakati huo hadi sasa, viongozi na wananchi wa Anjouan pamoja na Wacomoro kwa ujumla wanayo kumbukumbu ya mchango wa Tanzania katika kukikomboa kisiwa hicho.
![]() |
Mhe. Balozi Chabaka Kilumanga na ujumbe wake wakitembelea maporomoko ya maji wakati wa ziara ya kisiwa cha Anjouan, katika Muungano wa Visiwa vya Comoro. |
Mhe. Aniss Chamsidine, Gavana wa Kisiwa cha Anjouan (mwenye suti) akiwa na Mhe. Balozi Chabaka Kilumanga na Mke wake, Mama Irene Kilumanga na afisa wa ubalozi Ali Jabir Mwadini wakati wa ziara ya kisiwa cha Anjouan, katika Muungano wa Visiwa vya Comoro.
Safi sana.
ReplyDelete