Na Jovina Bujulu, Maelezo Dodoma.
Muungano wa Tanzania kwa miaka 50  umekuwa ni  undugu hivyo kuufuta ni sawa na kufuta  utaifa wetu na kukaribisha ukabila.

Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma, na Kapteni John Chiligati ambaye ni mjumbe aw Bunge Maalum la Katiba wakati wa mahojiano na kipindi cha Jambo kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha TBC One.

Aliendelea kusema kwamba muundo wa kimaisha  wa Muungano wetu ni wa serikali  mbili, hivyo tusivunje kabisa Muungano huo.

"Kuvunja Muungano ni kukaribisha ukabila na kuchanganya wananchi maana watajitenga kwamba wengine ni Wazanzibar, wengine ni Watanganyika, hivyo ni kurudi nyuma badala ya kusonga mbele" aliongeza Mhesh Chiligati.

Akizungumzia madhara ya serikali tatu Mhesh Chiligati alisema kwamba Serikali tatu italeta utata maana kutakuwa na Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. Kwa muundo huo Serikali tatu, serikali ya Muungano haitakuwa na watu, madaraka,utaifa na hata pesa zake.

Akichangia ya kuwa na serikali mbili, Mzee maarufu Mjini Dodoma Jumanne Gombashi alisema kwamba suala la zaidi ya Serikali mbili si tatizo la Watanzania, hivyo tusiwasingizie kwamba wanahitaji serikali tatu , kwani badala ya kutatua matatizo tutaongeza matatizona tutakuwa tunaicha chana nchi yetu.

" Tumekuwa na Serikali mbili kwa miaka 50, kama kuna makosa hatuna budi kujitathmini, na kujisahihisha na kujikosoa ili tutatue matatizo hayo na tuendelee na Serikali mbili.." alisema mzee Gombashi.

Aidha aliendelea kusema kwamba tunapozungumzia serikali tatu tuangalie pia upande wa gharama za uendeshaji wa Serikali hizi. Kila upande yaani Zanzibar na Tanzania Bara utatakiwa kuchangangia uendeshaji wa serikali ya Muungano, na pia tutalazimika kuwa na viongozi watatu, mabaraza ya mawaziri matatu na mabunge matatu.

"Kwa  kuwa na serikali tatu hawa watu wote wanahitaji huduma  kwa hiyo kwa kufanya hivyo tutapanua matumizi kwa nchi changa kiuchumi kama hii yetu" alisema mzee Gombashi.

Mhesh. Chiligati alitoa ushauri wa kudumisha Muungano,na kuepuka muundo utakaodhoofisha  Muungano bali tuhakikishe  Muungano unaimarishwa na pande sote mbili.

Naye mzee Gombashi  alimalizia kwa kuwahimiza Watanzania kutotetereka na kuburuzwa na watu wasiopenda Muungano, na kwamba iko siku tutafika kwenye serikali moja na tuwe wamoja zaidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. sidhani kama mtazamo wako ni sahihi bw chiligati
    muungano sio lazima kwa serikali , tumeungana kwa mambo mengi tu , kenya , burundi , rwanda uganda msumbiji nk kwani sio ndugu zetu? jee tumeungana nao kiserikali? tena bado tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuzipatia uhuru nchi kusini mwa afrika , jee walikuja kutaka muungano wowote na sisi? tusijidanganye unyonyaji wa znz unatakiwa uishe sasa mshatunyonya na kutudhulumu vya kutosha tuachieni nchi yetu tushirikiane kama vile tunavyoshikirikiana na nchi nyengine duniani, kufa kwa muungano ni mwanzo wa maendeleo ya znz , kama hamniamini kwa nini tusivunje muungano halafu tutathmini baada miaka kumi tumekwenda mbele au nyuma , kama tukiona tumekosea tutaruki kutaka muungano tena , hio ndio demokrasia ya kweli , waznz asilimia 90% hawataki muungano wenye kutaka ni viongozi vibaraka mliowapachika vyeo kama manyapara wenu

