Katika karne iliyopita, wasomi mbali mbali wakiwepo wanauchumi, pamoja na wataalamu wa maswala ya kijamii waligundua umuhimu wa rasilimali watu katika kukua kwa uchumi wa dunia. Kuwepo kwa elimu bora, na ujuzi katika nafsi ya binadamu huwasaidia watu kujitengenezea vipato vikubwa. Tanzania inahitaji idadi kubwa ya rasilimali watu ili iweze kupiga hatua kubwa za kiuchumi.

Kuwepo kwa mali asili kama madini, mafuta na gesi asilia kwa kiwango kikubwa imekuwa laana kwa mataifa kwani yamekuwa vyanzo vya unyanyasaji wa kijamii na umasikini uliopitiliza kwa jamii zisizokuwa na rasilimali watu ya kutosha ili kuzisimamia na kuziendeleza.

Baada ya vita vya pili vya dunia, Ujerumani ilikuwa katika wakati mgumu wa kujinyanyua kiuchumi. Miundombinu mingi iliharibiwa kipindi cha vita. Na Ili kujinyanyua kutoka katika uharibufu mkubwa uliosabishwa na vita,  serikali ya Ujerumani ilibuni mfumo wa elimu ambayo ilielekeza juhudi zake katika kutayarisha rasilimali watu. Elimu ilipewa kipaumbele; Ilifanywa kuwa ya bure na ya lazima kwa kila mjerumani. Mfumo huu wa elimu ulifanywa kuwa wa vitendo zaidi na lazima kwa kila mtoto mwenye umri wa miaka tano hadi kumi na tisa, huku kila mwanafunzi akipewa nafasi kuchagua cha kujifunza kutokana na uwezo wake lengo kubwa ikiwa ni kutayarisha rasilimali watu.

Jitihada hizi za serikali ya Ujerumani ilizaa matunda makubwa ambayo yaliitwa miujiza ya kiuchumi. Leo, uchumi wa Ujerumani ndio uchumi mkubwa zaidi katika bara la Ulaya, na pia ndio mdhamini mkubwa wa mataifa taabani kiuchumi kama Ugiriki, Hispania nk. Ujerumani ni moja ya mataifa yaliyo juu zaidi kwenye maswala ya uhandisi inaongoza kwa uhandisi. Ujerumani inaongoza kwa uzalishaji wa viwanda ikiuza nje ya nchi bidhaa yenye thamani ya dola za kimarekani trillion 1.52 kwa mwaka 2012 tu. Haya ni mafanikio yaliyotokana na kuipa elimu kipaumbele, pamoja na matumizi ya rasilimali watu zilizoko ndani na nje ya nchi.

Mataifa yasiyokuwa na mali asili nayo yameonyesha ubunifu wa hali ya juu. Israel kwa mfano, ni taifa dogo lenye rasilimali chache, huku ikizungukwa na maadui ambao lengo lao kubwa ni kuliangamiza. Ikiwa imezingirwa na maadui kila kona pamoja na kukosa rasilimali za asili, Israel imelazimika kutumia rasilimali watu ili isiangamizwe kijeshi na kiuchumi.

Licha ya kujitengenezea baadhi ya taasisi bora za kielimu na utafiti duniani, Israel iligeukia wataalamu wenye asili ya kiyahudi waliotapakaa katika kila pembe ya dunia, ikiwapa uraia watu wote wanaotaka kurudi nchini humo. Leo Israel ndio moja ya nchi iliyoendelea zaidi kiteknolojia. Vyuo vikuu vya Israel vimezalisha wataalamu wa kila aina ambao  wanasaidia nchi hiyo kujiendeleza kiuchumi na kujilinda kijeshi.

Baada yakugundua kwamba hatma yake haikuwa nzuri kiuchumi na kijamii, Singapore, nchi ndogo barani Asia ilianzisha mapinduzi ya miundombinu , viwanda, mawasiliano, na ya kielimu ili iweze kustahimili mabadiliko ya kiuchumi ya baadae. Leo, Singapore ni nchi ya nne duniani kwenye maswala ya kifedha na mmoja wa magwiji katika masoko yanayochipukia. Korea kusini nayo haina tofauti na Singapore, kwani ilikuwa masikini zaidi ya Kenya mwaka 1960. Leo hii Korea ya Kusini ina uchumi wenye thamani ya dola za kimarekani trillion 1.56 ambayo ni mara 47 ya Kenya. Hii yote imetokana na jitihada zake za kuzalisha rasilimali watu.

