Watanzania
wameshauriwa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu ili kuchota maarifa mbalimbali
na kuwasaidia katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Wito
huo ulitolewa na mwandishi wa vitabu, Bw. Evodius Katare (pichani) ambaye pia ni Kaimu
Mkurugenzi wa Utawa na Fedha wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka
(DART) akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
“Watanzania
wakijenga utamaduni huu wa kusoma vitabu itawasaidia sana kimaisha,” alisema na
kuongeza kuwa kusoma vitabu ni kuchota maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi.
Akitoa
mfano alisema watu wakipenda kusoma vitabu pia watapenda kuandika vitabu ili
wengine waweze kusoma.
Alisema
yeye anapenda kusoma vitabu na utamaduni huo umemsaidia pia kuwa na tabia ya
kuandika vitabu.
“Tabia
ya kusoma vitabu imenisaidia kuwa mwandishi wa vitabu japo taaluma yangu siyo
mwandishi,” alisema.
Kitabu
chake kipya kinaitwa “Julius Nyerere, Falsafa zake na dhana ya Utakatifu.”
Alisema
ameandika kitabu hicho kutokana na Kanisa Katoliki kutangaza mchakato wa
kumfanya Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu na uelewa mdogo wa jamii
hasa vijana kuhusu mchango wake kwa taifa hili.
Anaungana
na kanisa hilo kwa kutaka kumpatia zawadi hiyo kubwa Nyerere na kwamba
anastahili kuipata kutokana na matendo yake ya uongozi aliyoifanyia nchi hii.
“Mwalimu
Nyerere alikuwa mwanasiasa na kiongozi aliyeifanya jamii ya watanzania kuwa
sehemu ya familia yake na hiyo ikawa tunu kwenu ya uwepo wa amani na utulivu,”alisema
Bw.Katare.
Alisema
katika kipindi chote cha uhai wake alitumia muda wake kuwatumikia watanzania,
aliongoza harakati za kuikomboa nchi na pia aliliongoza taifa kwa uadilifu baada
ya uhuru.
Alisema
kitabu hicho kitaiwezesha jamii hasa vijana ambao hawakuishi kipindi cha
Mwalimu kumfahamu ili wawe na fursa nzuri wanapotaka kumfananisha na wanasiasa
wanaojitokeza leo ambao wengi wanajali familia na maslahi yao tu.
Alieleza
kuwa watu wasome kitabu chake hicho ili waweze kumfahamu zaidi mwalimu Nyerere na
mchango wake kwa taifa hili.
“Kitabu
hiki kitasaidia pia vizazi vijavyo kufahamu historia nzuri juu ya Mwalimu
Nyerere,”alisema Bw.Katare
Alisisistiza
kwamba tabia ya kusoma na kuandika vitabu hujengwa tangu awali vijana wakiwa
wadogo katika mashule.
Alisema
kuna kila sababu ya Tanzania kujenga maktaba shule zote za msingi na sekondari na
kuwa na walimu wa kuhamasisha wanafunzi kusoma vitabu ili kuwa na jamii bora
zaidi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...