Ankal naomba nipe nafasi nitangaze nia yangu ya kuanzisha kampeni ya kupambana na UKUDA hapa Tanzania. Ruksa kunisahihisha bila kuchafua hali ya hewa; ila nielewavyo mimi UKUDA ni hali ya kuwa na roho mbaya, roho ya kwa nini, kukatishana tamaa, na pia kutopenda maendeleo ya wengine - wakati MKUDA mwenyewe akibakia kama alivyo.
Kwa mtazamo huo huo, MKUDA ni mfuasi wa hayo mambo niliyotaja hapo juu. Na ndio kampeni hii itakapoelekezwa, na nitahitaji sana msaada wa mawazo ya wadau wa namna ya kuendesha kampeni hiyo kwa faida ya nchi yetu inayoelekea kupata katiba mpya ambayo naomba UKUDA usipewe nafasi kabisa kabisa!
Ingawa ni kweli sio wote, lakini si uwongo kwamba Watanzania wengi ni WAKUDA. Mifano ni mingi sana kiasi naweza kujaza blog nzima na nisiwe nimetaja japo robo yake tu. Lakini kwa faida yenu naomba nitoe mifano michache.

UKUDA NA WAKUDA KAZINI
Huko kazini utakuta mtu anaandamwa na wakuda kwa sababu anapenda kazi yake, anawahi kazini kila siku, anapiga mzigo kama kwamba ndio siku yake ya kwanza kazini na mabosi wote wanampenda. Hapo utakuta  wafuasi wa UKUDA wanamwandama as if  kaua mtu. Wanamwita mtaka sifa, anajipendekeza, hana lolote na kadhalika. Mradi inakuwa taabu kuwa mchapa kazi hodari kwa kuwa WAKUDA hawataki uwe hivyo.
Mbaya zaidi hao WAKUDA wao ni wategaji wakubwa kazini, wachelewaji na fitina haziwaishi kuwachongea wenzao ambao hawana tabia kama zao. Pia WAKUDA ni wajuaji wa kila kitu, wabishi wa kila jambo na daima utawakuta wanapanga njama za kukatisha tamaa asiye kama wao.

UKUDA NA WAKUDA MICHEZONI
Hapa napo hakuna tofauti na kazini. Mchezaji wa timu Fulani anajituma kwa kuwahi mazoezini, kufanya mazoezi ya ziada (baada ama kabla ya mazoezi rasmi na wengine), ana nidhamu kwa viongozi, wachezaji wenzie na hata mashabiki. Huyu naye haachwi na WAKUDA.
Watampachika majina kibao ikiwa ni pamoja na mtaka sifa, anajipendekeza apangwe kila siku. WAKUDA hao wanataka awe kama wao ili timu ikishindwa iwe lawama kwa wote.

UKUDA NA WAKUDA MITAANI
Huko nako ndio usisema. Mtu anaamua kuwa msafi, anafagia kila sehemu ya nyumba yake. Na kama ni nyumba ya kupanga anahakikisha usafi na unadhifu ni vya lazima kwake. Anaheshimu kila mtu mtaani na wala hajiingizi kwenye migogoro ya ‘Kiswahili’ , na pia kwenye kila shughuli iwe ya msiba ama harusi hakosekani. Kama hawezi kuhudhuria anatoa udhuru na mapema na atahakikisha anawakilishwa na mtu wa familia yake.
Huyu mtu naye unaweza ukamuonea huruma hapo mtaani ama katika nyumba anayoishi, kwa sababu zile zile za KIKUDA.

HITIMISHO
Kama niliyodokeza, mifano ni mingi mno. Ila kwa hiyo mitatu nahisi mada yangu hii inaeleweka sasa. Kifuatacho ni kuomba mawazo ya nini kifanyike ili kampeni ianze. Nimejiandaa kuifanya kampeni hii kupitia vyombo vya habar vyote, mikutano ya hadhara na makongamano. Wafadhili kadhaa nilioongea nao wameonesha nia kubwa ya kusaidia kampeni hii ifanikiwe kwa faida ya wote.

Naomba kuwakilisha
MPINGA UKUDA NA WAKUDA



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Haaa haaa.Nchi haiendelei kwa mtu anayejituma sana kazini na kila idara kwa Tanzania huwa hapendwi.Atapewa majina ya kila aina kama uluvyosema hapo juu...Uvivu unasumbua watu

    ReplyDelete
  2. Uvivu ndiyo chimbuko lake.

    ReplyDelete
  3. Sio uvivu ni tabia iliyojitokeza katika kipindi cha ujamaa na kujitegemea. Kila mtu alishindwa kuchukua jukumu la kuendeleza nchi tukisubiri kufanyiwa ama na serikali ambayo alikuwa ni baba wa taifa tu. Kila mtu aliona si kazi yake kufanya jambo la maendeleo.

    ReplyDelete
  4. Kwa upande wangu wakuda waliwahi kunifanya nipoteze kazi yangu kwa jambo ambalo sijafanya kabisa na kunichongea kwa boss ambae nae aliyachukua maneno kama yalivyo bila ya uchunguzi si unajua tena kazi za muhindi!

    ReplyDelete
  5. Mleta mada nikupo hongera na pole kwa wakati mmoja. Hongera kwa kugonga ikulu, maana watanzania, kama ulivyosema, wengi ni wakuda. tembelea katika hoteli ama duka lolote uone wafanyakazi walivyonuna na kufanya kazi kama hawataki vile ama kama wamelazimishwa. si nia yao kuwa hivyo. Ni wakuda waliowazunguka. wakifanya kazi kwa tabasamu na kujituma watapambana na waumimini wa ukuda. Hahaaaaaaa hii mada tamu kweli na inawafaa sana watanzania. Ona wenzetu wakenya. wao ni kazi tu hakuna ukuda. ndio maana wakiwa mabosi hapa bongo wanachukiwa (na wakuda) kwa kuchapa kazi bila noma.
    Nakupa pole kwa kuwa hata sijui utafanikisha vipi kampeni yako maana ukuda upo kila mahali. Ila usikate tamaa. mradi umeanza kwa hatua hii, zingine zitafuatia. Ushauri wangu ni kwamba endeleza hii kasi ya kuupigia kelele ukuda na wala usichoke.

    ReplyDelete
  6. Wakati mwingine siy ukuda ni kuelezwa ukweli unadhania unaonewa wivu, kuna kitu kinaitwa constructive criticism au feedback ambayo unapaswa uipokee kwa kufaraha na kujirekebisha badala ya kuitumia fursa hiyo vizuri unakataa ushauri.

    ReplyDelete
  7. Wewe anony wa hapo juu unayesema kuelezwa ukweli una harufu ya uumini wa ukuda. constructive criticism inakuaje valid unapomsimanga mwenzio anayejituma na kumwita mtaka sifa? Unajua maana ya maneno hayo kweli ama umeielewa mada? Rudia kuisoma mada yote kisha angalia katikati ya mistari, if u know what i mean. Kinachoongelewa hapa ni nyie wakuda mnaomuona mchakarikaji kuwa ni mtaka sifa, anajipendekeza etc. na si vinginevyo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...