    ReplyDelete
  2. Kwanza napenda mhe. hapo asitupotoshe kwa sababu mpaka sasa hivi huo utaifa anaouzungumzia upo, kila mtu anajua kuna Wazanzibar na Wanaoijiita Watanzania wakati Tanzania ni pande zote mbili. Tena wenzetu wakiwa nje ya nchi wala hawajitambulishi kama ni Watanzania wanasema ni Wazanzibar, tusidanganyane. Kwa hiyo huo utaifa upo siku zote. Kama ni wamoja mbona kuna Zanzibar na Tanzania na wale mhe. hapo hajawahi kulisemea hili, kwani Tanzania ndio iliungana na Zanzibar. Watanganyika tumelogwa.

    Eti Serikali ya tatu haitakuwa na watu, jamani, hivi kwenye Afrika mashariki lile shirikisho halina watu? Mbona tunadanganya watu. Serikali ya tatu itakuwa na watu tena wachache tu, kwa sababu hata kwa afrika mashariki ni wabunge tisa tu, so hata gharama ya kuiendesha itakuwa ndogo kuliko ilivyo sasa ambapo wabunge wa Zanzibar wana wabunge wawili wawili kila jimbo wa Zanzibar na jamhuri na kuleta wabunge wengi ambao hawana cha kufanya huku na wanakuja siku zote wala sio siku za mjadala wa mambo ya muungano, leo hata mambo yetu ya serikali za mitaa eti anaongoza mzanzibar, jamani! Kwa hiyo, hakuna gharama sana sana itapungua, watakuja kujadili mambo ya muungano tu na hawatakaa kila wakati, sio kama sasa. serikali tatu inapunguza gharama sana na itachangiwa na kila nchi huru ya Zanzibar naTanganyika.Kwa kufanya hivyo ndio uchumi utakavyozidi kukua kwa kila nchi.

    Suala la kudumisha muungano napenda hao waheshimiwa watueleze, mbona hawakuwazuia Zanzibar walipovunja muungano mwaka 2010 kwa kuandika katiba iliyovunja muungano? Kisheria mpaka tunavyoongea muungano ulishavunjika siku nyingi lakini viongozi na hasa watanganyika wanajidai hawaoini, ni muungano gani mnaotaka kuudumisha wakati haupo? Kama Zanzibar ina Rais wake ambaye anaweza kugawa mipaka yake, ni amiri jeshi mkuu, tunaona hata rais wa jamhuri akienda kwenye sherehe kule anayekagua gwaride ni rais wao na amiri jeshi mkuu amekaa tu, hivi hatuoni au tumelogwa. wana wimbo wao, wana bendera yao, wana mahakama zao mpaka rufaa tofauti na katiba sasa mnasema nini? Hivi kuna ubaya gani na upande mwingine kuwa na mamlaka kama hayo?

    Tunaomba hao wahe.watambue kwamba wananchi tumetoa maoni yetu ambayo ndio yako kwenye rasimu ya warioba, tunachoomba wasituwekee maoni yao, na kama walitaka hivyo hakukuwa na haja ya kuunda tume ya kupita kwa wananchi halafu mje muandike yetu, mngekaa bunge moja kwa moja na kutuandikia katiba, so tume ilikuwa danganya toto wananchi waone wameshirikishwa kumbe yanakuja kufutwa, tunahitaji maboresho sio vinginevyo

    Watanganyika tuamke.

    ReplyDelete
  3. kwani kukiwa na muungano wa serekali 3 ndio muungano utakuwa haupo mm mawazo yangu kama tume ya warioba ilojaa wazee wenye heshma zao majaji wana sheria ituletee mfumo wakuvunja muungano inaingia akilini mbona mfumo washirikisho unafanya kazi umoja wa falme za kiarabu kwa miaka mingi

    ReplyDelete
  4. Kitu chochote kizuri kina gharama, hivyo kuongezeka kwa gharama sio hoja yenye mashiko, ili mradi itaondoa manunguniko yote yaliyokuwepo uko nyuma, haswa haswa kumficha Tanganyika. Uvumilivu wa WaTanganyika usije ukachukuliwa kama wanaridhika na muundo ulivyo sasa. Busara zaidi zitumike bila kuogopa mabadiliko! na tuwe wawazi ndani ya nafsi zetu bila kuogopa kuwa fulani atanionaje nikiwa na mawazo tofauti, na huo ndio ukomavu wa jamii iliyostaarabika. Naomba tuendelee kutoa hoja nyingine nzito ili maamuzi yafanyike vema!!