Marekani imekuwa ni taifa lenye nguvu zaidi ya nchi yoyote ile duniani kiuchumi, kiteknolojia na kijeshi. Kwa kipindi kirefu sasa. Mapinduzi ya viwanda ya karne ya 19 iliisukuma nchi hiyo kutumia kila mbinu ; Marekani ilitumia rasilimali zake zote ikiwemo rasilimali watu. Mafanikio ya taifa hili kubwa duniani hayakuwa ya kubahatisha, yametokana na kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa, na pia kujivunia kile wanachokifanya.

Wamarekani wamewekeza kwenye elimu kwa kiwango kikubwa. Wameanzisha vyuo vikuu vya elimu na utafiti bora kuliko zote duniani. Sera zao za uhamiaji zimekuwa kivutio kwa wataalamu bora kutoka  kila pembe ya dunia ili tu watu wenye vipaji waendelee kusadia taifa hili kuendelea kuongoza kiuchumi. Hazina kubwa ya Tanzania imetapakaa ulimwenguni. Wataalamu mbali mbali wenye asili ya kitanzania wametapaa kila pembe ya dunia wakitafuta maisha huku wakichangia maendeleo ya mataifa mengine kutokana na kukosa uhuru wa kuchangia nchi yao ya kuzaliwa.

Wataalamu wenye asili ya Kitanzania wapo katika taasisi kubwa za kitafiti nchini marekani na mataifa mengine makubwa; wapo kwenye mashirika makubwa ya kifedha, wapo kwenye taasisi kubwa za afya nk. Mifano ni mingi ambayo siwezi kuielezea yote kwa leo, ila lengo langu ni kuielemisha jamii yetu kuhusiana na umuhimu wa watanzania waishio ughaibuni

Ushindani mkubwa wa kiuchumi katika eneo la maziwa makuu ni msukumo tosha kwa Tanzania kutumia kila mbinu inayoweza kuwa mstari wa mbele tukizingatia kwamba, Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika yenye utajiri mkubwa; kwani imebarikiwa na kila aina ya rasilimali muhimu ambazo zingesaidia kuharakisha maendeleo yake. Ugunduzi wa gesi asilia na mafuta, madini pamoja na mbuga zake za wanyama ni rasilimali adimu na  muhimu kulikwamua taifa kutoka katika wimbi la umasikini.

Kinachohitajika ni rasilimali watu; Kinachohitajika ni wataalamu wenye asili ya kitanzania waliopo ndani na nje ya nchi kushirikiana ili kuleta maendeleo ya haraka. Lazima watu wote wenye asili ya Kitanzania wapewe haki yao ya kikatiba pamoja na nafasi ya kushiriki kulijenga taifa, kijamii, kiuchumui na kisiasa

Kamwe Tanzania haiwezi na haitaweza kuendelea ikitegemea wageni. Watakaoleta maendeleo na mabadiliko makubwa ni watanzania wenyewe. Mipaka ya dunia imefunguka katika hii karne ya ishirni na moja. Badala ya kukumbatia misaada inayotudhalilisha na wageni wanaoiba rasilimali zetu, tutumie hazina kubwa tuliyonayo ya  rasilimali watu, ili tuweze kujikwamua kutoka katika wimbi la umasikini.

Wataalamu wa kitanzania waliotapakaa duniani, wanastahili haki ya kurudi kwenye ardhi yao ya kuzaliwa bila vikwazo vya aina yoyote. Katika kuandaa katiba mpya ya Tanzania, tusifanye kosa la kuwafungia nje ndugu zetu walio ughaibuni  kwa kuwa na  vibali vya kuishi na kusafiri. Ikumbukwe kwamba,  pamoja na kuwa na vibali hivyo, bado asili zao na mioyo yao itabaki Tanzania. Tusiruhusu historia ituhukumu hasa katika kipindi hiki ambapo ushindani wa maendeleo ya kiuchumi unazidi kuongezeka duniani
Mungu Ibariki Tanzania


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Ndugu Mashaka,

    Ahsante sana kwa Makala murua ktk Lugha yetu ya Kiswahili ambapo wengi wataweza kuelewa yenye Mtaji mkubwa sana na mashiko.

    Ingawa Msimamo wangu juu wa kukubali Suala la PASIPOTI MBILI sija shawishika na saba nyingi mnazotoa bado nipo ktk MSIMAMO MKALI WA PASIPOTI MOJA!

