Na Frank Mvungi-Maelezo 
Filamu ya Chini ya Kivuli cha Jua kuzinduliwa Jijini Dar es salaam wiki ijayo ikiwa ni moja ya hatua za kuelekea maadhimisho ya Mkutano wa Kimataifa kuhusu ualbino unaotarajiwa kufanyika hapa nchini mapema mwezi Mei mwaka huu. 
 Hayo yamesemwa na Afisa Mahusiano na Habari wa Chama cha Albino Tanzania Bw. Josephat Torner wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam kuhusu uzinduzi wa filamu hiyo. 
 Bw. Josephat alisema kuwa katika uzinduzi wa Filamu hiyo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda na uzinduzi unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Alliance De Francaise uliopo Upanga Jijini Dar es salaam. Akifafanua Bw. Josephat amesema kuwa lengo kuu la filamu hiyo ni kuwaelimisha watanzania kuhusu matatizo yanayowapata watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) hapa nchini ili jamii iweze kushiriki kikamilifu katika kuondoa matatizo yanayowakabili. 
 Aliongeza kuwa filamu hiyo imeandaliwa hapa nchini na baada ya uzinduzi wake itaonyeshwa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa muda wa miezi 9 ikiwa na lengo la kuwafikishia ujumbe wananchi kuhusu hali halisi ya maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Katika ziara ya kuonesha filamu hiyo Bw. Josephat amesema kuwa wataambatana na Madaktari wataalam wa ngozi watakaosaidia kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matatizo ya watu wenye ulemavu wa ngozi na hatua za kuchukua ili kuwakinga na athari zinazotokana na mazingira. 
 Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Standing Voice lililofadhili mradi wa uandaaji wa Filamu hiyo Bw.Jon Beale alisema filamu hiyo inaujumbe wa kutaka kuonyesha ulimwengu hali halisi ya maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na hatua ambazo jamii inapaswa kuchukua katika kuwalinda wale wenye tatizo hilo. 
 Watanzania wamepewa wito wa kushiriki vyema katika kuelimisha jamii kuhusu matatizo ya watu wenye ualbino hapa nchini ili kujenga jamii yenye kuzingatia misingi ya haki na usawa.
 Filamu hiyo imeshaonyeshwa katika nchi zisizopungua 50 tangu mwaka 2012 ambapo baadhi ya nchi hizo ni Mexico, Brazil, Marekani, Australia, Norway, Sweeden, Dernmark pamoja na nchi nyingine za Ulaya na mabara mengine.
 Afisa Mahusiano na Habari wa Chama cha Albino Tanzania Bw. Josephat Torner akizungumzia uzinduzi wa filamu hiyo jijini Dar es salaam leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Standing Voice lililofadhili mradi wa uandaaji wa Filamu hiyo Bw. Jon Beale akiongea

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Wabunifu wa filamu endelezeni ubunifu huu wa kutengeneza filamu zenye mafundisho.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...