Wananchi wa wilaya ya Mbinga wameonywa dhidi ya vitendo vya kuhujumu miundombinu ya barabara Peramiho Jct-Mbinga iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa kufanya shughuli ya uchimbaji madini kinyume cha sheria.
Agizo hilo amelitoa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu wakati alipofanya ziara ya ghafla katika kambi ya wachimbaji wadogo wa madini kitongoji cha Ngendambili kijiji cha Mkako wilaya ya Mbinga
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amejionea jinsi wachimbaji hao walivyoharibu eneo la hifadhi ya barabara kwa kuchimba mashimo makubwa kwa lengo la kutafuta madini ya vito yanayodaiwa kupatikana katika eneo hilo.
Amesikitishwa na kitendo cha wananchi hao na kuwaeleza kuwa serikali imefanya jitihada kubwa za kujenga barabara hiyo ya lami kutoka Peramiho hadi Mbinga mjini .
Barabara hii ya lami yenye urefu wa kilometa 78 na imegharimu Shilingi Bilioni 79.80 sawa na dola za Marekani Milioni 59.84 hadi kukamilika kwake.
“Barabara hii hata kuzinduliwa rasmi bado lakini ajabu ninyi wachimbaji haramu wa madini mmeanza kuihujumu kwa kuharibu kwa kigezo cha kutafuta vito. Hapana...serikali haitokubali kuona uharibifu huu ukiendelea” alisema Mwambungu
Ameongeza kusema inasikitisha kuona kazi ya uchimbaji huu haramu inafanyika usiku ambapo ni hatari sana kwa usalama wa wachimbaji.
Amewasihi kuondoka mara moja katika eneo hilo na kutafuta eneo jingine linaloruhusiwa kuchimbwa madini kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mwambungu alisisitiza kuwa “ni lazima viongozi kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya mhakikishe mnalinda miundombinu ya barabara na eneo lote la hifadhi yake ili lisiharibiwe na kazi ya uchimbaji madini usiofuta sheria na kanuni”.
Kufuatia hali hiyo amelitaka jeshi la polisi na magereza mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanalinda eneo hilo lililovamiwa na wachimbaji wadogo ili kuwadhibiti wahalifu hao.
Eneo lililovamiwa na wachimbaji wadogo linamilikiwa na gereza la Kitai wilaya ya Mbinga.
Aidha amewaagiza meneja wa TANROADS na afisa madini wa mkoa kuhakikisha wanachukua hatua za kufukia mashimo yote yaliyopo pembezoni mwa barabara hiyo haraka na kisha kupanda miti rafiki kwa utunzaji wa mazingira.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma Mhandisi Abraham Kisimbo amesema kwa mujibu wa sheria ya barabara hifadhi ya barabara ni mita 30 kutoka katikati ya barabara kwa pande zote mbili hivyo ni vema wananchi wakaepuka kufanya shughuli yeyote ndani ya eneo la hifadhi.
Katika hatua nyingine watu 9 wamekamatwa na tayari wamefunguliwa mashtaka mahakamani na jeshi la polisi wilaya ya Mbinga kwa kosa la kuhujumu miundombinu ya barabara kwa kuchimba madini ndani ya hifadhi ya barabara kuu ya Peramiho Jct-Mbinga.
Barabara ya Peramiho-Mbinga ilianza kujengwa mnamo mwezi Agosti 2010 na imekamilika mwezi Agosti 2013 ujenzi ulifanywa na mkandarasi Sino Hydro Corporation Limited kutoka nchini China .
Ujenzi wa barabara hii ambayo ni mojawapo ya mkakati wa serikali ya awamu ya nne kuhusu ujenzi wa barabara ukanda wa uchumi wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) ni msaada muhimu kwa kufungua makao makuu ya mkoa wa Ruvuma na wilaya zake za Mbinga na Nyasa na pia nchi ya Malawi.
Barabara hii imejengwa kwa ufadhili wa serikali ya Marekani kupitia mradi wa Changamoto ya Millenia -Tanzania (MCA-T).
Barabara ya Peramiho Jct-Mbinga inavyoonekana baada ya kukamilika ujenzi wake kwa kiwango cha lami lakini sasa ipo hatini kuhabika kutokana na kuvamiwa na wachimbaji wadogo haramu wa madini katika kijiji cha Mkako wilaya ya Mbinga
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu (wa nne kutoka kushoto) akitazama mashimo yaliyochimbwa na wachimbaji wadogo wa madini katika kambi ya Ngendambili kijiji cha Mkako wilaya ya Mbinga.Mashimo haya yamo ndani ya hifadhi ya barabara ya lami
Mashimo yaliyoachwa na wachimbaji wadogo wa madini ya vito yakiwa ndani ya mita 30 za hifadhi ya barabara.Haya yanahatarisha barabara kukatika kwani yapo pande zote mbili za barabara hii ya Peramiho-Mbinga eneo la kijiji cha Mkako wilaya ya Mbinga.
Picha na habari na Revocatus Kassimba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...