    NAOMBA NIULIZE MASWALI HAYA HAPA CHINI:

    1.Kama mnatambua Rasilimali watu ni muhmu sana kwa nchi, ina maana kwa wakai wote mchango wowote iwe kimali, kihalia ama kimawazo unahitajika sana ktk kujenga Uchumi wa Tanzania, JE, MFANO WEWE NI MTAALAMU W BENKI NI TAFITI NGAPI UMESHA FANYA KWA KUZIELEKEZA NA FAIDA KWA TANZANIA?

    JE, UNA MAANDISHI YEYOTE HATA KAMA YANGALI YAPO KTK MAKABRASHA JUU YA MAWAZO YA KUIJENGA TANZANIA?, MUDA WT ULIKUWA UANGOJA NINI USIYATOE?

    2.SUALA LENU LA KUTAKA URAIA PACHA LIMEKUJA WAKATI MGUMU KWA KUWA KUNA MJADALA MKALI WA BUNGE LA KATIBA UNAO EGEMEA SANA KTK HOJA YA MUUNGANO NA MASLAHI YA PANDE BAA NA VISIWANI HADI LENU LINAKUWA HALIPEWI UZITO, JE MTATUHAKIKISHIA VIPI KAMA WOTE MNAODAI URAIA PACHA SIO KWA MASLAHI YA MPITO NA NI KWA NIA NJEMA NA UZALENDO?

    -INAELEWEKA WAPO WANAODAI URAIA PACHA ILI KUTIMIZA MALENG YAO YA GIZANI KAMA UKWEPAJ KODI NA UHALIFU.

    -WAPO WANAOTAKAURAIA PACHA KWA LENGO LA KUSAKA UONGOZI TANZANIA, WAKTI UONGOZI UNAHITAJI SANA NIA NJEMA NA UAMINIFU.

    -NI WAZI YA KWA NCHI NYINGI ZENYE URAIA PACHA, UTARATIBU WA KUWAPATA VIONGOZI HASA WA NGAZI ZA JUU INAHITAJIKA MHUSIKA AWE NA URAIA WA NCHI MOJA TU HATA KAMA NCHI INARUHUSU URAIA PACHA.

    HIVYO MADIASPORA, MTITEGEMEE KTUAKA URAIA PACHA ILI KUWA VIONGOZI WA NGAZI ZA JUU, MTAKUWA VIONGOZI LAKINI WA NGAZI ZA CHINI TU.

    3.JE, MTATUHAKIKISHIA VIPI KAMA ENDAPO TUTAWAKUBALI KUWAPA URAIA PACHA NNYI MADIASPORA HAMTA ILETEA MAAFA TANZANIA NA WATU WAKE?

    -INAFHAMIKA WAZI PANA NCHI DUNIANI AMBAZO UKIWA RAIA WAKE DAIMA UNA KINGIWA KIFUA UWAPO NJE YA NCHI HATA KAMA NI MHALIFU KWA UTHIBITISHO NA USHAHIDI.

    Nadhani mkizingatia Utangulizi huo hapo juu ktk maswali hayo
    matatu (3) Madiaspora wengi mtaweza kuelewa zaidi kikwazo na pana uezekano mkafikia lengo l kuupata Uraia Pacha maana mtakuwa mmetatua kinacho wakwamisha kukubaliwa!

    ReplyDelete
  2. NIngependa kuangalia kwenye uhalisia zaidi, je kuna mtu mwenye asili ya Tanzania aliyechukua uraia wa nje ambaye kuna kitu tofauti atafanya kama akipewa uraia wa nchi mbili sasa?je, kuna yeyote kwasasa ambaye hafanyi kitu Tanzania kwa mfano kuwekeza au kujenga kwasababu hana uraia wa nchi mbili?katika kujibu maswali haya unatakiwa kumfikilia mtu umjuaye aliye katika hali hii. Maana mimi najuwa watu wengi wenye asili ya Tanzania lakini uraia wa nje wanawekeza, wanamiliki ardhi na kujenga kama kawaida. Ingawa ni kinyume cha sheria lakini wanafanya vyote na watanzania kwa asili ingawa sio kisheria huwa hatuwanyanyapalii watu wenye asili ya kitanzania hata kama wana uraia wa nchi nyingine. Hii ndio hali halisi, mambo ya uraia wa nchi mbili ni mazuri kwenye karatasi na kisheria lakini yakiruhusiwa hayata badili kitu kwa upande wa uwekezaji nk. kwasababu yanafanyika tiyari. Kwasababu yanafanyika tiyari mimi naona kwasasa hili swala sio priority. Naeleza hivyo kwasababu mimi nilikuwa mmoja wa watu wa diaspora tena msomi na nilifanya kila kitu, na jamaa zangu wanafanya kila kitu. jaribu kufikilia jina la mtu mmoja katika diaspora na utakubaliana na mimi kuwa wanamiliki ardhi, wamejenga, wamewekeza nk.Ambae hajafanya hivyo basi hata akipewa uraia wa nchi mbili hata fanya. Nawakilisha

