Na Ripota wa Globu ya Jamii.
OFISI ya mkurugenzi wa Mashtaka Nchini imemfutia mashtaka ya
mauaji,mmoja kati ya watuhumiwa nane wa mauaji ya kukusudia
dhidi ya
mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite bilionea , Erasto Msuya (43).
Hati ambayo imetumika kumwachia huru Joseph Damas (Chusa) ambaye pia
ni mfanyabiashara maarufu wa madini hayo imetolewa na kusainiwa
na
mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Elieza Feleshi na kisha Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuiwasilisha kwa Hakimu anayesikiliza
kesi hiyo, Munga Sabuni .
Hati hiyo ambayo hufahamika kama “Nolle Prosecution “ilitolewa mbele
ya mahakama hiyo April 16 mwaka huu kwa ajili ya kuingiza rasmi katika
kumbukumbu za Mahakama.
“Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii, umekamilika na
ikikupendeza, upande wa mashitaka tunaomba tarehe nyingine kwa ajili
ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya mashahidi kabla ya kulipeleka
jalada lenye mashitaka haya, Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza
kusikilizwa kwa kesi ya mauaji ya kukusudia namba 06 ya mwaka
2013.”alieleza Julius Semali wakili wa serikali.
“Tumepokea hati ya kuachiwa huru kwa mshitakiwa namba 07, Joseph
Damas,”alisema Wakili Semali.
Baada ya kupokelewa kwa taarifa hiyo, Hakimu Munga aliahirisha kesi
hiyo hadi Mei 06 mwaka huu na kuamuru washitakiwa saba, waliosalia
katika kesi hiyo kurejea rumande hadi hapo, shauri hilo
litakapotajwa
tena mahakamani hapo ikiwa ni kwa ajili ya kusoma maelezo ya mashahidi.
Bilionea Msuya aliuawa mwezi Agosti mwaka jana kwa kupigwa, majira ya
saa 6:30 mchana kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, eneo la
Mijohoroni, Wilaya ya Hai, Karibu na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA) na kufa papo hapo.
Washitakiwa wanaokabiliwa na kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia ni
Sharif Mohamed Athuman (31), Mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa
Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama Mredii
(38), mkazi wa Songambele Wilaya ya Simanjiro na Mussa Juma Mangu
(30), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu mkoani Arusha.
Wengine ni Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Mohammed
Jabir a.k.a “Msudani” au “Mnubi”(32), mkazi wa Dar es salaam na
Lang’ata Wilayani Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Kijiji cha
Lawate, Wilaya ya Siha na Alli Musa Majeshi, mkazi wa Babati mkoa wa
Manyara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...