Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro (katikati) akisisitiza jambo wakati akifunga mafunzo ya siku 3 kwa maafisa ugani wilaya hapo yaliyotolewa na TAHA hii leo, kushoto ni mwakilishi wa shirika la TAHA Bw. Manfred Bitala na kulia ni mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Iddi Nganya.
 Miongoni mwa bwana shamba akizungumzia atakayoyafanya pindi akirudi kwenye eneo lake la kazi mara baada ya mafunzo hayo kumalizika.
 Afisa Mifugo wilaya ya Makete Dr. Nuru Issae akizungumza watakavyopambana na magonjwa ya matunda ya apples.
 Bibi Shamba akichangia hoja.
Habari/picha na Edwin Moshi, Makete

Mabwana na mabibi shamba wa kata na vijiji wilayani Makete mkoani Njombe walioshiriki warsha ya siku 3 ya namna ya kuboresha kilimo cha matofaa maarufu kama apples iliyotolewa na shirika la TAHA, wametakiwa kutekeleza kwa vitendo mikakati waliyojiwekea ya namna ya kuboresha zao hilo

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya siku 3 kwa wagani kazi hao, Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro, amerudia kauli yake kuwa suala hilo ni mkakati wa kitaifa ambao umeagizwa na rais Dk. Jakaya Kikwete, hivyo mafunzo hayo waliyopatiwa yanatakiwa kutendeka kwa kuwa yana manufaa kwa wakulima na wananchi wa Makete kwa ujumla

Mh. Matiro amesema ndani ya muda mfupi anatarajia sifa ya Makete kuwa inaongoza kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi sasa itabadilika mara moja na kuonekana kuwa inaongoza kwa kuzalisha matunda ya apples

"Nadhani mtu ukienda pale Dar es Salaam ama sehemu nyingine ukasema unatoka Makete tayari wanaelewa kuwa kuna Ukimwi, sasa hilo tunaweza kulibadilisha, kwa kwenda kuwasaidia wakulima huko mnakotoka, wazalishe apples kwa wingi kwa kufuata utaalam mliopatiwa na TAHA ili tuone mabadililo" Alisema Mh. Matiro

Amesema mikakati waliyojiwekea baada ya mafunzo hayo ni njia nzuri ya kuifikisha wilaya kule inakotaka kuhusu kilimo cha apples, ambacho kinatarajiwa kuwa kilimo cha biashara kwa lengo la kuinua uchumi wa wakulima na wilaya kwa ujumla

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Iddi Nganya amesema wagani kazi hao ndio watekelezaji wakubwa wa mikakati hiyo na ndiyo maana wakapatiwa mafunzo hayo, hivyo kila mmoja ana jukumu la kwenda kuitumia ipasavyo kwa wakulima wake

Amesema tathmini itaonekana hivi karibuni, kwani kipimo cha hayo yote ni kuona wamebadilishaje kilimo cha wakulima wao huko wanakotoka, kama ikionekana kuna utofauti itaonekana kuwa mafunzo hayo yameweza kuwasaidia, hivyo waone jitihada zinazofanywa kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa

Naye Mwakilishi kutoka shirika la TAHA ambaye alikuwa miongoni mwa mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Manfred Bitala amesema ili kufanikisha malengo hayo kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kukubali kubadilika na kuwajibika ipasavyo kwa nafasi yake

Amesema wao kama TAHA wanawajibu wao ikiwemo kutoa elimu ambayo tayari wameshaitoa, na maafisa kilimo hao nao wana nafasi yao na hali kadhalika na wakulima, hivyo jitihada za vitendo zikifanywa anaimani lengo la kilimo cha apples kuzaliwa kwa wingi na kwa ubora wa hali ya juu litafanikiwa

Dk. Nuru Issae ni Afisa mifugo wilaya ya Makete ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ambapo amesema jambo watakaloanza kulifanyia kazi mara moja ni kutambua magonjwa yanayoshambulia apples na kuyatokomeza kwa kuwa wameelezwa aina mbalimbali za magonjwa yanayoshambulia matunda hayo

Dk. Issae amesema kabla ya mafunzo haya hawakuwa na wazo kuwa magonjwa yanaweza kuzorotesha jitihada za mkakati wa kuboresha kilimo cha apple wilayani hapo, na kwa kuwa wametambua kuwa magonjwa ni kikwazo kimojawapo, watapambana nayo mara moja

Miongoni mwa mikakati iliyopangwa baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa na kampeni ya pamoja ya kuyatokomeza magonjwa yanayoshambulia apples, kushirikiana na taasisi mbalimbali na wadau binafsi wanaolima matunda hayo, kukaa na wakulima na kupanga nao namna nzuri ya kulima apples kwa manufaa kama walivyoelekezwa na mengine mengi

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Wadau mafunzo haya hapa kwetu yamekuwa mengi sana,rasilimali zinatumika lakini maisha yapo vilevile hali ya mkulima ipo palepale,hakuna matokeo yanayopimika baada ya mafunzo elekezi na washa mbalimbali.ni wakati sasa wa kubadilika tuone matokeo yanayopimika.wakuu wetu baada ya mafunzo wekeni malengo yanayopimika muda wa utekelezaji na kila mtu awajibike tuone mabadiliko.Inawezekena tuanze na mafunzo haya kubadilisha hali ya kilimo chetu.Mliopewa madaraka simamieni wakati wa porojo umekwisha tufanye kazi.
    Erasto M.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...