    ReplyDelete
  3. Ndugu; umeeleza vizuri tu pamoja na mifano uliyotoa. Tatizo sisi katika kizazi hiki tumeshachelewa, wajanja ni wengi kuliko maelezo uliyotoa hapo. Hata hiyo Rasilimali watu unayoisema imekuwa ujanja ujanja tu. Shida ni moja, hatujaweka misingi Imara katika kuwalea vijana wetu kuwa wazalendo, wajivunie vyao, tuchukue mbinu za wageni lakini bado tujivunie Utanzania wetu. Angalia mifumo ya Elimu yetu, kila mtu anasoma anachotaka kiwe na mvuto au bila mvuto halafu mwishoni anatokomea kusikojulikana. Hi ni kwa sababu mifumo yetu haijakaa vizuri. Angalia, jinsi tunavyowaandaa watoto kielemu, hivi unadhani hao Ujerumani wamewezaje kuwa na Wahandisi kibao, na wanawezaje kuzalisha wao wenyewe bila shida, ni kwa sababu wameweka mifumo mizuri ya elimu, na Ajira na pia kipaumbele kwenye sekta moja. Sasa sisi kipaumbele chetu ni nini, tungejaribu tu kuweka kipaumbele kwenye Elimu, utalii na Madini, ungeona Tz ingekuwa wapi hii leo. Na hapa tunazidi kuchelewa tu. Leo hii tuna Wizara ya Sayansi, lakini Tanzania tunafanya Sayansi gani, labda teknolojia tu afu mbovu ya kichina! Wenzetu wana vituo maalum,mfano Marekani, na mataifa mengine, wamewajengea misingi watoto kusoma Sayansi, na kuwa na incubator za kuwafundisha watoto ili waendeleze vipaji vyao, lakini Tz tunawatafuta wazee waliogundua jiko la mkaa afu tunajivunia tunasema eti ni wagunduzi. Wagunduzi gani hao, hata darasa la 7 hajamaliza, shame kabisa. Haya hata katika utalii huo, service zenyewe ni mbovu kabisa, wapokeaji watalii sio multilingual ili kuwasaidia wageni, hii yote inatokana na mifumo mibovu ya Elimu yetu.Watoto wanamaliza form six hata hawajui watakuwa akina nani, sio ambitious tena, hatimaye wanaishia kusoma chuo ili kujipatia tu elimu ya kujipatia kipato cha njaa! Haya, ubinafsi nao unaongoza, hii inatokana na Misingi mibovu kabisa, hatuna uzalendo, uchapakazi hakuna, na tunafanya kazi kwa kibaba cha unga au mafuta, we don't save for the coming generation! kila mtu mtu mchoyo hata hao waliobaki ughaibuni ni wachoyo, wabinafsi, hata hao wanaochangia uchumi wa wengine, ni kwa sababu tu wamebanwa na mifumo, ila wakirudi Tz hata kodi hawalipi. Kila mtu anaona Tz ni tambarare. Thats absurd and insane! Hata kama kutakuwa na Katiba Mpya watu wataikiuka tu, wanaofanya ufisadi hawatanyongwa, wanaodeal na drugs hawatanyongwa, majambazi hawatanyongwa, wachafuzi wa Mazingira hawatapigwa faini, wanaoharibu miundombinu hawatachukuliwa hatua, wanaokiuka sheria barabarani, hawatalipa faini, rushwa itaendelea. SOLUTION: TUJIWEKEE MIFUMO MIZURI YA ELIMU, walimu wasomi, wanafunzi walioandaliwa vyema.

    ReplyDelete
  4. Kwanza pongezi kwa article nzuri kabisa.umeichambua tena kwa mifano hai.Kuna mambo mengi sana umeyaongelea ambayo naweza kusema au kuyaweka kwenye kama sub topics,ambazo ni muhimu sana.Lakni swala la elimu umeligusa kwa mifano hai na weledi mkubwa.

