Mahakama ya Rufani imewaachia huru wafungwa wawili raia China (pichani)  waliokuwa wakitumikia kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la uvuvi haramu katika katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania (Exclusive Economic Zone- EEZ)
Wafungwa hao , Hsu Chin Tai ambaye alikuwa nahodha wa meli ya Tawaliq 1 waliyokamatwa nayo wakifanya uvuvi huo haramu na aliyekuwa wakala wa meli hiyo, pamoja na baharia Zhao Hanquing. 
 Walitiwa hatiani na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Februari 23, 2012, na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela, au kulipa faini ya Sh20 bilioni, kila mmoja, faini ambayo walishindwa kuilipa na hivyo kutumikia kifungo, huku meli yao ikitaifishwa. 
Hata hivyo Mahakama ya Rufani leo imewaachia huru baada ya kushinda rufaa yao waliyoikata mahakamani hapo, kupitia kwa mawakili wao Kapteni Ibrahimu Bendera na John Mapinduzi.  Mahakama ya Rufani, katika hukumu yake, ilisema kuwa kulikuwa na dosari za kisheria katika taratibu za kuwafungulia mashtaka Mahakama Kuu na kwamba walifunguliwa mashtaka hayo bila kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). 
 Kutokana na kasoro hizo za kisheria mahakama hiyo iliamua waachiwe huru mara moja isipokuwa kama wataendelea kushikiliwa kwa kosa lingine. 
Hukumu hiyo iliandaliwa na Jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa yao - Salum Massati, Semistocles Kaijage na Bethuel Mmila. 
 Hata hivyo licha ya mahakama hiyo kuwaachia huru jana, lakini Wachina hao walirudishwa tena gerezani kwa ajili ya kukamilisha taratibu za Magereza, ambako wamekuwa wakiishi kwa muda wote huo tangu walipotiwa hatiani. 
 Katika rufaa yao, Wachina hao kupitia kwa mawakili wao hao walikuwa wakipinga hukumu na adhabu hiyo ya Mahakama Kuu, iliyotolewa na Jaji Agustine Mwarija.
Katika kesi ya msingi walikuwa wakikabiliwa na mashtaka mawili. La kwanza lilikuwa kufanya shughuli za uvuvi katika ukanda huo wa Tanzania bila kuwa na kibali na la pili  ni kuchafua mazingira ya bahari kwa kumwaga baharini mafuta machafu na uchafu wa samaki. 
Katika kosa la kwanza washtakiwa wote walihukumiwa adhabu ya kulipa faini ya Sh1bilioni kila mmoja au kifungo cha miaka 20 kila mmoja, na katika kosa la pili mshtakiwa wa kwanza aliadhibiwa adhabu ya kulipa faini ya Sh20bilioni au kifungo cha miaka 10 jela. 
Washtakiwa hao na wenzao 35, walikamatwa Machi 8, 2009 wakiwa samaki tani 293 aina ya Jodari na samaki wengineo, waliodaiwa kuwavua katika eneo la Bahari Kuu la Tanzania. 
 Washtakiwa 35 kati yao walikuwa ni raia wa mataifa tofautitofauti ya Bara la Asia, ikiwemo China Ufilipino Vietnam na wawili walikuwa raia wa Kenya. 
Mshtakiwa mmoja raia wa Kenya alifariki dunia akiwa mahabusu kabla ya kesi yao kuisha. Hata hivyo washtakiwa wengine 31 waliachiwa huru baada ya kuonekana kuwa hawana kesi ya kujibu, na kubakia washtakiwa watano, ambapo wawili kati yao ndio waliopatikana na hatia na watatu wakaachiwa huru, baada ya mahakama kuridhika kuwa hawana hatia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Huenda tumeingia kwenye mkataba wa kubadilishana wafungwa na China, pengine na ndugu zetu takribani 300 walioko kwenye magereza ya China watatolewa kirahizi...maana haingii akilini kuambiwa serikali imeloose hii kesi kwakushindwa kufuata taratibu za mashtaka..kweli?

    ReplyDelete
  2. Mimi nakata Rufaa !

    Haiwezekani jamaa Wachina washikwe ndani ya mchuma kwa uvuvi haramu halafu leo tena wapo huru?

    ReplyDelete
  3. Ama kweli Bongo tambarale!

    Yaani jamaa wanaondoka zao kwao kiulainiiii.

    Tunafunga Mateja, Wezi na Vibaka wa simu za Mikononi tu.

    ReplyDelete
  4. Inasikitisha sana kuona kila wakati serikali kila siku ina loose cases kilasiku na kuwapotezea watu muda na pia fedha za serikali zinazotumika kwa kesi hizo! Jee hawa wanaoiwakilisha serikali hawana ujuzi wa kutosha?? Wanafanya nini katika hizo taasisi kama hawajui kazi?? Au kuna mkataba mwingine unakuja?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...