Na Concilia Niyibitanga MAELEZO 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2014, katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, mkoani Kagera Mei tarehe 2. Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na Waandishi wa Habari Mjini Bukoba kuhusu Mbio hizo.

Mwenge huo utakaobeba ujumbe usemao “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi” wenye kauli mbiu “Jitokeze kupiga kura ya maoni tupate Katiba Mpya” utakimbizwa katika Halmashauri/Manispaa 165 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kilele chake kitakuwa Mkoani Tabora tarehe14/10/2014.

Ujumbe kuhusu mabadiliko ya Katiba kwa mwaka huu, umeandaliwa mahususi kwa lengo la kuwahimiza wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa ambao mwisho wake ni wananchi kupiga kura ya maoni ili tupate Katiba Mpya iliyoboreshwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Amesema Dkt. Mukangara.

Amesema kuwa ujumbe huu utaambatana na kauli za uhamasishaji kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI, Malaria, Rushwa na Matumizi ya Dawa za Kulevya. Dkt. Mukangara ameeleza kuwa nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto ya ugonjwa hatari wa UKIMWI, Malaria, matumizi ya dawa za kulevya na rushwa, hivyo mwaka huu kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru Serikali itaendelea kuwahimiza wananchi kupambana kwa dhati ili kumaliza changamoto hii inayoathiri maisha ya Watanzania.

“Hata hivyo, Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na kuendelea kuhimiza umuhimu wa amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa; Serikali kupitia Mbio hizi imekuwa ikiwahamasisha Wananchi, Mashirika, Taasisi na Wadau mbalimbali kuchangia kwa hali na mali kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo”. Amesema Dkt. Mukangara.

Amekumbusha kuwa falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni kumulika maovu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu, kuleta matumaini ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.

Aidha, Dkt. Mukangara ametoa wito wito kwa wananchi hasa kwa vijana wa Tanzania kutumia Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa lengo la kuimarisha amani, upendo na umoja wa Kitaifa.

Pia amewataka wananchi kutumia ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kama chachu ya kuleta mabadiliko ya kijamii hususani pale inapotolewa elimu kuhusu Mapambano dhidi ya UKIMWI, mapambano dhidi ya Rushwa na mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya.

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa huratibiwa kwa pamoja kati ya Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo (Tanzania Bara) na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto (Zanzibar).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...