Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Dodoma
Jeshi la Polisi nchini limebuni mikakati itakayosaidia kukomesha ajali za barabarani kwa kuvishirikisha vikosikazi vya Polisi Jamii vilivyotawanywa katika kila kata na tarafa nchini kote.
Mikakati hiyo imetangazwa na Kamishna wa Polisi Jamii CP Mussa Ali Mussa, wakati wa mafunzo ya maadili awamu ya pili yanayotolewa kwa Askari Polisi wa ngazi ya kati yanayoendelea Mjini Dodoma.
Kamishna Mussa amesema kuwa mpango huo utasaidia kuwanasa madereva wazembe wasiozingatia taratibu na sheria za usalama barabarani na hivyo kupunguza ajali ziletazo vifo na majeruhi kwa abiria na watumiaji wengine wa barabara wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Amesema vikosikazi hivyo vinaundwa na askari Polisi kutoka katika vitengo tofauti na kikubwa vikizingatia kazi ya msingi ya Jeshi la Polisi ya kuzuia na kukamata makosa mblimbali yakiwemo ya usalama barabarani.
“Kulinda usalama wa wananchi na mali zao ndiyo kazi kubwa ya Jeshi la Polisi na kwamba kwa yeyote atakayepatikana akienda kinyume na taratibu za usalama barabarani atatiwa mbaroni na hakutakua na huruma kwa mkosaji”. Alisema Kamishna Mussa na kuvitaka pia vikosikazi hivyo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya Afisa wa Polisi.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi kutoka Kamisheni ya Intelijensia nchini, ACP Andrew Mwang’onda, alisema kamisheni hiyo imepanga kuwatumia Mainspekta wakiwemo Wakuu wa Polisi wa Tarafa na Majimbo hapa nchini katika ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia kwa lengo la kubaini viashilia vya kihalifu na wahalifu.
Naye Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Andrew Makungu, ambaye amekokotoa idadi ya Watanzania, vitongoji, vijiji, kata, shehia, tarafa, majimbo, wilaya na mikoa iliyopo hapa nchini ikiwemo ya kipolisi, amewataka Mainspekta hao kuhakikisha kuwa wanashirikiana kwa karibu na wananchi katika kuwabaini wahalifu na maficho yao ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.
Awali Mkuu wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi nchini Naibu Kamishna Mpinga Gyumi, alisema Jeshi hilo limejipanga kuboresha mifumo ya utoaji huduma bora kwa wananchi na kujenga maadili mema ili kuepukana na vitendo vya kudai na kupokea rushwa.
Zaidi ya Mainspekta wa Polisi 300 kutoka katika mikoa mbalimbali hapa nchini wanashiriki katika mafunzo hayo ya wiki mbili mjini Dodoma ambayo yanafanyika kwa awamu tatu tofauti kwa lengo la kukuza maadili kwa askari Polisi wa ngazi ya kati.
Mratibu wa mafunzo SACP Patrick Byatao, akitoa mada kwa Mainspekta washiriki katika mafunzo ya kujenga maadili mjini Dodoma.
CP Mussa Ali Mussa, akitoa mada ya utekelezaji wa miradi ya utekelezaji wa miradi ya Polisi Jamii wakati wa mafunzo ya Maadili kwa Mainspekta wa Polisi ambao ni Wakuu wa Majimbo n Tarafa.
Mainspekta wanaoshiriki katika mafunzo ya maadili na rushwa wakiimba wimbo wa maadili kabla ya kuanza kwa mafunzo hao mjini Dodoma.
Mainspekta wa Polisi ambao ni Wakuu wa Mmajimbo na Tarafa wanaoshiriki katika mafunzo ya maadili mjini Dodoma wakimsikiliza Kamishna Mussa Ali Mussa, akitoa mada ya Utekelezaji wa Miradi ya Polisi jamii.
picha ya pamoja na CP Mussa Ali Mussa, katikati waliokaa pamoja na baadhi ya Mainspekta wa Polisi ambao ni washiriki wa mafunzo ya maadili mjini Dodoma.
Hii itsasaidia sana kwa sababu ukiangalia ajali zinazotokea katika nchi zetu kwa kweli vyombo husika vinahitaji kufikiria mbinu mpya kila wakati kuzikabili.
ReplyDeleteHii itaongeza wigo wa rushwa kama ilivyokuwa kwa wale jamaa wa Majembe walivyokuwa wanafunga magari ya watu minyororo
ReplyDeletePolisi DUME!!!
ReplyDelete