Serikali
ya China imekubali kuendesha mafunzo kwa wana michezo 30 wa Tanzania
wanaotegemewa kuiwakilisha Tanzania kwenye michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola
Julai 2014. Vilevile Tanzania na China zimekubaliana kuendeleza ushirikiano
wa kiuchumi na kidiplomasia unaoendelea kuimarika kila mwaka hususan kwa sasa
nchi hizo zinaposherehekea miaka 50 ya ushirikiano.
Makubaliano
hayo yalifanyika wakati Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na China
walipokutana mjini Beijing wiki iliyopita kuzungumzia masuala yanayohusu maeneo
ya ushirikiano wa nchi hizi. Mhe. Wang Yi alisema ushirikiano baina ya nchi
hizi ni wa kidugu na hivyo Serikali ya China itaendelea kusaidia kwa hali na
mali miradi waliyoahidi kwa maendeleo ya Tanzania na watu wake.
Mhe.
Membe ambaye alikuwa nchini China kwenye ziara ya siku tano, aliahidi kuratibu
Wizara na Taasisi za Serikali zinahusika na miradi ya ushirikiano ili
kuhakikisha matunda ya miradi hiyo yanaonekana. Mhe. Membe alisema China ni
marafiki wa Afrika lakini ni marafiki wa karibu wa Tanzania hivyo sherehe za
miaka 50 ya uhusiano huo zidhihirishwe na miradi ya mafanikio ambayo nchi zote
mbili zimekubaliana kwa maendeleo ya watu wake.
Mbali na
misaada ya vifaa mbalimbali vya ujenzi na huduma za maji na afya, hadi sasa
Serikali ya China imekamilisha miradi mikubwa ya ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano
wa Mwalimu Nyerere, ukarabati wa Uwanja wa Amaan Zanzibar, ujenzi wa Kituo cha
Utafiti wa Kilimo Ifakara na ujenzi wa shule mbalimbali. Miradi mingine kadhaa
inaendelea sasa ukiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es salaam. Miradi mingine mingi iko kwenye majadiliano kama vile
ujenzi wa jengo la Wizara ya Mambo ya Nje, awamu ya pili ya Mkongo wa Taifa,
Nishati ya Umeme wa Upepo Singida, Bandari ya Mbegani Bagamoyo na ukarabati wa
Reli ya TAZARA.
Akiwa
kwenye ziara hiyo, Mhe. Membe pia alikutana na Makamu wa Rais wa China Mhe. Li
Yuanchao ambaye alielezea China inaitazama Tanzania kama mshirika mwenza kwenye
maendeleo, hivyo uhusiano wa nchi hizo una manufaa sawa kwa pande zote mbili.
Alisema ukuaji wa uchumi wa nchi nyingi za Kiafrika umesababisha Serikali yake
kushawishi wawekezaji wengi kuwekeza Afrika, lakini hali ya usalama na utulivu
nchini Tanzania inawavutia wengi kuwekeza zaidi huko.
Mhe.
Membe na ujumbe wake pia walikutana na kufanya mzungumzo na Makamu Waziri wa
Biashara Mhe. Li Jinzao ambapo aliainisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na
China kwa sasa. Mhe. Jinzao alisema mbali na miradi mingi inayoendelea kwa sasa
mradi wa kukarabati Reli ya TAZARA unapewa kipaumbele na Serikali ya China
kwani ndio mradi wa kwanza baina ya nchi hizi mbili.
Katika
mazungumzo yake na Makamu Waziri wa Usalama wa Raia Mhe. Wang Hanning, Waziri
Membe alipendekeza kuanzisha ushirikiano wa karibu baina ya Wizara ya Usalama
wa Raia China na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania ili kusaidiana katika
kutatua changamoto mbalimbali za kiuhalifu duniani. Mhe. Hanning alikubali
pendekezo hilo na kueleza kuwa kwa sasa uhusiano wa wananchi wa nchi mbili
umeimarika, kuna raia wengi wa China nchini Tanzania na kinyume chake. Hivyo ni
wakati muafaka kwa Wizara hizo mbili kuanza ushirikiano wa karibu kwa manufaa
ya wananchi wa pande zote mbili.
Mhe.
Membe na ujumbe wake pia walifanya mikutano na Makamu Meya wa Jiji la Shenzhen
Bw. Chen Biao na Makamu Gavana wa Jimbo la Guangdong Bibi Zhao Yufang na ujumbe
wa Serikali ya Guangdong.
Waziri
Membe alimalizia ziara yake kwa kukutana na viongozi mbalimbali wa biashata na
makampuni ya sekta binafsi ambao wengi wao ndio wahusika wa miradi mbalimbali
inayotekelezwa nchini Tanzania kwa ushirikiano na China.
Imetolewa na: KITENGO CHA
MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA,
DAR ES SALAAM
5 MACHI, 2014
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...