    Nachoweza kusema kwa mtazamo wangu wa haraka haraka.Watanzania wengi hawataki mabadiliko.Viongozi walio wengi nao wanataka watanzania wasifunguke ilimradi mirija na system iwe rahis kwao.

    kwa mfano tu,suala la uraia pacha hichi sio kitu cha kupishana.
    Hiii ni kwa maslahi ya nchi.Mfano wanashangaa kwanin wamarekani watazidi kuwa Super Power miaka mingi ijayo wakati wao sera zao za uhamiaji hazina ubaguzi wala rangi.Kuna watu wengi sana kutoka kila pembe ya dunia wako USA wanafanya kazi au kusoma na marekani wanafaidika sana na hawa brilliant people.Kuna watanzania kila kona ya dunia ambao ni wataalam waliobobea,lakni kwetu wanadharaulika.Sasa tunategemea nani ajenge nchi yetu?mchina?au mwingireza?? watanzania wanashabikia mwekezaji mwekezaji,ilihali hawaeelwi mazingira halisi na jinsi mambo yanavyokwenda.Ilimraid mtu apate 10 percent yake,afiche hela uswis na wapi huko kazi imeisha.


    Kingine,Tanzania kila kitu ni siasa.Mayor mwanasiasa,mkuu wa mkoa mwanasiasa,waziri wa wizara naye mwanasiasa.Kutwa kulalamika nk, hakuna muda wa kuweka jitihada,akili na weledi na ujuzi na katika kujenga nchi.Kila mtu anangalia atakula vip.

    Zaid,nathani kunahitajika reforms mfano serikali inapaswa kupunguza kazi na kugawa kwa sekta binafsi.Tunakuwa na serikali kubwa isiyo na manufaa kwa wananchi na yenye matumizi makubwa.

    Natoa shukurani zangu,natamani kuongea mengi ambayo hayawezi kuisha hapa.Ila napenda kusema nimefurahi kwa uchambuzi wako mfupi na hai na unaoleweka.

    Victor Mbise.

    ReplyDelete
  5. pia kwa kweli ukiangalia nchi kama Amerika, kwa nini inawapa watu uraia? ni kwa sababu wanawachukua kama rasilimali. Nchi kama hii ya Amerika watu wageni wakiondoka nchi itakwisha kabisaaaaaa. Hivyo ni muhimu watu kufikiria saana kwenye hili jambo na sio kuponda tu bila mawazo yanayojenga hoja.

    ReplyDelete
  6. raia pacha my foot !!!

    ReplyDelete
  7. Wataalamu walioko nje wana nafasi nzuri ya kuleta maendeleo nyumbani.

    ReplyDelete
  8. Mashaka na Madiaspora wenzako:

    ''Rasilimali watu na Haki ya Kuzaliwa Tanzania''

    1.Kama mliona umuhimu huo wa Rasilimali watu muda wooote huo huko nyuma mlikuwa wapi kuchangia maendelo ya Tanzania hadi ndio mzinduke sasa hivi?

    2.Kwa nini mnatoa Mashariti ya kupewa Uraia Pacha na Pasipoti ili muwekeze Tanzania, wakati Wawekezaji wengine tunaopokea nchini wakitokea nje hawaweki Sharti la kupewa Uraia?

    3.Mlianza na sababu ya Kigezo cha ''Diaspora Remittances'' na sasa mmehamia ''Human Resources'' baada ya kuona mmezidiwa hoja tena humu humu jamvini kwa Wabishi wa Michuzi!

    Wakati ninyi sio watu baki hapa Tanzania hata kama mmepata Uraia mwingine nje ya TZ mnao unasaba hapa kama wazazi, ndugu na jamaa hivyo kutuma fedha na kutumikia nchi yenu ya asilia Tanzania haihitaji mpaka mpewe Uraia na Pasipoti!

    Bado hoja zenu zooote hazina tija wala mashiko!!!

    ReplyDelete
  9. Hivi ni nini kinachofanya watu wawaogope watu wa Ughaibuni? Mashaka na jamaa kibao wameeleza humu na sehemu nyingine faida ya uraia pacha. Naona jamaa wanaopinga hawana vithibitisho ya vitu wanavyosema. Mfano, mtu anauliza utatuhakikishia vipi kwamba "hamatailetea maafa Tanzania na watu wake?!" Kweli ndiyo swali nalo ilo? Nani anajua kitachotokea kesho? Tanzania inawaitaji sana raia wake wa Ughaibuni, kama watu watakuwa wanatoa mawazo kama haya, ni aibu. Ngoja nifuate maneno ya mkuu JK (nikae kimya), kwani amesema mijadala mingine humu kwenye mitandao ni aina tija.
    Ili swala lipite, lisipite haliwapunguzii kitu nyie jamaa wenye roho mbaya, najua likipita litaongeza kitu kwa TZ.
    *Mmbongo Chiberia*.

    ReplyDelete
  10. mdau namba mbili umegonga point

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...