NAIBU Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Abdurahman Kaniki, ameipa changamoto bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kuhakikisha majengo yanayojengwa nchini yanakuwa bora na salama kwa makazi ya watu na kuepusha majanga ya majengo kuporomoka kama ilivyowahi kutokea.
Naibu IGP Alitoa changamoto hiyo jana jijini Mbeya wakati akifungua mkutano wa mashauriano baina ya maofisa wa Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu (DPP) na maofisa wa AQRB, kuhusu masuala mbali yanayohusu ujenzi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa kazi zao za kitaaluma lengo ikiwa ni kuboresha huduma.
“Tumeshuhudia majengo yakiporomoka hivi karibuni na tunajiuliza je ni kweli wataalamu wa kutosha hakuna ? lakini jibu ni kwamba wapo, sasa kinachotakiwa ni usimamizi wa karibu kuhakikisha tunawapa watanzania makazi bora na salama,” alisema.
Alisema utaratibu wa AQRB kukutana na wadau na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya ujenzi na sheria ya ujenzi namba 4 ya mwaka 2010 imekuja wakati mwafaka lakini alishauri wapanue fursa hiyo ili kuwafikia wadau wengi zaidi.
“Nyie ni wadau muhimu sana kupendezesha miji yetu ambayo kwa kweli mingine imejengwa holela holela …..hii changamoto naileta kwenu mhakikishe mambo yanafanyika kisasa, hata sisi polisi milango iko wazi kwa chochote mnachohitaji kwa ajili ya kuboresha kazi zenu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya AQRB, Ambwene Mwakyusa, alisema bodi hiyo ilianza shughuli zake mwaka 1998 na imeshakagua miradi ipatayo 14,000 katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema katika shughuli za ukaguzi ambazo bodi huzifanya kwenye kanda zake mbalimbali wamekuwa wakilishirikisha Jeshi la Polisi ili wanapopata tatizo wakiwa kazini wasaidiwe.
Mwenyekiti huyo wa bodi alimwomba Naibu IGP kusaidia kuhakikisha wabunifu na wakadiriaji majenzi walioko ndani ya jeshi hilo wanasajiliwa na bodi yake kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Msajili wa bodi hiyo, Jehad Ahmed Jehad, alisema kupitia sheria ya AQRB wamekuwa wakibuni mikakati mbalimbali ya kuhakikisha shughuli za ubunifu na ukadiriaji zinafanyika kwa weredi wa hali ya juu.
Alisema bodi yake imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za serikali kama ya wakandarasi, wahandisi na wakala wa majengo ili kuwezesha majengo yanayojengwa yanakuwa bora na salama kwa wananchi.
Washiriki wa semina wakimsikiliza Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Abdurahman Kaniki akihutubia mkutano wa mashauriano baina ya maofisa wa polisi, maofisa wa ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu (DPP) na wataalamu wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) uliofanyika jijini Mbeya
Mwenyekiti wa bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Ambwene Mwakyusa akizungumza kwenye mkutano baina ya viongozi wa Jeshi la Polisi, Maofisa kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu (DPP) na maofisa wa bodi hiyo uliofanyika Mbeya jana, pembeni yake kulia ni Msajili wa Bodi hiyo, Jehad Abdalah Jehad na kushoto ni Naibu IGP, Abdurahman Kaniki.
3: Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Abdurahman Kaniki akizungumza kwenye mkutano wa mashauriano baina ya viongozi wa Jeshi la Polisi, maofisa kutoka ofisi ya DPP na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB),jijini Mbeya. Kulia wa kwanza ni Msajili wa Bodi hiyo, Jehad Abdalah Jehad na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Ambwene Mwakyusa.
Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Abdurahman Kaniki akizungumza kwenye mkutano wa mashauriano baina ya viongozi wa polisi na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB),jijini Mbeya. Kulia wa kwanza ni Msajili wa Bodi hiyo, Jehad Abdalah Jehad na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Ambwene Mwakyusa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...