Na Ally Kondo, Lilongwe
Nchi za Afrika zimehimizwa kufanya biashara baina yao ili kujiletea
maendeleo, badala ya kusubiri misaada isiyokuwa na uhakika kutoka nchi
wahisani. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Salum
(Mb) wakati wa hafla ya uwekaji saini Mkataba wa kuanzisha Kituo cha
Pamoja cha Uhamiaji na Ushuru wa Forodha cha Songwe - Kasumulu kati ya
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Malawi.
Uwekaji saini huo ulifanyika Lilongwe, Malawi leo Jumatatu tarehe
10 Machi, 2014 ambapo Mhe Salum aliweka saini kwa niaba ya Serikali ya
Tanzania, wakati Waziri wa Biashara na Viwanda, Mhe. Sosten Gwengwe
aliweka saini kwa niaba ya Serikali ya Malawi.
Mhe. Salum alieleza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho, kutasaidia, sio
tu kupunguza gharama za kufanya biashara kati ya Tanzania na Malawi
bali pia kutaimarisha uhusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili ambao
kimsingi wana utamaduni unaofanana.
Mhe. Waziri aliwataka wataalamu wa pande zote mbili kuandaa mpango
kazi wa kutekeleza Mkataba huo haraka iwezekanavyo ili wananchi na
Serikali waone matunda yake badala ya kuishia katika makaratasi.
Alipoulizwa na wanahabari kutoa maoni kuhusu utekelezaji wa Mkataba
huo, Mhe Wazri aliwahakikishia wananchi wa Malawi na Tanzania kwa
ujumla kuwa kituo hicho kitafanya kazi kama ilivyokusudiwa na hakuna
tishio lolote la kuvurugika kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake, Mhe. Gwengwe alifarijika na uanzishwaji wa kituo
hicho, kwa kuwa kitarahisisha usafirishaji wa bidhaa kwa haraka kutoka
Tanzania kuingia Malawi ambayo haina Bandari.
Uwekaji saini wa Mkataba huo umeenda sambamba na mkutano wa Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)
ambapo Mhe. Salum anaongoza ujumbe wa Tanzania.
Mkutano huo ulioanza
na vikao vya Makatibu Wakuu unatarajiwa kukamilika kesho 11 Machi,
2014.
Mhe. Salum, kulia akitoa neno baada ya shughuli za kusaini Mkataba kukamilika. Anayemsikiliza ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Malawi, Mhe. Gwengwe. |
Maafisa wa Tanzania na Malawi wakifanya maandalizi kabla ya Mawaziri kuwasili kwa ajili ya shughuli ya uwekaji saini Mkataba |
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...