    ReplyDelete
  5. Sikubalinia na kuvunjika Muungano, kuvunjika Muungano ni sawa na kuvunjika Ndoa yangu ya miaka 15 sasa na wanamke wa Kizanzibari!

    Nitasimamia wapi mimi Bakilana Mushumbusi wa Bara mwenye mke kwao Zanzibari nitakapo takiwa kuomba visa nikamwone mke wangu na wanangu?

    Je ikitokea nikanyimwa visa nani atanisaidia kwenda kupata haki yangu ya Ndoa Zanzibar?

    ReplyDelete
  6. Wadau mmesema kweli, kama ni undugu nani asiyejua kwamba Tanganyika ni ndugu kila kona, nani hajui Wahaya wako Bukoba na Uganda? Nani asiyejua watu wengi wa moshi na arusha wana undugu wa damu na watu wa Kenya? Nani asiyejua Waha wana undugu na watu wa Burundi na makabila mengine mengi ni hivyo hivyo. Mbona hatukuungana na Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na kadhalika tukaungana na Zanzibar? Muungano wananchi hatuuelewi ni siri tu na ndio maana malalamiko mengi. Tena ingekuwa ni jambo la msingi sana kama kabla ya kuandika katiba mpya tuulizwe kwanza kama tunauhitaji muungano tupige kura halafu ndio tuendelee lakini wenye kukataa au kuogopa mabadiliko au kung'ang'ania sera ya chama kama chiligati hata kama ukweli unaonekana wakaweka kifungu cha kuzuia kujadili kuuvunja muungano kwenye sheria ya mabadiliko ya katiba kwa kutumia wingi wao, lakini ilikuwa ni jambo la msingi. Lakini sasa hatuuvunji bali tunabadilisha mfumo tu uwe wa shirikisho ili na Tanganyika wawe huru kama walivyo wenzao washirika wa muungano.

    Halafu kuna mtu anasema mimi wala siijui Tanganyika eti kwa sababu kazaliwa baada ya muungano, tena msomi Mtanganyika. Hivi kweli mtu kujua kitu ni mpaka uwepo wakati huo. Kama ni hivyo kusingekuwa na somo la historia. Leo tunajua mambo ya miaka 1800, je, tulikuwepo? Yaani msomi anataka kutuambia hata kwenye historia hakusoma kwamba kulikuwa na nchi ikiitwa Tanganyika? Kwa hiyo, kwa historia yake Tanzania ndio iliyoungana na Zanzibar au Tanzania ndio iliyopata uhuru mwaka 1961? Hata kwenye google hawezi kuuliza historia ya Tanganyika akasoma kuliko kueleza bungeni kwamba haifahamu. Huo wote ni woga wa mabadiliko tu lakini tuangalie hoja za umuhimu wa serikali tatu. Cha ajabu watu wanasema itaendeshwaje, mbona Warioba kasema kabisa chanzo cha mapato yake? Tusome rasimu ili kwenye kura ya maoni tusibabaike.

    ReplyDelete
  7. HAKUNA ANAYETAKA KUVUNJA MUUNGANO,

    wanodai serikali tatu na pia wanodai muungano wa mkataba. HAKUNA ANAYETAKA KUVUNJA MUUNGANO

    Bwana chiligati aonyeshe wapi na nani kasema anataka kuvunja MUUNGANO?

    Taabu ya wanasiasa wetu wengine wanajaribu kutoa sababu zisizo za msingi ili kuwatia khofu wananchi na maoni yao yaonekane yana uzito.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...