Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally N. Rufunga amewataka wafugaji wanaoishi katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kutovuka mto Manonga na kuingia katika wilaya ya Igunga wakati serikali inashughulikia suala la mpaka wa wilaya hizo mbili.
Mhe Rufunga ametoa maelekezo mapema jana alipokutana na wafugaji hao katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu, ikiwa ni moja ya makubaliano ya kikao cha Kamati za ulinzi na usalama za mikoa ya Tabora na Shinyanga kuwa kila upande wananchi waelimishwe kutumia ardhi na kuwa watulivu wakati huu serikali inapofanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mgogoro na kufuatilia mpaka halali wa eneo hilo.
Awali wafugaji waliieleza kamati ya Ulinzi na Usalama ambayo Mkuu wa mkoa ni mwenyekiti, kuwa mpaka halisi ni mto Mwanyerere (Manonga) lakini mto huo ulihama kutokana na mvua mwaka 1998 na sehemu kubwa uliingia eneo la Kishapu hivyo eneo lao la kitongoji cha Magogo likabaki upande mwingine na wamekuwa wakichungia huko kwa muda mrefu hadi hapo wakulima wa wilaya ya Igunga walipovamia eneo hilo ndipo vurugu zilianza.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha wafugaji Kanda ya Ziwa Bw. Mrida Mshota amewasihi wafugaji wa kijiji cha Magalata kutulia na kusubiri taratibu za serikali kwani suala hilo limeanza kushughulikiwa muda mrefu tangu serikali ilipopata taarifa za uvamizi huo, chama cha wafugaji pia kinashirikiana kwa karibu na serikali kuhakikisha haki inapatikana.
Mgogoro huo unatokana na kugombea eneo kati ya wakulima wa kijiji cha Isakamaliwa wilayani Igunga mkoani Tabora ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu waliopewa eneo hilo na serikali ya mkoa ya Tabora kwa ajili ya kujiajiri kwa njia ya kilimo, wakati huohuo wafugaji wa kijiji cha Magalata wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga wenye asili ya Kitaturu wakidai wamevamiwa eneo hilo kwani wamelisha mifugo yao kwa miaka mingi hapo.
Serikali ya Mkoa wa Shinyanga na Tabora zinaendelea kushughulikia tatizo hilo lililosababisha vifo vya watu watano na majeruhi mmoja ambapo tume ya watu 18 imeshaundwa na kupewa muda wa wiki nne kufanya uchunguzi wa chanzo hasa na kujua mpaka halali wakati wananchi wakiendelea kuelimishwa kuwa na subira.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Ally N. Rufunga akizungumza na wananchi wa kijiji cha Magalata wilayani Kishapu kuhusu vurugu zilizotokea za kugombea eneo la malisho na wakulima wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Mwenyekiti wa chama cha wafugaji Bw. Mrida Mshota akiwasihi wafugaji kuiamini serikali hivyo wawe na subira kufuatia mgogoro kati yao na wakulima wa Isakamaliwa Igunga.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Shinyanga ambaye ni Mkuu wa Mkoa (hayupo pichani) Ally N. Rufunga akitoa maelekezo kufuatia mgogoro wa eneo kati ya wafugaji wa Magalata na wakulima wa Isakamaliwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...