Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani Prof. Kwaku Aning (mwenye tai ya bluu) akiwa ofisini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Patrick Makungu (wa kwanza kushoto) wakijadiliana kuhusu kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na Shirika hilo kwa ajili ya matumizi salama ya mionzi na ujenzi wa Kituo Mahiri cha Tiba ya Ugonjwa wa Saratani nchini.
Prof. Kwaku Aning, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (International Atomiki Energy Agency-IAEA) akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Patrick Makungu (hayupo pichani) ofisini kwake, Dar es Salaam kuhusu ujenzi wa Kituo Mahiri cha Tiba ya Saratani nchini Tanzania ambacho kinaweza kuhudumia Kanda ya Afrika Masharii na nchi za jirani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Patrick Makungu (mwenye tai nyekundu) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Prof. Kwaku Aning, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani na ujenzi wa Kituo Mahiri cha Tiba ya Saratani nchini Tanzania ambacho kinaweza kuhudumia Kanda ya Afrika Mashariki na nchi za jirani.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani Prof. Kwaku Aning yupo ziarani nchini Tanzania kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Machi, 2015 kwa lengo la kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na Shirika lake kuhusu matumizi salama ya mionzi kwa ajili ya tiba ya ugonjwa wa saratani.
Pia aliongeza kuwa Tanzania ni mahali panapofaa kujenga Kituo Mahiri cha Tiba ya Ugonjwa wa Saratani ambacho kitaweza kuhudumia wagonjwa wa kutoka Kanda ya Afrika Mashariki na nchi jirani.
Katika maelezo yake alisema kuwa ugonjwa wa saratani umekuwa ni tishio kwa wananchi wanaoishi kwenye nchi zinazoendelea kama vile Tanzania na ni ugonjwa ambao unasababisha vifo kwa watu wengi kwa mwaka ukilinganisha na magonjwa mwengine ya UKIMWI na Malaria.
Alizidi kuongeza kuwa hivi karibuni Shirika la Afya Duniani, (WHO) lilitoa taarifa kuwa inakadiriwa kiasi cha wananchi wapatao 4.6 milioni wanakufa kutokana na ugonjwa wa saratani kwa mwaka kwenye nchi zinazoendelea kama vile Tanzania ikilinganishwa na wagonjwa wapatao 2.1 milioni wanaokufa kwa ksababu ya UKIMWI na takribani milioni moja kwa sababu ya malaria.
Nchi nyingi zimetoa kipaumbele kwenye magonjwa ya UKIMWI na Malaria ambapo ni tofauti ikilinganishwa na ugonjwa wa saratani ambao unasababisha maumivu makali na hatimaye vifo kwa wananchi walio wengi. Hii inajidhihirisha pia kwa namna ambavyo nchi husika zinatoa msukumo na kipaumbele kwa magonjwa mengine ikiwa ni pamoja na kupata misaada kutoka nchi mbalimbali za nje.
Pamoja na juhudi za kuwepo na Hospitali ya Saratani ya Ocean Road ya Dar es Salaam na ile ya Bugando, Mwanza Prof. Aning ametoa wito kwa Tanzania kuendelea na jitihada za kuweka kipaumbele kwenye kudhibiti na kutibu ugonjwa wa saratani kwa wananchi wake.
Aidha, aliongeza kuwa Shirika lake liko tayari kushirikiana na Tanzania kujenga Kituo Mahiri cha Tiba ya Ugonjwa wa Saratani. Alisisitiza kuwa wanachi waelimishwe kuhusu dalili za ugonjwa wa saratani na kupima afya zao mara kwa mara ili waweze kuchukua hatua mapema.Prof. Aning alisema kuwa kuna zaidi ya aina 178 za ugonjwa wa saratani.
Hivyo alitoa rai kwa wananchi kuacha kutumia sigara na kuepuka uchafuzi wa mazingira kwa kuwa kwa namna moja au nyingine zinaweza kusababisha ugonjwa wa saratani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Patrick Makungu alimueleza Prof. Aning kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Shirika lake kwa kuwa tayari nchi imekuwa ikifanya hivyo na wananchi wa Tanzania wamenufaika na misaada ya Shirika hilo kwa kuleta vifaa tiba, wataalamu na kutoa mafunzo kwa watanzania kwenye masuala mbalimbali yanayohusu matumizi salama ya mionzi na nguvu za atomiki ikiwa ni pamoja na kusaidia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania iliyopo chini ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Prof. Aning atakutana na viongozi na watendaji wa Wizara ya Afya, Taasisi ya Chakula na Dawa, Hospitali ya Saratani ya Ocean Road na ile ya Bugando, Mwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...